Na OMARY MLEKWA-
SIHA
WAKAZI wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kushirikiana na Serikali ili kukamilisha ujenzi wa wodi ya akinamama, watoto na upasuaji hali itakayosaidia kuboresha huduma wilayani hapo.
Akizungumza na kamati ya maandalizi  ya harambe ya ujenzi wa wodi hiyo, Onesmo Buswelu, alisema jamii ikiondoa dhana ya kuwa huduma za kijamii ni za Serikali itasaidia kukamilika kwa wodi hiyo.
Alisema lazima jamii kuonyesha ushirikiano wa kutosha katika kuchangia huduma za maendeleo ili kuweza kukamilisha kwa wakati na kuwaondolea adha ya upatikanaji wa huduma husika.
Buswelu alisema moja ya vitu ambavyo amevipa kipaumbele ni upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi ikiwa ni pamoja na huduma ya afya ya uzazi ya mama na mtoto ili waweze kuhudumiwa kwa uhakika.
“Nawaombeni wananchi tuungane na Serikali kwa kuchangia nguvu zetu kuhakikisha wodi ya akinamama, watoto na upasuaji inakamilika.
Alisema heshima ya mwanamke inapotea kutokana na kutokuwa na wodi hiyo ambayo ingewafanya akinamama kujifungulia sehemu ambayo ina wasitiri tofauti na ilivyo sasa hakuna stara kwa wanawake.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Andrew Method, alisema ujenzi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh milioni 800 hadi kukamilika na kuwaondolea adha wananchi wanaohitaji huduma za upasuaji kusafiri hadi Hospitali ya Rufaa ya KCMC au Mawenzi ndiyo upate huduma hiyo.
“Tumekusanya Sh milioni 12 leo kwenye kamati ya maandalizi ya harambee hiyo itakayofanyika Aprili mwaka huu kwa lengo la kujenga wodi ya watoto na wodi ya kinamama na upasuaji zinahitajika Sh milioni 800 kukamilisha ujenzi huo.
Mkazi wa Kijiji cha Sanya hoyee, Safina Hamisi, alisema wodi hiyo ikikamilika itawaondolea usumbufu waliokuwa wanaupata na pia itawaondolea ngarama za kuwapeleka kwenye hospitali za mkoa.
Mbunge wa jimbo hilo, Dk. Godwin Mollel, alisema katika kipindi hiki atahakikisha kuwa wanaimarisha mahusiano katika kutekeleza miradi ya maendeleo hali itakayosogeza huduma kwa jamii.