Hayo yalielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Waryoba, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, mjini Moshi.
Alisema kwamba, kwa sasa Serikali ya wilaya hiyo imeanza kupitia upya  mikataba ya viwanda 75 vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji na kushindwa kufanya uzalishaji, ili viwanda hivyo viweze kurudi katika mikono ya Serikali na kubinafsishwa kwa wawekezaji wengine.
“Viwanda vilikufa kutokana na baadhi ya wawekezaji waliouziwa kutumia hati za viwanda hivyo kukopa mabilioni ya fedha katika mabenki na kuzifanyia biashara nyingine, jambo ambalo Serikali haipo tayari kulivumilia.
“Suala muhimu kwa sasa ni kufanya mapitio ya mikataba ya mauziano ya viwanda hivyo na hii itasaidia viwanda hivyo kurudi serikalini na kuvitoa kwa wawekezaji wengine.
“Naamini kama hivyo viwanda 75 vikifufuliwa, vitasaidia kupunguza changamoto ya ajira mkoani hapa.
“Katika kufanikisha hili, Serikali ya wilaya kwa kushirikiana na kituo cha uwekezaji, kanda ya kaskazini, tayari tumefanya tathmini ya viwanda vilivyokufa na sasa tupo kwenye jitihada za kuhakikisha tunafufua viwanda hivyo,” alisema Kippi.
Mbali na hilo, mkuu huyo wa wilaya alisema ili nia hiyo iweze kufanikiwa, Serikali itaanzisha mashamba ya kilimo cha umwagiliaji na kujenga masoko ya mboga mboga na mazao ya biashara ya kimataifa.
Katika hatua nyingine, Kippi alisema Serikali ya wilaya hiyo imetenga eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 14.06 katika eneo la Lokolova, kwa lengo la kujenga viwanda 12 na kuanzisha miradi mbalimbali, ikiwamo kujenga soko la nafaka la kimataifa.