Na Walter Mguluchuma-Katavi
MIMBA za utotoni bado ni tishio kubwa katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi ambako wasichana 624 walio na umri wa chini ya miaka 18, wamejifungua  katika vituo vya afya vilivyopo katika manispaa hiyo.
Hayo yalisemwa hapo jana na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia  zilizofanyika viwanja vya Sabasaba Kabungu wilayani Tanganyika.
Meja Jenerali Muhuga alisema taarifa  kutoka katika vituo vya afya vya Manispaa ya Mpanda ya kipindi cha mwaka jana inaonyesha wasichana 624 wenye umri wa chini ya miaka 18 walijifungua katika vituo  vya afya vilivyopo katika manispaa hiyo na kwamba kiwango hicho ni kikubwa na ni tishio.
Alisema utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya maralia  wa mwaka  2015/16 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto umeonyesha Mkoa wa Katavi unaongoza kitaifa kwa tatizo hilo.
Alisema utafiti huo umeonyesha kitaifa kuwa  asilimia 27 ya wasichana wa  miaka  15  hadi 19 wameishaanza uzazi, huku asilimia 21 wakiwa wamezaa mtoto hai angalau mmoja, huku Mkoa wa  Katavi asilimia 45 ya  wasichana  wenye umri wa  miaka 15  hadi 19 tayari ni wazazi.
Kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, alisema kesi 1,178 ziliripotiwa katika vituo vya kutolea huduma za  afya mkoani humo na maofisa ustawi wa jamii mwaka  2016.
Alisema kati ya kesi hizo, kesi 401 zilihusu ukatili wa kimwili , 66 zilihusu ukatili wa kingono, 264 zilihusu ukatili wa kisaikolojia na 447 zilihusu kutelekezwa watoto na familia zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Liliani Matinga,  aliwataka wanawake ambao wana tabia ya kupiga waume zao waache tabia hiyo mara moja kwa kuwa inawaaibisha wanawake wote nchini.
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda, alisema licha ya jitihada zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na makundi mbalimbali ya kijamii, takwimu bado zinaonyesha ongezeko la ukatili wa kijinsia.
Alisema ongezeko hilo linachangiwa na changamoto zifuatazo ambazo ni imani za kishirikina, mila na desturi za baadhi ya makabila, umasikini, elimu na ukosefu wa nyumba salama, ambapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwalaza wageni wao na watoto wao na kusababisha wageni hao kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.