Na Jeremia Ernest, Mtanzania Digital
SHIRIKA la DKT Tanzania limefanya hafla ya ambayo imekutanisha wadau mbalimbali wa uzazi wa mpango katika ofisi zake zilizoko Masaki, Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii.
Tukio hilo lilikuwa na nia ya kubadilishana mawazo juu ya namna ya kukabiliana na mahitaji ya uzazi wa mpango nchini, lilihudhuriwa na Mashirika mengine kama Engender Health, UMATI, Medicins Du Monde pamoja na wadau mbalimbali akiwamo Miss Tanzania 2022, Halima Kopwe.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Mkuu wa Masoko wa DKT Tanzania, Deogratius Kithama, amesema shirika hilo limejikita kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya uzazi wa mpango kwa urahisi hapa nchini.
“Shirika letu limejikita katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za uzazi wa mpango wa kama Kiss condoms na vidonge vya majira vya Trust Daisy ambavyo vinapatikana kwa bei nafuu ambayo mwananchi wa hali ya chini anaweza kuvimudu,” amesema Kithama.
Kwa upande wake Miss Tanzania 2022/23, Halima Kopwe amezungumzia umuhimu wa kuongeza elimu juu ya afya hususan kwa vijana ambao wapo chini ya miaka 18 na bado wapo masomoni.
“Elimu hii ya uzazi wa mpango inahitajika kuwafikia vijana walio shuleni sababu ya kuepusha mimba zisizotarajiwa pia wasichana wengi wamekuwa wakipoteza maisha wakati wa kujifungua,” amesema Kopwe ambaye ni muanzilishi wa mradi wa Afya ya Mama na Mtoto.
Serikali ya awamu sita imekuwa ikiongelea juu ya umuhimu wa uzazi wa mpango, hasa baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hasani kuelezea umuhimu wa “kupunguza spidi kwenye uzazi”