28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

MISHAHARA, MADENI YATAFUNA TRIL. 1 KILA MWEZI

Na FREDY AZZAH-DODOMA


SERIKALI imesema inakusanya Sh trilioni 1.3 kwa mwezi ambazo kati yake Sh bilioni 550 hulipa mishahara, Sh bilioni 600 hulipa deni la taifa na kiasi kinachobaki kinapelekwa kwenye miradi ya maendeleo.

Hayo yalisemwa jana mjini hapa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kutoa ripoti yake ikionyesha malengo ya makusanyo ya Serikali yanafikia asilimia 94, lakini fedha za maendeleo zinazotolewa ni takribani asilimia 50.

Dk. Mpango pia alijibu hoja ya CAG iliyosema si busara kuangalia kigezo cha pato la taifa dhidi ya deni la taifa ukasema unaweza kuendelea kukopa, akisema kwa vigezo vyote Tanzania iko vizuri kuendelea kukopa.

 

FEDHA ZINAVYOTUMIKA

Akizungumzia matumizi ya fedha zinazokusanywa kutokana na kodi, Dk. Mpango alisema: “Kwahiyo maana yake kwenye trilioni 1.3, umebakiwa na bilioni 200 ambazo ndizo hizo unatumia kuendesha Serikali.

“Lakini humo namo kuna shughuli nyingine ambazo hazikwepeki, kwa mfano askari wetu shupavu wanalala nje, lazima Serikali tuwape posho ya chakula, ndiyo sisi tunaweza tukaendelea na vurugu huku bungeni tukabishana, tukala nyumbani kwa amani.

“Kuna mishahara ya majaji lazima ilipwe na marupurupu yao mengine, kuna viongozi wetu nao hawalali. Niwahakikishie ni kawaida kabisa kumpigia Rais (John Magufuli) simu saa nane, saa tisa yuko macho, hawa viongozi wamebeba dhamana kubwa, lazima Serikali iwahudumie.

“Kwahiyo unaponiuliza hizi nyingine zinaenda wapi, naweza nikaendelea na kuendelea.”

Awali Dk. Mpango alisema Serikali ya awamu ya nne ilikuwa inakusanya Sh bilioni 850 kwa mwezi, lakini tangu Serikali  ya awamu ya tano kuingia, imekuwa ikikusanya wastani wa Sh trilioni 1.

“Kwahiyo ni rahisi sana kuhesabu hicho kinachoingia mfukoni, lakini ni muhimu kuangalia hicho kinachotoka, zinatoka zinakwenda kwenye nini,” alisema Dk. Mpango.

“Ulipaji wa deni la taifa inategemea, kwa mwezi inaweza ikatoka kati ya Sh bilioni 600, tumewahi kwenda mpaka Sh bilioni 900, kutegemea na hayo madeni yanaiva wakati gani.

“Mwezi huu unaweza ukalipa Sh bilioni 600 na kidogo, mwezi ujao ukalipa Sh bilioni 700, ni kwa sababu ya tofauti ile mikopo inaiva wakati gani.

“Ukichukua wastani wa Sh bilioni 550 mishahara, ukaongeza Sh bilioni 600 kwa ajili ya kulipa deni, tayari Sh trilioni 1.1 umeitumia kwa hivyo vitu viwili ambavyo huwezi kukwepa,” alisema Dk. Mpango.

 

UWEZO WA KUKOPA

Akijibu hoja ya CAG aliyesema si busara kuangalia kigezo cha pato la taifa dhidi ya deni la taifa na kusema unaweza kuendelea kukopa, Dk. Mpango alisema: “Tunapofanya tathimini ya uhimivu wa deni la taifa, uwiano tunaouangalia si deni kwa pato la taifa peke yake.

“Tunaangalia vigezo vingi sana, kwa kuangalia hivyo vigezo vingi vya kimataifa, taifa letu lina uwezo kabisa wa kuendelea kukopa. Si kwa kuangalia mwenendo na deni na pato la taifa peke yake, takwimu nilizonazo ni current (za karibuni), CAG yeye ameishia Juni 2017, sisi tulifanya tathmini ya uhimilivu wa deni Novemba 2017.

“Thamani ya sasa ya deni la taifa, kwa pato la taifa ni asilimia 34.4, ukomo wake kimataifa ni 56 asilimia, kwahiyo hapo tuko vizuri.

“Thamani ya sasa ya deni la nje peke yake kwa pato la taifa ni asilimia 19.7 ukomo asilimia 40 kimataifa, alafu tunaangalia thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje, ni asilimia 81.8, ukomo ni 150 asilimia.

“Thamani ya sasa ya deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 117. 1,  ukomo kimataifa ni asilimia 200, sasa mnaona kwa viashiria vyote hivyo, hatuangalii tu deni kwa pato la taifa, tunaangalia pia mpaka uwezo wa mapato ya ndani wa kulipa hilo deni.

“Tunaangalia vigezo vyote hivyo ndiyo tunafika tunasema kwa viashiria vyote hivyo vinne ambavyo vinapima uwezo wa nchi kukopa, Tanzania tuko vizuri kabisa,” alisema Dk. Mpango.

Alisema pia ullipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani umefikia asilimia 13.3 ukilinganisha na ukomo wa asilimia 20 za ulipaji deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje.

 

HOJA YA CAG

Juzi Profesa Assad akizungumzia deni la taifa, alisema limefikia Sh trilioni 50 na kwamba ni vyema kama nchi ikakopa kwa tahadhari ili isirudi nyuma miaka 20 ambako ilisamehewa sehemu ya deni.

Alisema hadi kufikia Juni 30, 2017, deni hilo lilikuwa Sh trilioni 46.08 kutoka Sh trilioni 41.03 za Juni 2016, ikiwa ni ongezeko la Sh trilioni 5.04 sawa na asilimia 12.

Profesa Assad alisema deni la ndani ni Sh trilioni 13.33 na deni la nje ni Sh trilioni 32.75.

Alisema katika deni hilo, kuna Sh trilioni 4.58 ambazo hazikujumuishwa kutokana na kutojumuishwa kwa madeni ya mifuko ya pensheni na dhamana ambazo masharti yake yalikiukwa na kwamba kwa ujumla wake deni hilo ni Sh trilioni 50.

 Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,307FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles