Na Esther Mbussi, Dodoma
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Thomas Mgori, amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Dodoma, baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Tukio hilo lilitokea juzi saa mbili usiku, eneo la Area A, ambako watu hao walimshambulia kwa mawe na kumjeruhi shingoni, taya na miguuni.
Akisimulia mkasa huo jana, Mgori, ambaye ni Mjumbe kutoka Kundi la 201, alisema siku ya tukio alikuwa na watu hao katika baa ya jirani na nyumba aliyopanga ambao walimuuliza hatua yake ya kutounga mkono msimamo wa UKAWA.
“Mara nyingi wamekuwa wakiniuliza kwa nini siiungi mkono UKAWA na uhalali wangu wa kuwepo bungeni wakati UKAWA hawapo, wakasema hawatakubali.
“Sasa juzi ndiyo nikasema niwaeleze sababu, wakasema haiwezekani, wakaanza kunipiga kwa jiwe likanipata shingoni, wakati nakimbia nikaanguka katika mtaro nikasaidiwa na watu kwenda polisi,” alisema.
Mjumbe huyo kutoka kundi la vyama vya siasa aliwataja wafuasi wa chama kimoja cha siasa kuwa wanahusikana na mpango huo wa kumpiga.
Hata hivyo, alipoulizwa aliwatambuaje watu hao kuwa ni wafuasi wa chama hicho, Mgori alisema hana shaka na kauli hiyo kutokana na watu hao kujitanabahisha kwake ambao walikuwa na mavazi ya magwanda ambayo ndio utambulisho wa chama hicho cha siasa.
Alisema mmoja wa watu hao aliyetambulika kwa jina la ‘Vampire’, alishawahi kukutana naye zaidi ya mara sita na mwingine ambaye hakumtambua jina lake, walishakutana mara mbili isipokuwa wengine ilikuwa ni mara ya kwanza kuwaona.
“Nilizoeana nao kwa muda mfupi kwa sababu nilichukulia kama sehemu ya utamaduni wetu Watanzania kushirikiana, sikudhani kama tungeweza kufikia huko.
“Siwezi kusema kwamba ni wafuasi CCM, kwa sababu wao wanataka wajumbe waingie bungeni, sasa inawezekana vipi wanipige kwa kuingia bungeni?” alihoji.
Akizungumza hospitalini hapo, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, aliwataka wajumbe hao kuwa makini na watu wanaokutana nao wawapo nje ya Bunge.
Sitta alisema kama kweli ni wafuasi wa chama hicho cha siasa wamempiga mjumbe huyo, lazima wachukuliwe hatua kama wahalifu wengine na kwamba ifike mahali UKAWA na Watanzania wengine wakubali kutofautiana kimtazamo.
“Wanataka kuzuia mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya, lakini watambue sisi tuko hapa kwa mujibu wa sheria na Katiba itakayotoka itakuwa bora kuliko iliyopo.
“Pia wajumbe tuwe makini na mijadala tunayokuwa nayo tuwapo nje ya Bunge, tuzungumze kwa hoja siyo kugombana, kwa niaba ya Bunge Maalumu la Katiba, nampa pole Mgori na tunashukuru Mungu hakupata madhara zaidi,” alisema Sitta.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel, ambaye pia alimtembelea hospitalini hapo, alisema kama hali imefikia huko ni hatari zaidi.
“Kama kweli ni wafuasi wa chama cha siasa wametenda haya, nadhani kuna tatizo kubwa kwa sababu huu ni uadui,” alisema.
Daktari bingwa wa upasuaji wa hospitali hiyo, Dk. Ibenzi Ernest ambaye anamhudumia Mgori, alisema kwa sasa anaendelea vizuri, isipokuwa ana maumivu ya nyama tu, kwani kipimo cha X-Ray kinaonyesha hakuvunjika mfupa au mshipa wowote.
“Kwa sasa anasubiri kipimo kimoja cha taya, akishafanya hicho anaweza kuruhusiwa hata leo (jana),” alisema.
Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Mzee Nassoro, alisema wamempokea mgonjwa huyo na anaendelea vizuri.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema hadi sasa wanawashikilia watu watatu kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.
“Ni kweli tukio hilo lilitokea juzi baada ya Mgori na wenzake kutofautiana kimtazamo wakiwa katika baa moja maeneo ya Area A, ambapo walimhoji kwa nini haiungi mkono Ukawa na yeye kabla ya kujieleza wakampiga.
“Tunaendelea na uchunguzi wetu kwa kuwahoji watu hao watatu ambao wote ni wanaume, huku tukiendelea kuwatafuta wengine,” alisema Kamanda Misime.
Watu wengine waliomtembelea Mgori ambaye ni Mjumbe wa Kamati namba 12 ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Mwenyekiti wa Kamati namba 12, Paul Kimiti na Mjumbe wa Kamati hiyo, Doreen Maro.
KAFUMANIWA NA MKE WA MTU .AACHE KUKICHAFUA CHAMA KWAMBA KINAUSIKA NA KUPIGWA KWAKE WAKATI ALIKUWA KWENYE POMBE.