25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

‘Mila ya kuosha nyota mtoto wa kike chanzo mimba shuleni Kishapu’

Na DAMIAN MASYENENE – SHINYANGA

MILA ya samba, marufu kama kuosha nyota watoto wa kike kwa kuwapaka dawa ili wapate wanaume wilayani Kishapu, imeelezwa kuwa chanzo cha watoto wengi kupata mimba wakiwa shuleni.

Inaelezwa kwa mwaka jana pekee mimba 56 ziliripotiwa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Kishapu, huku kesi 30 zikifikishwa mahakamani na 25 zikiwa zinaendelea kufanyiwa upelelezi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba, alisema suala la mimba za utotoni kwa wanafunzi limekuwa changamoto.

Alisema jeshi hilo limefanya jitihada mbalimbali kwa kutembelea maeneo yote yanayotajwa na kukutana na wadau, huku akikemea tabia za kuendelea kudumisha mila zinazochochea vitendo hivyo.

“Sababu kubwa ya tatizo hili imekuwa ni mila na desturi potofu, kule Kishapu wazazi ndio kichocheo, furaha yao ni kuona binti anatongozwa, kwahiyo wakiona amefikia umri fulani na hajatongozwa ama kupata mwanaume, wanampeleka kwa waganga wa kienyeji aweze kuoshwa nyota.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba

“Kwahiyo nashauri wadau wote tushirikiane kulipiga vita na kuwaokoa mabinti hawa waweze kutimiza ndoto zao hasa za kielimu,” alisema Kamanda Magiligimba.

Mkuu wa Kikosi cha Upelelezi Mkoa wa Shinyanga, Davis Msangi, alisema Wilaya ya Kishapu imekuwa sugu katika suala la mimba kwa wanafunzi.

Alisema sababu kubwa ni mnada katika eneo la Muunze siku ya Alhamisi ambao hutumika kuwarubuni watoto wa kike na kukatishwa ndoto zao.

Desemba 8, mwaka jana wakati wa kikao cha kupanga wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020 mkoani hapa, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba alisema watoto wengi wa kike wamekuwa wakishindwa kuendelea na masomo kutokana na wazazi wao kuendekeza tabia ya kuwaosha nyota ili wawavutie wanaume, hivyo kujikuta wakiolewa na kupewa mimba.

“Jamii za huku kuna utamaduni wa watoto wa kike kuoshwa nyota ili wawavutie wanaume, yaani mtoto akitoka kutembea jioni mama anamuuliza kama amesemeshwa na mwanaume na wengi wanaoshwa hizo nyota kuanzia darasa la nne, hapa cha muhimu kila mtu asimamie sheria na kuwajibika katika eneo lake,” alisema Talaba.

Alikemea tabia iliyojengwa siku za karibuni na wazazi na watendaji wa taasisi za Serikali kugeuza tatizo la mimba kwa wanafunzi kama mradi wa kujipatia fedha.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles