23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Miradi ya umeme kimkakati 2025 yatajwa

Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dk. Tito Mwinuka ameeleza kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo inalenga kutimiza adhma ya Serikali ya kuwa na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

Taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo ameitoa leo Jumatano Oktoba 23, katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika jijini Dodoma ambapo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliiongoza Wizara ya Nishati katika uwasilishaji wa taarifa hiyo akiwa ameambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Hamisi Mwinyimvua na Menejimenti ya Wizara pamoja na Taasisi zake.

“Wizara ya Nishati kupitia TANESCO inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya umeme ikiwemo ya kuzalisha umeme, usafirishaji umeme katika msongo mkubwa na usambazaji lengo likiwa ni kukidhi mahitaji ya umeme yanayoongezeka  na miradi hii itakapokamilika itachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya umeme.” amesema.

Dk. Mwinuka ametaja miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (MW 2115) ambao mkandarasi ameanza rasmi utekelezaji wake tarehe 15 Juni, 2019 kwa kuanza ujenzi wa bwawa pamoja na njia ya kuchepusha maji ambapo mpaka sasa uchorongaji wa handaki la mchepuko wa maji unaendelea na matarajio ya kumaliza mradi huo ni Juni 2022.

Ametaja mradi mwingine wa kimkakati kuwa ni mradi wa kuzalisha umeme  wa Rusumo (MW 80) ambao kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 55 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.

“ Mradi mwingine tunaoutekeleza ni mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi I Extension (MW 185) ambao upo katika hatua za mwisho za utekelezaji kwani umefikia asilimia 84 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020,” amesema Dk. Mwinuka.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alitaja miradi mingine ya kuzalisha umeme wa maji ambayo ipo katika hatua za awali za utekelezaji kuwa ni mradi wa Ruhudji (MW 358), Mradi wa Kakono (MW 87), mradi wa Rumakali (MW 222), mradi wa Malagarasi (MW 45) na mradi wa Kikonge (MW 300).

Aidha, ameongeza kuwa, mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia ambao upo katika hatua za awali za utekelezaji ni mradi wa Mtwara ambao utazalisha  megawati 300.

Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge wametoa maoni mbalimbali yatakayosaidia kuboresha sekta ya umeme nchini ambayo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ameahidi kuwa yatafanyiwa kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles