
NA RAYMOND MINJA, IRINGA
MSANII anayefanya vyema katika muziki wa kizazi kipya kutoka Iringa, Junaisaty Daimond (Junay), amesema anaendelea kushangazwa na mkali wa hip hop nchini, Emanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, kutokuomba radhi hadi leo kwa wasanii na mashabiki wa wasanii aliowatukana katika wimbo wake wa ‘Shika Adabu yako’.
Msanii huyo alisema kitendo cha kuwasema vibaya wasanii wenzake ndicho kinachoshusha muziki wa Nay wa Mitego kwa kuwa hajali heshima kwa wenzake na maisha ya watu wanaomzunguka kwa ujumla.
Msanii huyo anayetamba na wimbo wake wa ‘Changanyachanganya’, alisema kila mtu ana maisha yake aliyoyachagua kuishi ili mradi hamkeri mtu na kwamba hakuna haja ya kumdisi au kumdhalilisha mwingine kwa kuwa tu una sehemu ya kusemea .
Junay alisema licha ya msanii huyo kuwa na jina kubwa katika medali ya muziki, yampasa kuomba radhi kwa kuwa aliwaudhi wasanii hao pamoja na mashabiki wao.
“Kumekuwa na tabia ya wasanii kuwasema wenzao vibaya kupitia muziki au watangazaji wanaowafahamu, ni vyema kila mmoja aheshimu uhuru na mawazo ya mtu kwani kila mtu ana haki ya kuishi jinsi anavyotaka ili mradi havunji sheria za nchi,” alieleza msanii huyo.