ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu Benjamin Mkapa ameelezea namna ilivyokuwa ngumu kuandika kitabu kuhusu maisha yake, kwa sababu hakuwahi kuhisi kuna jambo kubwa la kujifunza kuhusu maisha yake.
Alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa kitabu cha maisha yake kilichozinduliwa na Rais Dk. John Magufuli.
“Haikuwa kazi rahisi kuandika kitabu hiki. Baada ya Taasisi ya Uongozi chini ya mkurugenzi wake Profesa Joseph Semboja kunishawishi, nilisita si kwa kuwa mimi ni mchoyo wa kugawana uzoefu wa uongozi wangu la hasha, ila sikuweza kuhisi kama kuna kubwa la kujifunza kwenye safari hii ya maisha yangu.
“Baada ya mvutano mkubwa, Profesa Semboja akabadilisha mtazamo wangu, kwanza unyeti wa urais kwa heshima kwa kutumikia nchi, kutokana na hili ndiyo maana ni watu wanne (marais wastaafu) ambao wako hai, isipokuwa Mwalimu Nyerere, ambao nao wamehudumu kwa vipindi vyao.
“Nikaona ni vyema kushukuru tunu hiyo kwa kujaribu kuelezea ili wale wenye ndoto ya kuhudumu kwenye nafasi hiyo pamoja na kujifunza juu ya makosa, lakini pia watambue kwamba nafasi ya urais inaweza kushikwa na binadamu yeyote aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu,” alisema Mkapa.
Aidha alisema katika historia yake kuna watu wengi ambao wamechangia kwa njia moja au nyingine, hivyo ameona kitabu hicho kitampa fursa kuwashukuru kwa ujumla wao.
Alisema amekuwa na bahati ya kufanya kazi na Mwalimu Nyerere kwa kipindi kirefu, hivyo ametenga sura nzima kumzungumzia.
“Nimekuwa na bahati ya kufanya kazi na Mwalimu Nyerere kwa kipindi kirefu sana, hii ni bahati adhimu kwenye kunijenga mimi na mtazamo wangu kuhusu masuala mbalimbali binafsi, masuala ya ukombozi wa Bara la Afrika.
“Nimeweza kumwelezea Mwalimu Nyerere kwa mtazamo wangu kama nilivyomjua na hili limenipa faraja sana, nimenufaika sana kuwa na Mwalimu Nyerere kama ‘mentor’ wangu, ni kutokana na sababu hiyo ndiyo maana mmeona kwenye kitabu hiki pamoja na mambo mengine nimetenga sura nzima kumwongelea nilivyomfahamu na kubwa zaidi nini nilichojifunza kutoka kwake.
“Nilijfunza mengi na kuvutiwa sana juu ya uongozi, maono yake kuhusu haki za binadamu na mapenzi juu ya nchi yake,” alisema Mkapa.
Vilevile alisema katika kitabu chake hicho amezungumzia sana umuhimu wa taifa kujitegemea na si kuomba misaada.
“Hii haimaanishi kwamba tusithamini au tusiombe misaada, lakini iombwe kwa ajili kuongeza nguvu kwenye juhudi ambazo tumezianza wenyewe,” alisema Mkapa.
Alisema maisha ya binadamu ni fumbo kubwa kwani baba yake mzazi alimweleza kuhusu maono yake wakati akiwa mdogo.
“Nianze kwa kunukuu maneno ya baba yangu, aliniambia kwamba ‘nataka uwe padre ikishindikana uwe daktari hivyo viwili vikishindikana basi angalau uwe mwalimu’, lakini badala yake leo nimekuwa rais na baba yangu hakuwahi hata kuota kama ningekuwa rais,” alisema.
Mkapa alisema lazima akiri kwamba kuna matukio yalikuwa magumu kuyahadithia na kuyaweka kwenye maandishi, lakini hakuyaacha kwa sababu kiongozi wa kweli anajengwa na matukio hasi na chanya kwenye maisha binafsi na uongozi wa umma.
“Kama binadamu wakati mwingine tunafanya makosa, hivyo vitabu kama hivi vinasaidia kuelezea kwanini ulifikia maamuzi uliyofikia ili viongozi wa sasa na wale watarajiwa waweze kujifunza,”alisema.
Alimshukuru Rais Magufuli kwa kukubali kuzindua kitabu chake na huku akimpongeza kwa msimamo wake wa kuhakikisha Tanzania inajitegemea, hasa katika maendeleo.
Uzinduzi wa kitabu hicho umekwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 81 tangu kuzaliwa kwake.