27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Miradi ya REA ni ya Wananchi- Wakili Kalolo

Na Veronica Simba  – REA

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo amesema wananchi wana haki ya kujulishwa kuhusu miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika maeneo yao kwani kimsingi miradi hiyo ni ya kwao.

Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti hivi karibuni akiwa katika ziara ya kazi mkoani Tanga, Juni 13 hadi 16, 2022 ambapo alifuatana na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.

Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy (wa pili-kushoto), akifafanua jambo kwa Msaidizi wa Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kwemkola, Mheshimiwa Hozza Mandia (kulia), wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo (wa tatu-kushoto) wilayani Lushoto, Juni 15, 2022 kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Akifafanua, Mwenyekiti wa Bodi alisema Serikali imewekeza fedha nyingi katika kutekeleza miradi hiyo ambayo imelenga kuwanufaisha wananchi hususan waishio vijijini.

“Kwa mantiki hiyo, wananchi ndiyo wamiliki wa miradi husika; miradi ni ya kwao maana inatekelezwa na Serikali kwa ajili yao hivyo wanapaswa kuijua vizuri ili watoe ushirikiano katika utekelezwaji wake,” alisisitiza.

Aidha, Wakili Kalolo alisema kuwa endapo Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo watawashirikisha wananchi, itasaidia pia kupata suluhisho la changamoto ya uharibifu na wizi wa miundombinu ya umeme ambayo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy na Ujumbe waliofuatana nao wakikagua miundombinu ya umeme katika kijiji cha Horohoro wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, walipokuwa katika ziara ya kazi, Juni 14, 2022.

Alisema kuwa, wananchi wakishirikishwa watakuwa sehemu ya Mradi hivyo watatoa ushirikiano katika usimamizi wake ikiwemo utunzaji wa miundombinu.

Aliongeza kuwa ushirikishwaji uwalenge pia viongozi wa wananchi ambao ni Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wabunge, Madiwani na viongozi wote ngazi ya vijiji na vitongoji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Saidy akizungumza katika ziara hiyo aliwataka wananchi kuondoa hofu kuhusu suala la wigo wa miradi ya umeme vijijini, ambapo kumekuwa na malalamiko ya umeme kufika eneo dogo katika kijiji na maeneo mengine kutofikiwa.

Alifafanua kuwa, malengo ya Serikali katika hatua ya awali ilikuwa ni kuhakikisha walau kila kijiji kinafikiwa na miundombinu ya umeme mkubwa ili upatikanaji wa huduma za msingi hususan za kijamii ziwepo katika kila kijiji.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo (wa kwanza – kushoto) akifafanua jambo kwa Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga ambaye ni Katibu Tawala, Joseph Sura (wa kwanza – kulia) wakati wa ziara ya kazi ya viongozi wa REA wilayani humo, Juni 14, 2022. Wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.

Mhandisi Saidy aliongeza kuwa, kwa sasa Serikali imejipanga kuongeza wigo ambapo katika kila kijiji zitaongezwa kilomita mbili kutoka kilomita moja ya awali, hivyo kufikia kilomita tatu.

Aidha, alisema kuwa Wakala unaendelea kutekeleza miradi mingine mbalimbali inayolenga kuendelea kuwafikishia umeme wananchi wote ikiwemo miradi ya ujazilizi.

Pia, alibainisha kuwa mpango wa Serikali kwa sasa kupitia REA ni kuanza kupeleka umeme katika ngazi ya vitongoji ambapo ukikamilika, wananchi wote watakuwa wamefikiwa na nishati ya umeme.

Katika ziara hiyo, viongozi mbalimbali walipongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali kupitia REA na wakaahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuwezesha utekelezaji wa miradi inayoendelea.

Viongozi hao ni pamoja na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Adam Malima, Mbunge wa Handeni Vijijini Mheshimiwa John Sallu, Msaidizi wa Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kwemkola, Mheshimiwa Hozza Mandia, na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni ambaye ni Katibu Tawala, Mashaka Mgeta.

Wengine ni Diwani wa Kata ya Mponde Mheshimiwa Richard Mbuguni, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga ambaye ni Katibu Tawala, Joseph Sura, Afisa Mtendaji Kata ya Mwakijembe, Prosper Marumbo, Mwenyekiti wa kijiji cha Msomera wilayani Handeni Martin Parakett na viongozi wengine mbalimbali ngazi ya vijiji na vitongoji.

Ziara hiyo ya siku tatu ililenga kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini ikihusisha kukagua kazi zinazoendelea pamoja na kuzungumza na wakandarasi, viongozi na wananchi.

Nguzo zikishushwa katika Kitongoji cha Olomoti, Kijiji cha Msomera wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga kwa ajili ya matumizi ya kuunganisha umeme katika miradi ya umeme vijijini inayoendelea. Taswira hii ilichukuliwa Juni 15, 2022 wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles