31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mkapa aeleza anavyoumia kuona wasionacho wakinyanyaswa

Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

RAIS Mstaafu, Benjamin Mkapa, amesema jambo kubwa alilojifunza akiwa mtumishi Serikalini ni kujali watu wa kawaida na kuepuka kuwagawa kwa misingi ya wenye nacho na wasionacho.

Akizungumza juzi wakati wa mahafali ya 15 ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), alisema wahitimu hao wanatakiwa kujitoa kuwatumikia wananchi.

 Aliwataka wahitimu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan kutumia taaluma na ujuzi walioupata kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

“Kama kuna kitu ambacho naamini nimejifunza katika utumishi wangu Serikalini na nje, kitu muhimu ni kumjali mtu wa kawaida. Hakuna kitu kinachonisumbua zaidi ya kuona wale ambao wana kitu kidogo wakinyanyaswa na wale wenye kikubwa.

“Ninyi walimu na madaktari, mustakabali wa nchi yetu unategemea ubora wa elimu mtakayotoa kwa vijana wetu. Inategemea uwezo wako wa kuzuia shida zisizohitajika na kuwarudisha wagonjwa kwenye afya, furaha na tija,” alisema Mkapa.

Katika hotuba yake Mkapa alirejea misingi mbalimbali ya utawala wa Mwalimu Nyerere akisema kwa kufuata nyayo za kiongozi huyo kumemsaidia kuwa mfano bora.

“Miongoni mwa mambo muhimu ambayo nimejifunza kutoka kwa Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) ni umuhimu wa kushauriana na kusikiliza kwa uangalifu kabla ya kufanya maamuzi.

“Wakati wowote alipokabiliwa na suala kubwa, alitafuta mitazamo anuwai. Nimejaribu kila wakati kufuata mfano wake na maamuzi yangu bila shaka yamekuwa bora zaidi,” alisema.

Naye Rais wa Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Firoz Rasul, alisema chuo hicho kimeendelea kufanya vyema na kwamba mwaka jana kilikuwa ni miongoni mwa vyuo 100 duniani katika upande wa kozi za udaktari.

Alisema mpaka sasa karibu watu 1,200 wamehitimu katika chuo hicho hapa nchini wakiwamo walimu, waganga, wajasirimali, watumishi wa umma na watunga sera.

Rais huyo alisema pia upanuzi wa Hospitali za Aga Khan na vituo vya afya katika maeneo ya pembezoni nchini utawezesha kutoa huduma kwa watu zaidi ya milioni moja kila mwaka.

Kwa mujibu wa Rasul, uwekezaji mwingine katika sekta ya afya ni ule uliofanywa kupitia Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) na Shirika la Maendeleo ya Ufaransa (AFD), uliogarimu Sh bilioni 192.

Mmoja wa wahitimu wa Shahada ya Uzamili katika Elimu, Mwalimu Mpendwa Milanzi, alisema mafunzo aliyoyapata yatamuongezea umahiri katika mbinu za ufundishaji na kumpa uwezo wa kutafuta maarifa zaidi ambayo hayapatikani kwenye vitabu.

Katika mahafali hayo wahitimu 21 walitunukiwa shahada ya uzamili katika elimu na watano walitunukiwa shahada ya uzamili ya udaktari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles