27.5 C
Dar es Salaam
Friday, July 1, 2022

MIRADI YA KINYWE ULANGA, NACHINGWEA YALIPA FIDIA

 

 

Na Mwandishi,

MAHITAJI ya bidhaa au mali yoyote ndio ngao yake kubwa ya kuwekeza katika rasilimali hiyo na si vinginevyo.

Kwa kuzingatia hayo, mabadiliko ya matumizi ya grafaita (Kinywe) na lithium kwa kutengeneza betri za magari ya umeme, imebadilisha kwa kiasi kikubwa mwonekano na mwenendo wa uwekezaji katika madini hayo.

Kumekuwa na wimbi la wawekezaji wenye haja ya kuwekeza katika upatikanaji wa madini hayo kutokana na taarifa kutoka ofisi za madini.

Kamishna wa Madini, Ally Samaje, amethibitisha kuwa kuna ongezeko kubwa la wale wanaoomba leseni za utafutaji wa madini hayo nchini.

Samaje anasema kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya kutengeneza magari  duniani  ambapo yale yanayotumia umeme wa betri badala ya mafuta  ndio magari pendwa, mahitaji ya madini ya kinywe (grafaita) na lithium yameongezeka duniani kote na Tanzania inayo nafasi kubwa kufaidika kutokana na hilo, kwani inayo sehemu nyingi zinazopatikana madini haya pendwa kwa sasa.

Mkakati wa Taifa ni kuwezesha utafutaji na uchimbaji wa madini hayo.

Taarifa za Jarida la Business Insider la Agosti na Oktoba mwaka jana la huko Marekani, zimebaini kampuni moja ya MIT imetengeneza aina mpya ya betri ambayo inaweza kudumu mara mbili ya muda wa betri ya smartphone au ya komputa  mpakato.

Kampuni hiyo ya Solid Energy Systems  ya Marekani iliyotengeneza betri hizo, ilipata fedha za wawekezaji Dola milioni 12 kwa kuzitoa betri mwanzoni mwa mwaka huu kwa vifaa vidogo vidogo  na zile zenye uwezo mkubwa zitatolewa mwakani na haswa kwa magari.

 Kamishna Samaje alisema kwa kuzingatia umuhimu wa madini hayo, Serikali imeyapa kipaumbele na hivyo miradi ya Kinywe kule Mahenge na Lindi itaanza kutekelezwa hivi karibuni.

“Fidia imeanza kutolewa kwa wale wanaozunguka migodi tarajiwa kule Mahenge ambako asilimia 80 ya waathirika wameshalipwa vilivyo.

“Kuhusu  Nachingwea Graphite Mining (Nachu), kampuni ya Uranex kutoka Australia imeshafikia hatua ya utekelezaji mradi kwani wananchi wote pale Nachingwea walioathirika na mradi huo wamekwishalipwa ili kupisha uanzishwaji wa shughuli ya uchimbaji madini hayo,” alisema Samaje.

Kwa hiyo Nachingwea wako mbele ya Mahenge katika utekelezaji wa mradi.

Akizungumza kwa kujiamini Samaje alidai kuwa ndani ya mwaka mmoja Tanzania itakuwa nchi mojawapo rasmi ya uchimbaji wa kinywe na hilo ni jambo la kujivunia kwani litakuza pato la Taifa na kutoa ajira kwa wananchi wake.

Suala la betri hizo limekuwa kubwa kwani kufuatia utafiti wa Bloomberg New Energy Finance, inasemekana kuwa bei ya betrei hizo itapungua sana na kufikia miaka ya 2020, magari ya umeme yatatawala kwa kuwa ya kiuchumi zaidi kuliko yale yanayotumia mafuta ya petroli au dizeli katika nchi nyingi duniani.

Wasomi na watafiti wengi wamechangamkia taaluma hiyo mpya ya magari na betri zake  na hivyo Prof. Rubhera Mato wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaaam idara ya Uinjinia wa Mazingira, anasema madini kama hayo yamepata umaarufu mkubwa katika kusanifu teknolojia mpya  ya kufuta matokeo hasi ya mabadiliko ya Hali ya Nchi (climate change ) yatokanayo na kuharibika kwa mazingira  kunakoletwa  na kuzalisha gesi haribifu kwa Mazingira.

Tanzania yaongoza kwa Hazina

Taarifa ya CBC News ya Marekani ya Februari 21, inasema hazina ya kinywe ulimwenguni ni  tani milioni 230 ambayo yako nchi  za China, Uturuki, Brazil, Mexico na India wakati Uturuki ndiyo yenye hazina kubwa ya tani milioni  90. Tanzania hazina yake ni tani milioni 500  na hivyo kuongoza ingawa haijulikani na wengi kutokana  na taarifa za makisio ya watafutaji madini hayo nchini.

Taarifa hiyo inasema kuanzia mwaka 2015, uzalishaji wa madini ya kinywe ulikuwa tani milioni 1.21 duniani wakati China ikiwa ndio mzalishaji mkubwa kwa kuzalisha tani elfu 800.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,419FollowersFollow
544,000SubscribersSubscribe

Latest Articles