22.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Milioni 134 zilizotaka kutafunwa zaokolewa na Takukuru Pwani

Na Gustafu Haule,Pwani

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Pwani imeokoa kiasi cha Sh milioni 134.8 zilizokuwa zimechepushwa na kufanyiwa ubadhirifu kinyume na sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani, Suzana Raymond, alitoa taarifa hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ikiwa ni ya kipindi cha robo mwaka iliyoanzia Januari hadi Machi 2021.

Raymond amesema uokoaji wa fedha hizo umetokana na kuyafanyiakazi malalamiko 136 yaliyopokelewa katika ofisi yake katika kipindi cha miezi mitatu.

Amesema kuwa,kati ya malalamiko hayo 79 uchunguzi wake bado unaendelea katika hatua mbalimbali na malalamiko 57 yalionekana kuangukia katika sheria nyinginezo na kwamba walalamikaji walishauriwa kuelekeza sehemu husika za kimamlaka.

Aidha, alisema jumla ya kesi 17 ziliendelea kuendeshwa katika mahakama mbalimbali za mkoa wa Pwani ambapo kati ya hizo kesi mpya tatu zilifunguliwa.

Akitaja baadhi ya maeneo zilikookolewa fedha hizo Mkuu huyo wa Takukuru alisema Wilaya ya Bagamoyo waliokoa Sh milioni 57.7 fedha ambazo ni za michango ya mafao ya NSSF na PSSSF kwa watumishi wa Shule ya Sekondari ya Eagle.

“Kiasi hicho cha fedha kilichepushwa na kilikuwa hakijawasilishwa na mwajiri ambaye ni mmiliki wa Shule hiyo ya Sekondari kwenye mifuko husika lakini ofisi ilifuatilia na hatimaye mwajiri alilipa kiasi hicho cha fedha na wahusika kupata malipo yao ya mafao,”amesema Raymond.

Ameongeza kuwa mbali na fedha hizo lakini pia kwa Wilaya hiyo waliweza kuokoa  fedha nyingine kiasi cha Sh milioni 14 zilizotolewa kwa Baraza Kuu la Waislam Tanzania ( Bakwata )na mfadhili Raia wa Oman kwa ajili ya faida ya wananchi wa Kata ya Zinga.

Amesema fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya kutumika katika kuchimba visima vinne vya maji lakini tangu fedha zitolewe visima havikuchimbwa na kwamba Takukuru ilipopata taarifa ilifuatilia na kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na kufanyakazi iliyokusudiwa ya kuchimba visima kwa ajili ya wananchi hao.

Raymond amesema kuwa pamoja na kuokoa fedha hizo lakini bado Takukuru Mkoa wa Pwani wanaendelea kuweka mikakati ya kukomesha vitendo mbalimbali vya rushwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mwananchi.

Amefafanua zaidi kuwa moja ya mikakati hiyo ni kuendelea kuelimisha umma kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika mapambano ya rushwa, kuongeza kasi ya uchunguzi, pamoja na kuendelea kufanya ufuatiliaji wa mifumo kwa lengo la kuziba mianya ya rushwa.

Aidha, Raymond ameendelea kuwasihi wananchi wa Mkoa wa Pwani na Watanzania kwa ujumla kufanyakazi kwa uadilifu kwa kuepuka vitendo vya rushwa kwakuwa dhamira ya Serikali chini ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha rushwa inatokomea.

Hata hivyo amesema kwasasa Takukuru imeanzisha huduma ya Takukuru inayotembea(PCCB MOBILE) na kuwataka waitumie bila woga kwakuwa ndio sehemu sahihi ya kuhakikisha wananchi wanawasilisha malalamiko yanayohusu vitendo vya rushwa na hivyo kuweza kushughulikiwa kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,205FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles