25.7 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Mikoa kumi yagundua wagonjwa wapya wa Ukoma

VERONICA ROMWALD, MOROGORO

LICHA ya Tanzania mwaka 2006 kufikia viwango vya utokomezaji wa Ukoma kitaifa kwa kiwango cha chini ya mgonjwa 1 kati ya watu 10,000, inaelezwa ugonjwa huo bado umeendelea kuwa tatizo la kiafya miongoni mwa jamii nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo jana mjini Morogoro kupitia tamko alilotoa kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Ukoma Duniani.

“Kwa mujibu wa takwimu za Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua kikuu na Ukoma (NTLP) za mwaka 2017, jumla ya wagonjwa wapya 1,933 waligunduliwa na hivyo kufanya kiwango cha ugunduzi kuwa watu 4 kwa kila watu 100,000.

“Takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuendelea kuwa miongoni mwa nchi 22 zenye wagonjwa wengi wa Ukoma duniani nchi nyingine ni India, Indonesia, Brazili, Ethiopia, Msumbiji, Nigeria na DRC Kongo.

“Hivi sasa bado kuna mikoa kumi ambayo inagundua wagonjwa wapya wa Ukoma wengi zaidi kila mwaka na kuchangia karibia 80% ya wagonjwa wote,” alisema

Aliitaja mikoa hiyo ni Lindi, Rukwa, Mtwara, Morogoro, Pwani; Tanga, Geita, Dodoma, Tabora na Kigoma.

Alisema bado zipo wilaya 20 ambazo kiwango cha ukubwa wa tatizo la Ukoma lipo juu sana na bado hazijafikia lengo la utokomezaji.

Alizitaja Wilaya hizo ni Liwale,  Lindi vijijini, Nachingwea, Ruangwa, Nanyumbu, Masasi mjini,  Pangani, Mkinga, Korogwe,  Mvomero, Kilombero, Morogoro vijijini, Ulanga, Shinyanga manispaa,  Mafia, Rufiji, Kilwa, Chato, Nkasi,  na Mpanda.

“Ni dhahiri ugonjwa huo umekuwa ukiogopwa mno katika jamii yetu toka enzi na enzi hasa kutokana na ukweli kwamba unasababisha ulemavu wa kudumu mwilini na kufanya waathirika kuwa tegemezi na kutothaminiwa,” alisema.

Alisema Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI inatekeleza shughuli mbali mbali katika kuhakikisha Ukoma unatokomezwa  kabisa.

SONONA

Inaelezwa asilimia 50 ya wagonjwa wa Ukoma hupatwa na sonona na huishi maisha ya huzuni na wasi wasi mkubwa.

Hayo yote husababishwa na mtazamo hasi wa jamii dhidi ya waathirika wa ugonjwa wa Ukoma. Mtazamo huo hasi ndio kikwazo kikubwa katika vita ya kutokomeza Ukoma duniani na hapa nchini.

Wakati huo huo, Wajumbe wa Kamati ya Kuzuia Ulemavu utokanao na Ukoma  Wilaya ya Mvomero wamefanya uchunguzi wa nyumba kwa nyumba katika kaya sita zenye wagonjwa wa ukoma.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Mratibu wa Shughuli za Kupambana na Kifua Kikuu na Ukoma Kilombero, Dk. Amani Nkilingi, alisema uchunguzi huo umelenga kuwaibua mapema waliopata maambukizi ili kuwaingiza katika mfumo wa matibabu.

“Tunapita katika familia ambazo zina wagonjwa wa ukoma, tunawachunguza ndugu wa karibuni naye, wale ambao wataonekana hawana dalili za ukoma wanapatiwa dawa kinga,” alisema.

“Tumewachunguza watu 26, tumewapa dawa kinga kwani hawakukutwa na dalili za ukoma lakini wanaishi karibu na wale waliowahi kuugua ukoma,” alisema.

Jumapili ya mwisho ya Januari, kila mwaka dunia huadhimisha siku ya Ukoma ambapo mwaka huu yataadhimishwa leo mkoani hapa.

Maadhimisho hayo, hapa nchini yanafanyika sanjali na maadhimisho ya miaka 60 ya uwepo wa Shirika la Ujerumani linaloshughulikia masuala ya Kifua kikuu na Ukoma (GLRA).

Shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia serikali kuhakikisha Ukoma unatokomezwa kwa kufadhili shughuli mbali mbali ikiwa ni pamoja na kutoa vyombo vya usafiri kwa waratibu wa Kifua kikuu na Ukoma nchi nzima.

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema   “Tutokomeze Ubaguzi, Unyanyapaa na Chuki Dhidi ya Waathirika wa Ukoma”.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,897FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles