27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Miradi ya kimkakati, viwanda vilivyoteka sekta ya uchumi 2019

Na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

KWA siku kadhaa sasa tumekuwa tukiyaangazia matukio makubwa yaliyotokea nchini kwa mwaka huu wa 2019. 

Kama ilivyo katika sekta zingine yapo pia matukio kadhaa ya kukumbukwa mwaka huu katika sekta ya uchumi na makala haya yanaangazia matukio hayo.

UZINDUZI WA VIWANDA

Mara kadhaa Rais magufuli amekuwa akihudhuria sherehe za uzinduzi wa viwanda mbalimbali nchini hatua ambayo ni ishara ya harakati za kujaribu kuimarisha zaidi uchumi kuelekea Tanzania ya Viwanda.

Juni 25, Rais Magufuli alizindua ghala na mitambo ya gesi ya kupikia inayomilikiwa na Kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited iliyopo Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es Salaam.

Kampuni hiyo ambayo awali ilijulikana kama Mihan inamilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 na iliandikishwa mwaka 2005 na kuanza kufanya biashara mwaka 2008.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Hamisi Ramadhani, alisema uwekezaji huo uliokwenda sambamba na ujenzi wa maghala na mitambo ya gesi katika mikoa 20 hapa nchini umegharimu Sh bilioni 150.

Hatua hiyo inaifanya kampuni hiyo kuwa kubwa zaidi ya uwekezaji kwa idadi ya mitambo na kwa ukubwa wa ghala lenye mitambo ya kisasa kuliko yote Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Alisema gesi hiyo ya LPG ni rahisi kusambazwa kwenye mitungi na kwamba hadi sasa wameshasambaza mitungi milioni moja ya ujazo kati ya kilo tatu hadi 38.

Uwekezaji huo umetoa ajira kwa vijana 260 wakiwemo wahitimu 130 wa elimu ya juu na ajira zisizo za moja kwa moja 3,500.

Agosti Mosi, Rais Magufuli alizindua kiwanda cha kusaga nafaka kilicho chini ya Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) kilichopo Kurasini, Dar es Salaam.

“Kila ninapoalikwa kwenye uzinduzi wa kiwanda moyo wangu huwa unafurahi, sikutegemea kuona mambo makubwa ambayo nimeyaona humu ndani,” alisema Rais Magufuli.

Alisema viwanda ndiyo mhimili mkuu wa maendeleo, hakuna taifa lolote duniani ambalo linaweza kufanya mabadiliko ya haraka ya kiuchumi bila kufanya marekebisho kwenye sekta ya viwanda.

“Nyerere alijenga viwanda nchi nzima kwa ajili ya mazao, bahati mbaya viwanda hivi tuliviua kutokana na usimamizi mbovu. Ukweli ni kwamba tukiwa na viwanda vya kimkakati kwa ajili ya mazao tunaweza kusindika mazao, hii itaongeza thamani ya mazao na kuwainua wakulima wetu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hadi sasa viwanda vipya nchini vimefikia zaidi ya 4,000.

Aprili 8, Rais Magufuli pia alizindua kiwanda cha kuchakata mahindi cha Mlale baada ya kilio cha muda mrefu cha wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kubaki na mahindi yao kwa kukosa soko.

Hivi sasa wananchi wa mkoa huo wanaweza kuuza unga na si mahindi tena waliyokuwa wakidhulumiwa na walanguzi.

Rais Magufuli alisema kiwanda hicho cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale kitakuwa suluhisho la ukosefu wa soko la mazao kwa wakulima mkoani humo.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, alisema kiwanda hicho kimejengwa kwa umahiri mkubwa na JKT.

Aprili 29, Rais Magufuli pia alizindua kiwanda cha parachichi cha Rungwe mkoani Mbeya, na kusema Serikali itayafanyia kazi matatizo yaliyopo yakiwemo ya uhaba wa maji, barabara na mengine.

Aliwapongeza bodi ya wakurugenzi na mwekezaji wa kiwanda hicho kwa kutoa ajira kwa kinamama na vijana wengi, wakulima na kuwaahidi kuwa Serikali inafanya jitihada ili uwanja wa ndege wa Songwe ukamilike kwa ajili ya kusafirisha mazao hayo na mengine kwenda nje ya nchi.

MIRADI MIKUBWA

Julai 26, Rais Magufuli alizindua ujenzi wa bwawa la kufua umeme katika eneo la mto Rufiji mkoani Pwani.

Mradi huo utakaozalisha megawati 2,115 unatekelezwa kwa gharama ya Sh trilioni 6.5 na utakapokamilika utashusha bei ya umeme na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini.

Rais Magufuli alisema bwawa litakalojengwa litakuwa la kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki na la nne kwa ukubwa Barani Afrika.

Alipendekeza liitwe Bwawa la Nyerere ikiwa ni kutambua na kuenzi maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyetaka kujenga bwawa hilo wakati wa uongozi wake.

Alisema mradi huo hautaathiri mazingira na badala yake utaimarisha ukuaji wa uchumi kupitia ujenzi wa viwanda.

Pia Oktoba 26, Rais Magufuli alieeleza furaha yake kuhusu ununuzi wa ndege uliofanyika tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania Novemba 5, 2015.

Alieleza furaha yake hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) muda mfupi baada ya kuongoza mamia ya Watanzania kupokea ndege ya mpya ya pili, Boeing 787-800 Dreamliner iliyowasili ikitokea nchini Marekani.

Magufuli alisema ndege hiyo ni kati ya ndege 11 zinazotarajiwa kununuliwa na Serikali ifikapo mwaka 2022.

“Kwangu ninajisikia vizuri kuwa kiongozi wa Tanzania, lakini najisikia vizuri kuwa Mwenyekiti wa CCM. Haya yalizungumzwa kwenye ilani ya uchaguzi na sisi ni watekelezaji.

“Mungu anatupenda Tanzania, ndege kama hii inashuka hapa lazima tujiulize kwa nini haikushuka zamani? 

“Huo ndiyo ukweli bila kuficha. Kwa nini ndege kama hii isubiri Magufuli ndio ishuke,” alisema Magufuli.

Rais Magufuli alisema mkakati wa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ni wa uhakika kulingana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.

“Waswahili husema ukitaka kwenda safari ndefu lazima uende na hatua fupi. Tulipoanza kulifufua ATCL na kuanza na ndege kubwa baadhi ya watu walidhani tuna ‘beep’ na wengine walipiga kejeli za chini.

 “Nataka niwahakikishie kuwa shirika letu la ATCL linafufuliwa kama ilivyoelezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya 2015.”

Awali akieleza mkakati wa miaka mitano wa ATCL, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho, alisema shirika hilo linatarajia kuwa na ndege mpya tisa zikiwemo nne za  Bombardier Q400, tatu za masafa ya kati za Airbus A220-300 na mbili kubwa za masafa marefu ambazo ni Boeing 787 Dreamliner.

Julai 9, 2019 wakati akipokea ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kuliimarisha Shirika la ATCL kwa gharama ya Dola 224.6 milioni (Sh bilioni 512) kwa mujibu wa taarifa kwenye tovuti ya kampuni ya Boeing, Rais Magufuli aliwapongeza Watanzania kwa kuchapa kazi na kulipa kodi.

Alisema hilo liliiwezesha Serikali kupata fedha za kutekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ununuzi wa ndege kwa ajili ya kuimarisha ATCL ambayo ilikuwa na hali mbaya.

“Shirika letu la ndege lilikuwa na hali mbaya sana, lilikuwa na ndege moja tu tena ilikuwa inafanyiwa matengenezo mara kwa mara, soko la ATCL lilishuka hadi kufikia asilimia 2.5, lakini sasa tumenunua ndege 7, hii ni ndege ya 4 na nyingine mbili zitakuja kabla ya mwaka huu kuisha. Nyingine kubwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner itakuja mwaka 2020.

“Tangu tumeongeza ndege tatu mpya aina ya Bombardier Q400 biashara ya ATCL imeongezeka, Shirika letu lilikuwa linasafirisha abiria 4,000 tu kwa mwezi lakini sasa linasafirisha abiria 21,000 na ndege zinatua katika vituo 12,” alisema.

Rais Magufuli anaamini ununuzi wa ndege hizo utachangia kuimarisha uchumi wa Tanzania, kwa pamoja na miradi mingine mikubwa inayotekelezwa na Serikali.

Alisema; “Tumeleta ndege hizi ili ziimarishe na kuongeza mapato yetu ya utalii nchini, asilimia 70 ya watalii wanatumia ndege. Tunaboresha usafiri wa reli, majini na barabara. Waliodhani kuwa maboresho ya Bandari hayana tija sasa wameaibika.

Rais Magufuli alibainisha kuwa Serikali iliamua kuchukua hatua ya kulinusuru Shirika la Ndege la Taifa ili kujenga heshima na kulinda hadhi ya Taifa, kuimarisha na kuboresha huduma za usafiri wa anga na kukuza utalii.

“Tumefufua ATCL kurejesha heshima ya nchi, ilikuwa aibu kutokuwa na ndege kwa nchi kubwa kama Tanzania,” alisema.

Rais Magufuli pia aliwasuta waliokuwa wanadai kwamba ndege hiyo ni ya gharama ya juu na haitaifaa Tanzania. Alisema ndege hizo zimenunuliwa kwa kutumia kodi na kwamba si kwa kupitia mkopo.

“Ndege zote hizi tumenunua kwa fedha zetu wenyewe, hatujakopa kwa mtu. Ndege hizi ni matokeo ya Watanzania kulipa kodi na kuchapa kazi. Nawapongeza wote walioshiriki kikamilifu.

“Madai kuwa Watanzania wengi hawafaidiki na ndege hayana msingi. Wapo wengi wanaohitaji ndege bei ilikuwa juu.

“Ndege hii imewafurahisha wengi na kama yupo mtu hajafurahia tukio hili basi huyo atapata taabu sana,” alisema Rais Magufuli.

Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 262 ni ya kisasa zaidi kuwahi kumilikiwa na Serikali ya Tanzania.

Ina uwezo wa kusafiri kilomita 13,620 kwa wakati mmoja na urefu wake ni mita 57. Upana wa mabawa yake ni mita 60. Urefu wake kutoka chini hadi juu ni mita 17.

Rais Magufuli aligusia hilo aliposema; “Ndege hii ni ya kisasa na kote walikopita walikuwa wana uwezo wa kunipigia simu na kuongea nao angani.

Ethiopia ilikuwa nchi ya kwanza duniani kando na Japan kuanza kutumia Boeing 787-8 Agosti 2012.

Agosti Mosi, Rais Magufuli alizindua jengo la tatu la abiria katika uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal III), lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita.

Kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo sasa zaidi ya abiria milioni nane watahudumiwa katika uwanja huo.

Jengo la kwanza la abiria (Terminal 1) lina uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka wakati jengo la pili (Terminal 2) likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka.

Wazo la kujenga uwanja huo lilikuja baada ya jengo la pili kulemewa na wingi wa abiria mpaka kufikia milioni 2.6 kwa mwaka. 

SERIKALI, BARRICK WAUNDA KAMPUNI YA TWIGA

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, akikagua ghala la kuhifadhia nafaka la Kampuni ya Ria Mills Ltd lililopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Baada ya mgogoro uliodumu tangu mwaka 2017, Kampuni ya Barrick na Serikali zimeunda Kampuni ya Twiga itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa chini ya Kampuni ya Acacia.

Kwenye kampuni hiyo mpya, Barrick itamiliki asilimia 84 ya hisa zote huku Serikali ikiwa na asilimia 16. Utaratibu huo ni utekelezaji wa sheria mpya ya madini iliyopitishwa mwaka 2017.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema ‘sasa amezaliwa mtoto mpya baada ya Barrick kukubali kumuua mtoto wake, Acacia.’

Mgogoro baina ya Serikali na Kampuni ya Acacia iliyokuwa inasimamia migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu ulianza mwaka 2017 na Rais Magufuli aliunda tume ya kuchunguza mwenendo wa biashara ya madini.

Tume hiyo ilibaini ukiukwaji wa sheria, utaratibu na kanuni zilizopo hivyo kuikosesha Serikali mapato inayostahili. Kutokana na hilo, Serikali iliipiga faini ya Dola bilioni 190 jambo lililosababisha kuanza kwa mazungumzo baina ya pande hizo mbili.

Kwenye mazungumzo hayo, Acacia ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick iliwekwa pembeni na majadiliano yakafanywa na Barrick. Mwisho wa siku, Acacia imefutwa sokoni na badala yake, Twiga itachukua nafasi yake.

 “Twiga Minerals Company Limited itakuwa na makao makuu yake jijini Mwanza, kampuni hii imeundwa baada ya kufutwa kwa Acacia iliyokuwa na makao makuu yake jijini London,” alisema Profesa Kabudi.

UNUNUZI WA KOROSHO

Septemba 20, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alitangaza mfumo mpya wa ununuzi wa korosho kwa mwaka 2019/20 utakaokuwa katika minada ya wazi katika jukwaa la Soko la Bidhaa (TMX).

Waziri Hasunga alisema mfumo huo ulioanza rasmi Septemba 30 wakulima wote watasajiliwa na Bodi ya Korosho kupitia mfumo wa wizara ya kilimo wa kusimamia biashara za Kilimo (ATMIS).

 “Tutaendesha minada ya wazi, kila Mtanzania anaweza kuona na kushiriki na kote duniani watashiriki. Wanunuzi waliosajiliwa na kukidhi vigezo watatakiwa kulipa kinga ya dhamana kutegemea kiasi cha korosho mnunuzi anachotaka,” alisema Hasunga.

Akifafanua zaidi alisema mfumo huo unatofautiana na minada ya awali ambapo wanunuzi walikuwa wakiweka zabuni zao kwenye sanduku kisha linafunguliwa.

“Mtu yeyote anayetaka kununua korosho ataingia kwenye tovuti ya wizara na kuweka kiasi anachohitaji. Mpaka sasa kuna watu wengi na kampuni nyingi zimejisajili,” alisema.

Alisema wanunuzi wa ndani na nje wataruhusiwa kununua korosho kwa mafungu kati ya tani 50 mpaka 500 kulingana na mahitaji.

Alisema katika msimu huu, Tanzania inatarajia kuvuna tani 300,000 za korosho kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji.

Kuhusu msimu uliopita alisema kati ya tani 224,000 zilizokusanywa baada ya Serikali kuamua kununua korosho zote kwa wakulima katika msimu wa 2018, Serikali ilishalipa Sh bilioni 723 huku zaidi Sh50 milioni zikiendelea kulipwa kwa wakulima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles