27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

MJANE ALIYEIBUKA KWA MAGUFULI ASHINDWA KESI

Na Amina Omari – Tanga

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tanga imetupilia mbali rufaa ya kusikiliza upya shauri la mirathi ya marehemu Mohammed Shosi lililofunguliwa na Swabaha Mohamed Ali.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Swabaha aliyedai kuwa ni mke wa marehemu Shosi, aliibuka mbele ya Rais Dk. John Magufuli wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria na kulalamika kutaka kudhulumiwa haki yake ya mirathi.

Rufaa hiyo uamuzi wake ulitakiwa kutolewa kesho, lakini hata hivyo ulitolewa juzi na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Amour Hamis.

Katika kesi hiyo ambayo Swabaha aliifungua dhidi ya Saburia Shosi, ambaye ni mtoto wa marehemu Shosi aliyeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu baba yake, Jaji Amour akitoa uamuzi alisema mahakama hiyo imeridhika na hukumu iliyokuwa imetolewa hapo awali na mahakama ya wilaya pamoja na ile ya mwanzo.

Katika hilo, jaji huyo aliamuru taratibu nyingine za uendeshaji wa mirathi kuendelea kama ilivyokuwa imeamuliwa na mahakama ya mwanzo na ile ya wilaya.

Katika kesi iliyofunguliwa na Saburia katika Mahakama ya Mwanzo Desemba 16, 2012, kuomba awe msimamizi wa mirathi, mahakama hiyo ilimruhusu.

Hata hivyo, mwaka 2015 Swabaha alikata rufaa Mahakama ya Wilaya akifungua kesi ya kuzuia mali za marehemu, ambayo nayo upande wa akina Saburia walishinda huku mahakama ikimuamuru aendelee kuwa msimamizi wa mirathi.

Katika umuzi wake wa sasa, Jaji Amour alisema kuwa pamoja na hukumu hiyo, Swabaha ambaye alikuwa akiwakilishwa na wakili wake Ngomela, atatakiwa kumlipa Saburia gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo.

Awali Jaji Amour alisema kuwa Swabaha aliwasilisha mahakamani hapo ombi la kukata rufaa nje ya muda baada ya kesi ya msingi kumalizika na hukumu kutolewa.

Aidha alisema kuwa kesi ya msingi ilitolewa uamuzi katika Mahakama ya Wilaya Septemba 9, 2016 na Swabaha alikuja kukata rufaa nje ya muda, Novemba 14, 2016.

Akizungumza mara baada ya hukumu hiyo, Saburia ambaye alikuwa akitetewa na Wakili Abdon Rwegasira, aliipongeza mahakama kwa kumaliza mapema shauri hilo ambalo lilikuwa likiwasumbua kwa muda mrefu.

Saburia ambaye anadai kuwa ni miongoni mwa watoto tisa wa marehemu Shosi, alisema hukumu ya kesi hiyo ilipangwa kutolewa kesho, lakini juzi akiwa nyumbani alipigiwa simu kwamba anahitajika mahakamani.

“Nilipigiwa simu kama saa nne hivi nikiambiwa nahitajika mahakamani, basi tukaenda, huwezi kujua pengine ndio mambo ya tume aliyosema rais, tukaambiwa kesi yetu inatolewa uamuzi na tunashukuru Mungu tumeshinda,” alisema.

Saburia ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya familia yake, alisema kwa uamuzi huo sasa wataweza kuendelea na taratibu nyingine za mirathi.

“Nimefurahishwa sana na uamuzi wa mahakama kwani haki imeweza kutendeka kwa wakati na sasa tunaweza kuendelea na mambo ya kugawana mali za marehemu baba,” alisema Shosi.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Swabaha ili kuzungumzia uamuzi wa kesi hiyo na alisema ameupokea vizuri na kwamba kwa sasa anajiandaa kupeleka maombi Mahakama Kuu kufanya mapitio (review) ya hukumu mbili zilitolewa katika Mahakama ya Mwanzo na ile ya Wilaya.

“Yalikuwa ni maombi ya kuingia kwenye rufaa na actually tulikuwa tumechelewa kukata rufaa, sasa ni nafasi ya mahakama kuangalia hukumu zile mbili, nitakwenda Tanga kati ya Jumatatu (kesho) au Jumanne (keshokutwa) kupeleka maombi hayo,” alisema Swabaha.

Mjane huyo pia alikwenda mbali na kumtaja kwa jina askari mmoja (jina tunalihifadhi kwa sasa kwa sababu za kitaaluma), kwamba katika siku za hivi karibuni amekuwa akimfuatilia kumchunguza.

“Nashangaa alikuwa wapi muda wote, nimesikia amekwenda hadi Bakwata kufuatilia cheti cha ndoa yangu, na wakati alikwisha kwenda siku za nyuma, si hilo tu, amekwenda hadi Buguruni, sasa mimi nina uthibitisho wa kila kitu,” alisema Swabaha ambaye anadaiwa alifunga ndoa nyingine Buguruni.

Kabla ya uamuzi wa sasa, Februari 4, mwaka huu, siku moja baada ya mama huyo mjane kutoka mkoani Tanga kuibuka mbele ya Rais Magufuli na kudai kudhulumiwa haki yake ya mirathi na vyombo vya sheria, gazeti hili lilizungumza na pande mbili zinazovutana katika sakata hilo la mirathi kabla ya baadae kufika yalikokuwa makazi ya marehemu Shosi Mohamed ambaye Swabaha anadai kuwa ni mume wake mkoani Tanga.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili baada ya kusambaa kwa andiko lililokuwa likieleza upande wa pili wa ‘mama huyo mjane’ likimtuhumu kama tapeli ambalo liliandikwa na rafiki wa karibu wa familia hiyo, mtoto wa marehemu Shosi, Saburia alisema madai yote yaliyotolewa na mama huyo mjane si ya kweli na hivyo kutamani Rais Magufuli asikilize upande wa pili unaotuhumiwa wa familia hiyo.

Saburia ambaye alizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, kwa simu na baadae nyumbani kwao Tanga, alianza kueleza jinsi anavyomfahamu mama huyo mjane akisema ni dada yake na kwamba marehemu baba yake alikuwa akimwita mjomba.

“Simfahamu kama mke wa marehemu baba, namfahamu kama dada, mama yake mzazi na baba yangu (Shosi) ni mtoto wa mkubwa na mdogo na kwa kabila letu Wagunya, aliyepaswa kuolewa na baba yangu ni mama yake ambaye ni shangazi yangu na si yeye,” alisema.

Saburia alisema baba yake alioa wake watatu ambao ni Mariam Tayb ambaye ni mama yake mzazi aliyekuwa amezaa watoto saba, lakini walio hai ni wanne, Mariam Sadick anayeishi Mkumbara Korogwe na Methe Mwanga ambaye kwa sasa ni marehemu.

“Kwa kifupi sisi tulikuwa hatumfahamu kabisa, tulimfahamu siku ya 40 baada ya baba kufariki na alikuwa amekuja kutupa pole tukiambiwa kuwa ni ndugu yetu kutoka Mombasa, sasa wakati tunaandaa muhtasari wa kikao tukashangaa anasema aliolewa na baba yetu.

“Hebu jiulize, anasema baba alimuoa mwaka 1993, mwaka 2011 alikuwa Buguruni, Dar es Salaam eda baada ya kufiwa mume wake mwingine aliyekuwa akiishi naye huko, mwaka 2013 alikuwa anafuatilia mirathi ya huyo mume wake wa Buguruni, sasa mwanamke anawezaje kuolewa na watu wawili kwa wakati mmoja?” alihoji Saburia.

Wakati akisema hayo, mama huyo mjane alikaririwa pia na vyombo vya habari akidai kuwa Saburia ni mtoto wa nje wa marehemu mume wake na kwamba amekuwa akitumia nguvu yake ya pesa za dawa za kulevya kutaka kumpora haki yake, jambo ambalo mtoto huyo wa marehemu amekuwa akilipinga.

Akizungumza na gazeti hili, Swabaha ambaye mara ya kwanza alikataa kueleza kuhusu ndoa yake ya Buguruni, jana alikuwa tayari kueleza kuhusu jambo hilo.

Alikiri alikuwa akishughulika na mirathi ya Buguruni, lakini alikana kwamba mtu huyo haliwahi kuwa mume wake.

“Ni kweli nilikuwa nashughulika na mirathi ya Buguruni kwa sababu marehemu huyo nilikuwa nikimdai shilingi milioni 8.6,” alisema.

Wiki kadhaa zilizopita gazeti hili lilifika yalikokuwa makazi ya marehemu Shosi, mkoani Tanga jirani na Hospitali ya Rufaa ya Bombo na kuzungumza na Marium Tayb ambaye anadai kuwa ni mke mkubwa wa marehemu.

 Nyumba hiyo anayoishi Tayb kila upande unakiri kuwa yalikuwa ni makazi ya marehemu na shughuli zote za maziko zilifanyika hapo.

 “Najua marehemu aliwahi kuoa wake watatu, lakini hakuwahi kusema kama ameongeza mke mwingine na kama angekuwa ameolewa tungeweza kujua kwani tungetambulishwa kwake,” alisema.

Tayb alisema sakata la Swabaha kudai mirathi hiyo lilianza mwaka 2012 wakati wa kikao cha arubaini ya marehemu mumewe wakati wakili wao alipowasilisha nyaraka ya mirathi.

Alisema Swabaha ambaye alikuwapo kwenye kikao hicho alijitambulisha kama mpwa wa marehemu na baada ya kusomwa wosia wa marehemu aliomba auone kwa ukaribu ili ajiridhishe na kilichoandikwa.

“Alipopewa akasimama na kusema na yeye ni mke halali wa marehemu, hivyo anastahili kurithi mali za marehemu kwani na yeye ana haki na kisha kukimbia na wosia huo,” alisema Tayb.

Alisema walijaribu kumfuatilia kupitia kwa ndugu pamoja na wazazi wake wanaoishi Mombasa kuomba arudishe wosia huo, lakini badala yake alikataa na kuamua kuwapa kopi.

Tayb alisema kuwa ilipofika Desemba, 2012  Swabaha aliamua kufungua kesi ya kudai mirathi na kuweka zuio la mali zote za marehemu.

Februari 4, mwaka huu, Rais Magufuli aliagiza mama huyo mjane apewe ulinzi, huku akimwagiza Jaji Kiongozi kuhakikisha analifuatilia suala lake na kulimaliza kwa taratibu za kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles