23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Milima usiyoifahamu inayoongoza kwa urefu nchini

MWANDISHI WETU

WATU wengi wanaujua zaidi Mlima Kilimanjaro kutokana na upekee wake katika Bara la Afrika. Ni wachache mno wanaoweza kutaja au kuielezea kwa ukamilifu milima mengine mirefu nchini ambayo nayo ina vivutio lukuki vya utalii.

Ripoti ya Utafiti ya Wageni wa Kimataifa ya mwaka 2016 (The 2016 International Visitor Exit Survey Report) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Oktoba mwaka jana, inaeleza kuwa upandaji wa milima ni kuvutio cha tatu kwa wageni wa nje wanaoingia nchini kwa mara ya kwanza baada ya utalii wa wanyamapori na ufukweni.

Tanzania kuna milima 10 mirefu, ambayo inayo fursa za kitalii.

Uchambuzi zaidi wa takwimu muhimu za mwaka 2016 za NBS (Tanzania in figures 2016) unabainisha kuwa milima tisa kati ya 10 mirefu zaidi nchini ipo katika mikoa miwili ambayo ni Kilimanjaro na Arusha. Ni mlima mmoja tu wa Mtorwi ndiyo unapatikana mkoani Iringa. 

Ifuatayo ni orodha ya milima 10 mirefu zaidi Tanzania 

Mlima Kilimanjaro

Mlima Kilimanjaro si tu ni mlima mrefu zaidi nchini, bali katika bara zima la Afrika. Mlima huo wenye urefu wa mita 5,895 (futi 19,340) pia ni hifadhi ya Taifa. Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 755 na uko umbali wa kilometa 45 kutoka Moshi mjini. Kilele cha Kibo ndio kivutio kikubwa kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na kufunikwa na theluji.

Mlima huo unaopatikana katika Mkoa wa Kilimanjaro, ni moja kati ya milima ambayo kilele chake hufikiwa kwa urahisi na hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa wapanda milima kutoka kila pande za dunia.

Mlima Meru

Mlima wa pili kwa ukubwa Tanzania ni Mlima Meru, wenye kilomita za mraba 4,566 (futi 15064) kutoka usawa wa bahari ikiwa ni tofauti ya mita 1329 kutoka Mlima Kilimanjaro. Katika anga za kimataifa, Mlima Meru unashika nafasi ya tisa kwa urefu barani Afrika.

Mlima Meru unapatikana ndani ya Hifadhi ya Arusha ambayo ilianzishwa mwaka 1960. Baadhi ya wanyamapori waliopo katika hifadhi waliletwa kutoka katika maeneo mengine na hupenda kuzungukazunguka katika Mto Momella na Kreta ya Ngurudoto (Ngurudoto crater).

Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 137 na ipo umbali wa kilometa 35 kutoka mji wa kitalii wa Arusha na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Inaelezwa kuwa kupanda Mlima Meru kunachukua siku tatu hadi nne na wakati mzuri wa kupanda ni kuanzia Juni hadi Februari, ambapo mvua zinaweza kunyesha Novemba. Na wakati mzuri wa kuona Mlima Kilimanjaro kutokea Meru ni kati ya Desemba na Februari.

Mlima Klute

Mlima Klute unashika nafasi ya tatu kwa ukubwa hapa Tanzania. Mlima huo wenye urefu wa mita 3,952  unapatikana katika Mkoa wa Kilimanajaro ikiwa ni tofauti ya mita zipatazo 1,943 na Mlima Kilimanjaro.

Mlima Lool Malasin

Mlima Lool Malasin ni wa nne kwa urefu Tanzania kati ya milima mirefu 25 iliyopo Tanzania. Mlima huu una urefu wa mita 3,648 na unapatikana katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Mlima Shira

Mlima Shira wenye urefu wa mita 3,626 ni miongoni mwa vilele vitano Tanzania. Mlima huo uliopo mkoani Kilimanjaro unatofautiana mita 22 tu na Mlima Lool Malasin.

Mlima Oldeani

Mlima Oldeani unaopatikana katika mikoa miwili ya Manyara na Arusha, una urefu wa mita 3,188 na kuufanya kuwa mlima wa sita kwa urefu nchini. Tofauti na milima maarufu ya Kilimanjaro na Meru, hakuna taarifa nyingi za kina kuhusu Mlima Oldeani.

Mlima Hanang

Mlima Hanang unashika nafasi ya saba kati ya milima kumi mirefu zaidi Tanzania, ukiwa na mita 3103. Mlima huu unapatikana katika Mkoa wa Manyara ukitofautiana mita 1,463 na Mlima Meru unaopatikana mkoani Arusha. 

Jaeger, mita

Jaeger ni mlima wa nane katika orodha milima mirefu zaidi nchini. Unapatikana katika Mkoa wa Arusha. Jaeger ni mlima wa nne kwa urefu mkoani humo baada ya milima Meru, Oldeani na Hanang. Tofauti na Mlima Meru, Jaeger hauna taarifa za kutosha za kuwasaidia watalii kujua kwa undani namna ya kutalii.

Monduli

Mlima Monduli una mita 3,000 upo katika Mkoa wa Arusha, ukiwa ni mlima wa tisa kwa urefu nchini. Huu ni mlima wa tano kwa urefu Arusha. Hii ina maana iwapo unataka kuvunja historia, unaweza kuipanda milima yote mkoani humo ukawa umeshapanda milima mitano kati ya 10 mirefu zaidi nchini. 

Mtorwi

Watu wengi hudhani mlima Rungwe ni moja ya milima yenye vilele virefu zaidi, hii ni kutokana na umaarufu wake lakini takwimu za NBS zinaonyesha tofauti.

kilele cha Mlima Mtorwi uliopo mkoani Njombe

Rungwe unazidiwa urefu wa mita moja tu na Mlima Mtorwi kutoka mkoani Iringa ambao ndiyo mlima wa 10 kwa urefu Tanzania. Mtorwi wenye mita  2,961 ndiyo kilele cha Nyanda za Juu Kusini. Mlima Mtorwi ni sehemu ya Platu ya Kitulo ambayo ni maarufu kutokana na maua yake. 

Hata hivyo, mtandao wa lonelyplanet unasema miundombinu ya upandaji mlima hususan wakati wa masika siyo mzuri hivyo ni bora wapandaji wakafanya utalii wakati wa kiangazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles