23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

‘Miswada sheria za mchakato wa katiba ipelekwe bungeni’

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) limeiomba Serikali kuangalia upya muda uliotangazwa wa kutoa elimu ya katiba kwa miaka mitatu badala yake ipeleke miswada ya sheria za mchakato wa katiba bungeni kwa ajili ya marekebisho.

Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Bob Wangwe, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mchakato wa katiba mpya.

Jukwaa hilo pia limetoa sheria mbili za mfano yaani ya marekebisho ya katiba na sheria ya mfano ya kura ya maoni na nyaraka zinazotoa sifa za upatikanaji wa kamati ya wataalamu.

Akizungumza Agosti 31,2023 na Waandishi wa Habari, Mwenyekiti wa Jukata, Dk. Ananilea Nkya, amesema utoaji elimu ulishafanywa na iliyokuwa Tume ya Marekebisho ya Katiba.

“Tunapendekeza Serikali kuachana na mpango wa kutoa elimu ya katiba ya mwaka 1977 kwa miaka mitatu na badala yake ipeleke miswada ya sheria za mchakato wa katiba bungeni kwa ajili ya marekebisho.

“Tunatoa wito kwa Waziri Pindi Chana (Waziri wa Katiba na Sheria) kutoa ratiba ya hatua za mchakato wa katiba mpya ili kuondoa sintofahamu ambayo imetawala miongoni mwa wadau wa katiba na Watanzania kwa ujumla,” amesema Dk. Nkya.

Kuhusu sheria za mfano amesema zimeainisha namna migogoro inavyoweza kutatuliwa na kusimamiwa katikati ya mchakato.

Aidha imependekeza masuala ya kibajeti na vitu vinavyoweza kufanyika katika hatua za mpito wa nchi kupata katiba mpya.

“Serikali ione umuhimu wa kutumia nyaraka hizi katika kutunga au kurekebisha sheria za mchakato wa katiba kwani zimezingatia mahitaji ya sasa ya nchi pamoja na uzoefu wa mchakato uliokwama mwaka 2014,” amesema.

Naye Mjumbe wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba, amesema kinachotakiwa kufanywa ni mazungumzo na kazi za kitaalamu ili katiba ipatikane kwa wakati.

“Wasaidizi ambao wanakuwa uwezo wao ni mdogo wanaweza kukwamisha mchakato huu, presha ambayo inahitajika ni mazungumzo na kazi za kitaalamu.

“Jukwaa la Katiba msimamo wetu ni kwamba hakuna haja ya mchakato kuanza miaka miwili ijayo, uanze sasa lakini waziri atoe ratiba,” amesema Kibamba.

Mkurugenzi wa Jukata, Bob Wangwe, amesema “Tunahitaji kupata ratiba ya utekelezaji wa hatua za mchakato, tulivyokuwa tunafahamu hapo nyuma baada ya rais kutoa agizo kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuratibu wadau ili kuanza mchakato, lakini tumeshangaa tena waziri anasema watatoa elimu ya katiba ambayo tumesema ina mapungufu kwa muda wa miaka mitatu,” amesema Wangwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles