30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MKAPA: KAGAME WEWE UNASTAHILI


Na ARODIA PETER, ALIYEKUWA KIGALI -

“RAIS Paul  Kagame ni mbunifu, mtengenezaji, mtekelezaji, msimamizi, mkaguzi wa  miradi na mwajibikaji kwa mafanikio ya ajabu aliyoyafikia katika nchi hii ya Rwanda.

Haya ni maneno ya Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamini Mkapa akiuambia Mkutano Mkuu wa wa chama tawala nchini Rwanda, RPF Inkotanyi uliofanyika kwenye makao makuu ya chama hicho eneo la Rusororo kilometa chache kutoka mji mkuu wa  Kigali hivi karibuni.

Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, anasemaRwanda ni nchi anayoendelea kwa kasi na mfano katika kukomesha na kuondosha, unyanyasaji kijinsia na ubaguzi wa kikabila.

Rais huyo Mstaafu ambaye katika utawala wake alisifiwa kwa kusimamia vema uchumi wa Tanzania, anakishauri RPF kumshukuru Rais Kagame kwa utaifa na uongozi wake.

Anasema Kagame ameondosha umasikini na kuleta maendeleo ya kisasa  kwa ajili ya maisha ya watu wote, kuwarejeshea raia wake usawa na heshima na sasa Rwanda inatambuliwa kama kitovu cha kukua kwa biashara ya kikanda na maendeleo ya teknolojia(ICT).

Mkapa ambaye hotuba yake ilikuwa ikishangiliwa kila mara anasema ni jambo la kupendeza katika ulimwengu unaoendelea na kinachoitwa maendeleo.

“Kufikia mambo yote haya ni dhahiri tulielezee taifa hili kama ni lenye roho ya msamaha, roho ya undugu na kazi ngumu iliyofanywa na  wananchi, hata hivyo mafanikio haya makubwa ni tunu ya kuwa na uongozi mzuri.

“Huwa kwa Kiswahili tunasema hivi: Usione vinaelea, vimeundwa ! Endapo utaona gari linatembea ujue limebuniwa na limeundwa.

“Rais Kagame wewe unastahili na kupata heshima ya wananchi wako na wananchi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Afrika”anaeleza Mkapa.

Kagame naye kwa upande wake, ameahidi kuifanya Rwanda kuwa Singapore ya Afrika.

Rais Kagame ambaye amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa RPF Inkotanyi kwa miaka mingine mitano anasema ingawa nchi yake haina raslimali kama zilivyo zingine za Afrika atatumia ubunifu kuimarisha uchumi wao.

Anasema Rwanda ina rasilimali chache za asili, lakini ina mpango wa kugeuka yenyewe kuwa kitovu cha teknolojia ya habari na mawasiliano barani Afrika.

Anasema kuwa tayari Serikali yake imetenga kiasi cha Dola milioni 1.5 za Marekani kwa ajili ya kujenga na kuendesha kiwanda cha kuchakata taka ambacho kitakuwa cha pili kwa ukubwa Afrika kikifuatia kile cha Afrika ya Kusini.

“Kile tunachokisherekea leo hii ni mafanikio ya kizazi hiki. Lakini hatutakiwi kuridhika bali tunapaswa kutafakari cha kufanya leo hii kwa ajili ya manufaa ya kizazi kijacho,”

Ushauri huo wa Kagame ulionyesha kugusa hisia za wanachama, viongozi na wapambanaji wa RPF ambao wanajulikana kama RPF Inkotanyi, wasomi, wataalam na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari wa ndani na nje ya Rwanda.

“Acheni kutumia nguvu katika kutafuta suluhu ya matatizo yetu, hebu tujipe thamani yetu kwa kutumia lugha kama hiyo, hiyo si sehemu ya utamaduni wetu, “Rais Kagame anawahimiza wanachama wenzake.

Hata hivyo Rais Kagame anakumbusha kwamba mafanikio ya mapambano ya kijeshi ya Rwanda na RPF yalikuja na changamoto mpya.

Kwamba baadhi ya wanachama waliiingiwa na  ubinafsi na kudhani kwamba kuna kitu cha ziada wanapaswa kulipwa.

Hata hivyo anasema kulingana na misimamo waliyojiwekea, RPF hakiwezi kuruhusu kuwapo kundi la watu  wa daraja ambalo haliguswi.

Anaeleza kwamba baadhi ya watu wa aina hiyo walijikuta wakitumbukia njia mbaya, sahihi na wengine mpaka sasa wanaishi uhamishoni.

“Wale wote waliopotea na kuamua  kuweka maslahi yao binafsi katika maadili na misingi ya RPF, waliruhusiwa kutumiwa na vikosi vya nje na hawakutaka  tuendelee na tuwe kama tunavyostahili kuwa ,” alichambua Kagame ambaye pia ni mwenyekiti wa RPF Inkotanyi.

Rais Kagame anasema RPF ilifanikiwa kurejeshea heshima Wanyarwanda akisema kuwa tofauti na siku za nyuma ambapo palikuwapo na watu ambao walianza kukata tamaa na wengine kujikuta wakitafuta uraia wa nchi zingine za kigeni na hata kuishia kuwa walinzi katika maduka makubwa nje ya nchi.

Anasema kuwa tayari Serikali yake imetenga kiasi cha Dola milioni 1.5 za Marekani kwa ajili ya kujenga na kuendesha kiwanda cha kuchakata taka ambacho kitakuwa cha pili kwa ukubwa Afrika kikifuatia kile cha Afrika Kusini.

Rais wa zamani wa Benki ya Maendeleo Afrika (ADB), Dk Donald Kaberuka aliwaambia wajumbe wa mkutano mkuu huo kuwa takwimu zinaonesha kuwa nchi za kiafrika ambazo zina rasilimali chache lakini zimekuwa na uwezo mkubwa wa kubuni mbinu ambazo zimezifanya kupiga hatua kubwa za maendeleo.

Dk Kaberuka alizionya nchi za Afrika akisema zinapaswa kujifunza kufanya mambo ambayo huthamini maslahi yao na kuacha kufanya  yale yenye lengo la  kufanikisha ajenda za nchi zenye nguvu za Magharibi.

Msemaji mwingine aliyezungumza katika mkutano huo alikuwa, Dk. Clet Niyikiza, ambaye ni mvumbuzi wa madawa nchini Marekani, yeye alisema Rwanda haipaswi kujiepusha na ubunifu kwa kuogopa kwamba watu wengine wataiba mawazo yao.

“Mtu yeyote ambaye anahofia kulima mazao akiogopa ndege watakuja kuyala kamwe hawezi kuwa na chakula kwa ajili ya watoto wake,” alisema.

Anafafanua kwamba kwa kubaki nyuma kwa woga wa aina hiyo moja kwa moja ni kukwamisha ubunifu na uvumbuzi.

Dk Niyikiza anasema kwamba dawa ya kupambana na tatizo kama hilo ipo katika kuunda sheria nzuri za kuwa na hatimiliki ya kile kilichobuniwa.

“Endapo mmojawapo atakuibia wazo lako mfikishe mahakamani, lakini tusiwe wakarimu wa woga unaweza kupitwa na kila mmoja ambaye unamdharau,” alifafanua zaidi.

Aidha mbunifu huyo wa kimataifa anasisitiza kwamba Wanyarwanda wachanga wanaweza kupata mengi kutokana na hati miliki za mali zao.

Ili kufikia akili ya ubunifu, Dk.  Niyikiza anasema ni lazima mfumo wa utoaji elimu ubadilike.

Kwamba licha ya ufahamu unaotokea katika shule na vyuo vikuu nchi humo kuwa mzuri, lakini vijana wanatakiwa kufikiri jinsi ya kujifunza na wanahitaji kujifunza mengi kutoka kwa wazee.

Kwa sasa barabara za Rwanda ni mpya na safi, majengo mapya yamejengwa na miongoni mwa hayo yamepatikana kutokana na kutolewa kibali cha mtaji binafsi jambo ambalo limewavutia wawekezaji wengi kutoka pembe mbalimbali za dunia na kuamini kwamba watakuwa salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles