NA ESTHER MNYIKA, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amemsimamisha kazi Meneja wa Fedha wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Stephen Kasubi kwa tuhuma za kuisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 700.
Pamoja na hatua hiyo meneja huyo pamoja na wakala mkuu wa tiketi wa Kampuni ya Salama World Travel wa nchini Comoro, wanatakiwa kurejesha serikalini fedha hizo zilizopotea.
Hatua hiyo imekuja siku saba baada ya Rais Dk. Magufuli, kuahidi kununua ndege mpya sita za ATCL kwa Sh bilioni 750 katika kilele cha Siku ya Sheria nchini na kuwaondoa wafanyakazi 250 wa shirika hilo waliopo sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Profesa Mbarawa, alisema taarifa za ndani zimebaini kuwa Wakala wa Kampuni ya Salama World Travel iliyopo nchini Comoro kwa kushirikiana na meneja huyo walifanya wizi wa tiketi kwa njia ya mtandao nchini humo.
Alisema wakala huyo anayeishi Comoro ambaye ni mdau wa Serikali, alikuwa akiuza tiketi nyingi lakini fedha hazionekani wala kuingizwa kwenye akaunti ya ATCL.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni ya ATCL wakala huyo alipewa fursa ya kukatisha tiketi za ndege za Sh milioni 15 kwa kila safari ambazo huingizwa kwenye akaunti moja kwa moja kabla ya kukatisha tiketi zingine.
“Hata hivyo kampuni hiyo haikuwa ikitekeleza sheria hiyo badala yake waliendelea kukatisha tiketi kwa zaidi ya safari moja bila kutuma fedha kama inavyotakiwa.
“Kwa mfano Mnamo Oktoba 29 mwaka 2015 alipewa fursa ya kukatisha tiketi zenye thamani ya Sh milioni 181, Novemba 11 mwaka jana (mwaka 2015), tiketi zenye thamani ya Sh milioni 60, Desemba 13 mwaka jana tiketi zenye thamani ya Sh milioni 121 na Januari 10, mwaka huu tiketi zenye thamani ya Sh milioni 121 fedha zote hizo hazikuingizwa kwenye akaunti.
“Hasara hiyo imesababishwa na wakala mmoja wa Kampuni ya Salama World Travel ya kukatisha tiketi za ndege za ATCL ya nchini Comoro kwa kushirikiana na Meneja wa Fedha wa ATCL aliyepo nchini,” alisema Profesa Mbarawa.
Waziri huyo wa Uchukuzi, alisema baada ya kufuatilia kwenye mitandao walingundua Meneja Kasubi, alitoa fursa hiyo ya tiketi zenye thamani ya Sh milioni 700 na alipoulizwa zilipo fedha hizo alijibu kuwa namba ya siri ya mtandao huo amesahau.
Kutokana na tukio hilo, Profesa Mbarawa, alisema kikosi maalumu cha mtandao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini, kinaendelea na uchunguzi ambapo baada ya wiki moja watatoa ripoti na kwamba watahakikisha waliochukua fedha hizo wanazirejesha serikalini kwa mujibu wa sheria.
Licha ya hatua hiyo Profesa Mbarawa, alisema hatua inayofuta kutokana na wizi wa fedha hizo amemwagiza Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya uchunguzi kwa mawakala wote wa ATCL nchini kote
Februari 4, mwaka huu Rais Magufuli wakati akihutubia katika kilele cha siku ya sheria nchini, alisema kuna kesi 442 za kukwepa kodi ambazo zingeamuliwa Serikali ingepata Sh trilioni moja, ambayo ingeweza kununua ndege zaidi ya sita.
Kutokana na hali hiyo alimwomba Jaji Mkuu, Othman Chande kuzimaliza kesi hizo na kama zikimazilika fedha hizo Sh trilioni moja, ataipa Idara ya Mahakama Sh bilioni 259 na Sh bilioni 750 zilizobakia zitanunuliwa ndege sita na wafanyafakazi 250 wa ATCL waliopo sasa wataondolewa.