Mwandishi Wetu -Arusha
SHUGHULI za biashara na uingizaji mizigo hazijazuiwa katika mpaka wa Namanga kwa nchi za Tanzania na Kenya.
Kutokana na hali hiyo sasa madereva watakaoingia nchini Kenya kupeleka mizigo watatakiwa kupima corona kwanza na pindi wakibainika hawana maambukizi ya ugonjwa huo wataruhusiwa kupita na kupeleka mizigo katika nchi husika.
Mei 13, madereva 23 ambao ni raia wa Tanzania , mmoja wa Uganda na mmoja kutoka taifa la Rwanda walizuiwa kuingia nchini Kenya baada ya kukutwa na virusi vya corona.
Kwa mujibu wa wizara ya afya nchini Kenya madereva hao walipimwa na kupatiwa majibu yao katika kipindi cha saa 24 kwenye mpaka wa Namanga.
Serikali ya Kenya imesema kwamba hatua ya kuzuia madareva hao kuingia nchini humo inalenga kuwalinda Wakenya dhidi ya maambukizi kutoka kwa raia wa kigeni.
Katika mkutano wake na wanahabari Katibu Tawala wa Waziri wa Afya, Rashid Aman aliongezea kwamba maabara mbili za kuhama hama zitazinduliwa katika mpaka wa Namanga ili kuimarisha upimaji wa wagonjwa wapya.
Juzi Kenya ilimetangaza kufunga kwa muda wa siku 30 mipaka yake ya kimataifa na nchi za Tanzania na Somalia kuanzia juzi lakini ikiruhusu uingizaji wa mizigo na shughuli za biashara.
Akilihutubia taifa lake, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alisema hatua hiyo inajumuisha udhibiti usafiri wa watu kutoka mataifa hayo kuingia nchini Kenya.
Alisema watu hawataruhusiwa kusafiri kuingia au kutoka Kenya kwenda Tanzania na Somalia.
Hatahivyo alisema usafirishaji wa mizigo utaendelea kati ya Kenya na mataifa hayo mawili.
Na kwa upande wa Somalia masharti ni hayo hayo, mizigo peke yake ndio itakayoruhusiwa.
Aidha Rais Kenyatta alisema madereva watakaoingia nchini Kenya kwa ajili ya kupeleka mizigo watatakiwa kupimwa corona kwanza.
Alisema madereva watakaobainika wameambukizwa virusi vya corona hawataruhusiwa kuingia Kenya.
Rais Kenyatta pia ameongeza muda wa watu kutoka nje wa kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja asubuhi hadi Juni 6,2020.
Pia Kenya imeongeza tena muda wa marufuku ya kutoka nje kwa muda wa siku 21 baada ya ule wa awali kuisha juzi.
Kufikia sasa idadi ya watu walioambukizwa na virusi vya corona nchini Kenya imeongezeka hadi 830 baada wagonjwa wapya 49 kuthibitishwa kuwa na ugonjwa huo.
Waliofariki kutokana na corona ni watu 50 baada ya wengine watano kufa.
Rais Kenyata pia ametangaza kuwa wagonjwa 17 wametolewa hospitalini walipokuwa wakipata matibabu.
“’Najua Wengi wanataka maisha yarudi kama vile ilikuwa lakini wenzagu sitaki niwadanganye. Jukumu la kwanza la serikali ni kulinda maisha ya Wakenya,” alisema
Marufuku ya usafiri kuingia na kutoka miji mitano ikiwemo Nairobi, pia imeongezwa kwa siku 21.
Katika hilo Uhuru ameongeza muda hadi Juni 6 kufungwa kwa mipaka ya eneo la kibiashara la Nairobi, kaunti ya Mombasa, Kilifi, Kwale na Mandera.