27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Mjumbe Bunge la Katiba apigia kura wodini

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba aliyepigwa na watu wasiojulikana, Thomas Mgoli
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba aliyepigwa na watu wasiojulikana, Thomas Mgoli

NA ESTHER MBUSSI, DODOMA

MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba aliyepigwa na watu wasiojulikana, Thomas Mgoli, amepiga kura akiwa wodini katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikolazwa.

Mgoli alipiga kura jana akiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati namba 12, Thuwaibay Kissassi.

Alipiga kura ya wazi kwa kuzipigia kura ya ndiyo sura ya pili hadi ya tano isipokuwa ibara ya 59.

Akizungumza baada ya kupiga kura, ni kwanini aliikataa ibara ya 59 ambayo inapendekeza mfungwa ambaye ni mlemavu kuingia mahabusu au jela na magongo yake, Mgoli alisema yanaweza kutumika kama silaha.

“Nimeikataa kwa sababu mlemavu ni mtu asiyejiweza, unapomruhusu kuingia na magongo yake mahabusu, wababe wa huko wanaweza kumnyang’anya na kuyatumia vibaya kumjeruhi au kujeruhi wengine,” alisema.

Mgoli ambaye bado amelazwa hospitalini hapo, alisema ameamua kupiga kura akiwa mgonjwa kwa sababu ni haki yake ya msingi na ya kisheria, na pia alikuwa ameshashiriki sehemu ya majadiliano hayo.

“Sikutaka wengine waniamulie, najua kura yangu moja tu inaweza kubadilisha kila kitu, ndiyo maana nikaomba kupiga nikiwa hapa katika hali hii. Kabla ya kupiga kura, niliandaliwa kisaikolojia, kwa hiyo uamuzi niliofanya ni wangu, sijashurutishwa na mtu yeyote,” alisema Mgoli.

Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel, ambaye alikuwapo hospitalini hapo pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati namba 12, alisema mjumbe huyo aliomba kupiga kura akiwa hospitali.

“Aliomba kupiga kura na kwa sababu ni haki yake, tulichokifanya kwa sababu yuko nje ya eneo, tuliomba tuwe na waangalizi kutoka Bunge la Jamhuri, Baraza la Wawakilishi na wajumbe wa kamati yake,” alisema.

Mgoli alipigwa na watu wasiojulikana mwanzoni mwa wiki hii maeneo ya Area A.

Kwa mujibu wa maelezo yake, aliwatambua watu hao kuwa ni wafuasi wa chama fulani cha siasa kutokana na jinsi walivyokuwa wamevaa.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia watu watatu kwa mahojiano huku likiendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles