MGOMBEA urais wa Chadema anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ametaja mambo manne ya msingi na mengine 16 atakayoshughulikia endapo atachaguliwa katika uchaguzi utakaofanyika kesho, huku akitoa jibu juu ya vilio vya Watanzania alivyovishuhudia wakati wa kampeni akisema: ‘Nimeona, nimesikia, nimeelewa na nitatenda’.
Akihutubia Taifa kwa njia ya televisheni, redio na hotuba yake kusambazwa katika mitandao ya intaneti jana jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema CCM imekuwa madarakani kwa zaidi ya nusu karne, hivyo imechoka na haina pumzi ya kuongoza Taifa.
“Watanzania sasa wanataka mabadiliko; mabadiliko ya kweli na ya uhakika. Tarehe 25 mwezi huu tuhakikishe tunaing’oa CCM madarakani na kuanza safari mpya ya kuleta mabadiliko,” alisema Lowassa ambaye pia katika hotuba yake hiyo alitafsiri dhana ya mabadiliko akisema ni kufikiri na kutenda tofauti na hali ilivyo.
Lowassa pia katika hotuba yake hiyo kabla ya kuelezea mikakati yake hiyo endapo atachaguliwa, alizungumzia kile alichokiita dhana na fikra potofu zinazojengwa na uongozi wa CCM kwa nia ya kuwaogopesha Watanzania kuhusu kuchagua upinzani, huku akivitaja vyama tawala vilivyoondolewa madarakani pasipo kutokea fujo ya aina yoyote kuwa ni UNIP cha Zambia, Chama cha Malawi Congress cha Malawi na Chama cha KANU cha Kenya vilivyoondolewa madarakani bila kutokea fujo yoyote.
Lowassa ambaye alitumia hotuba yake hiyo akisisitiza amani huku akisisitiza kuwa wanachama wao hawavunji, hawajavunja na hawatavunja sheria, alisema dhamira yao ni kushinda uchaguzi huu na kuing’oa CCM madarakani ambayo imekuwa madarakani kwa nusu karne lakini haina jipya na zaidi ikikosa pumzi ya kuongoza.
Mambo manne ya msingi
Akifafanua kuhusu mabadiliko atakayoyafanya endapo atachaguliwa, Lowassa aliyataja mambo manne ambayo ni mabadiliko ya Katiba yenye kuleta ukombozi mpya wa Mtanzania, ukombozi katika hali za maisha, mabadiliko ya mfumo wa uongozi na kutetea Katiba katika uadilifu na kupiga vita vitendo vyote vya rushwa na ufisadi.
Kuhusu mabadiliko ya Katiba, Lowassa alisema CCM ilikwamisha mchakato wa kupata Katiba mpya na endapo atachaguliwa atauanzisha tena ili ipatikane.
“Nikichaguliwa kuwa Rais, suala hili la Katiba mpya yenye masilahi kwa mwananchi litapewa kipaumbele…Hakuna maendeleo bila uhuru na haki. Mtanzania hana budi kuwa na madaraka ya Kikatiba juu ya maisha yake na kuweza kujisikia ana haki kamili na yuko huru katika nchi yake.”
Kuhusu ukombozi katika hali za maisha ya mwananchi, Lowassa ambaye alipinga dhana ya kufikiri na kutenda kana kwamba hatuna dharura ya maendeleo, alikishutumu CCM kutangaza takwimu za pato la Taifa ambazo hazionyeshi maisha halisi ya Mtanzania.
Katika hilo, Lowassa alisema Serikali yake itaboresha maisha hali kadhalika akisisitiza kuleta maendeleo bila kutegemea wafadhili na kwamba hilo litawezekana kwa Taifa kutumia rasilimali zake kwa ufanisi na kujiendeleza na si kuwanufaisha wageni na kuwafanya Watanzania watumwa katika nchi yao.
“Watu hawali takwimu. Watanzania wanataka milo mitatu yenye lishe bora; wanataka huduma bora za elimu, afya, maji safi na salama; wanataka umeme vijijini na ajira toshelezi kwa vijana, wanataka mapinduzi katika kilimo chenye tija na bei bora za mazao. Watanzania wamechoka na umasikini,” alisema.
Lowassa aligusia taarifa ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2015 kuhusu hali ya furaha ya wananchi katika nchi mbali mbali akisema katika mwaka 2013 kati ya nchi 156 zilizofanyiwa utafiti, Tanzania ilishika nafasi ya chini kabisa ya 151 ikidhihirisha kwamba Watanzania hawana furaha kabisa.
“Kwa vipimo hivi vitatu, Serikali ya CCM imeshindwa vibaya sana. Imefilisika. Baada ya zaidi ya miaka 50 ya Uhuru tunashuhudia kina mama wengi wanaotuzalia watoto wa Taifa hili na vichanga vyao vikizaliwa sio kwenye kitanda kilichotayarishwa bali sakafuni,” alibainisha Lowassa.
Aligusia pia utafiti na Taasisi ya Dunia iitwayo HelpAge kuhusu hali ya wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 na kusema CCM na Serikali yake imeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa kutowajali wazee.
“Tanzania katika mwaka wa 2015 inashika nafasi ya 91 kati ya nchi 96 zilizofanyiwa utafiti. Wagonjwa hawapati dawa hospitalini na hata wanaojiweza lazima wakatibiwe nje ya nchi; wenye mahitaji maalumu ya kibinadamu na ambao hawana njia ya ajira hawayapati; huduma za walemavu ni finyu pamoja na kuendelea kwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.” Alisema Lowassa ambaye katika hitimisho lake la hotuba hiyo alisisitiza kuwa maghorofa marefu yanapendeza lakini maendeleo ni watu.
Kuhusu mabadiliko ya mfumo wa uongozi, alisema Serikali ya CCM imekuwa na mfumo mbovu wa uongozi na uchumi kiasi cha kusababisha nchi kuingia kwenye deni kubwa la Taifa.
Alisema Serikali ya CCM imeingiza nchi katika deni kubwa katika historia ya nchi linalofikia Sh trilioni 35 hivi sasa, kutokana na matumizi mabaya ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Alisisitiza kuwa uongozi wake na ule wa Maalim Seif Sharif Hamad wa Zanzibar, hautakuwa wa kuyumba au kuyumbishwa bali wa kuthubutu katika utatuzi wa matatizo ya wananchi, uchapakazi na wa kuchukua maamuzi magumu kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho.
Akitaja jambo la nne, Lowassa ambaye alijipambanua kama ana hofu ya Mungu akiahidi kutenda kwa uadilifu mkubwa alisema ataheshimu Katiba kwa kufuata uadilifu, kupiga vita vitendo vyote vya rushwa na ufisadi na kuhakikisha kwamba rushwa inakuwa adui wa haki na maendeleo.
Mambo 16 ya kutekeleza
Akifafanua zaidi mambo 16 ambayo Serikali yake itayatekeleza, Lowassa alisema ataboresha elimu kama hatua ya kwanza ya kuwapa Watanzania uwezo wa kujikomboa.
Alisema pia ataondoa kodi zote za kero kwa wafanya biashara hususani wafanya biashara wadogo wadogo, mama lishe, bodaboda na machinga na kodi zote za mazao kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo wadogo ili kuongeza kipato na uwezo wao wa kuwekeza na kuliwezesha Taifa kujitosheleza kwa chakula na lishe bora.
Kuhusu sekta binafsi alisema ataimarisha uzalishaji wa bidhaa za ndani kwa kuwapa Watanzania upendeleo wa makusudi ili waimarike na waweze kuhimili ushindani.
Alisema Tanzania ina kodi nyingi kuliko nchi zote Afrika ya Mashariki na zile za SADC, kiasi cha kupoteza uwezo wa ushindani katika soko la ndani na la nje kutokana na ubovu wa miundombinu pamoja na urasimu hali ambayo imesababisha gharama za usafiri na usafirishaji kuwa kubwa kupita kiasi.
Alizungumzia pia ukuzaji wa viwanda vidogo vidogo ili viwe mhimili wa uchumi wa nchi kwa ajili ya uzalishaji na kusindika mazao ili kuongezea thamani na kutengeneza vyanzo vya ajira.
Kuhusu afya alisema ataimarisha huduma za msingi na kinga ili kuepukana na gharama kubwa za tiba.
Kuhusu uchumi alizungumzia udhibiti wa matumizi serikalini na katika mashirika ya umma kwa kupiga marufuku matumizi ya magari ya anasa, kupunguza safari za ndani na nje, usafiri wa anga wa daraja la kwanza na semina na makongamano yasiyo ya lazima na kuimarisha sekta ya gesi.
Aliongeza kuwa Serikali yake itadhibiti vitendo vya rushwa iliyokithiri katika bandari, ukwepaji kodi za ushuru wa forodha na kupiga marufuku misamaha ya kodi holela ili kuokoa mabilioni ya fedha yanayopotea kila wiki.
Lowassa pia alivitaja vyanzo vipya vya ajira kwa kukuza sekta za kilimo, viwanda na utalii na kuimarisha miundombinu na kujenga mtandao wa reli kwa kuanza kujenga upya na kwa viwango vya kisasa Reli ya Kati na Reli ya Tanga-Arusha-Musoma.
Kuhusu umeme alisema usambazaji wake utafika mijini, vijijini ili kufikia zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania ifikapo mwaka 2020.
Katika suala la Katiba mpya alisema atahakikisha inakuwepo ili kujenga misingi ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari na kuwapa nafasi asasi za kiraia, vyombo vya dola, Bunge na wananchi kusimamia uwajibikaji nchini.
Kuhusu masilahi ya kazi alisema Serikali yake itaunda Tume Maalumu ya kupendekeza mishahara ya watumishi serikalini, sekta ya umma na binafsi kwa maana ya kima cha chini cha mshahara.
Alisema pia Serikali yake itaimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, usalama na udugu wa Watanzania kwa misingi ya haki na usawa na kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Taasisi nyingine za kimataifa.
Ili kufanikisha mambo hayo, Lowassa alisema ataboresha mishahara ya wafanyakazi wa Serikali na ushauri wao wa kitaalamu utawekwa maanani na vitendea kazi vyao vitatiliwa mkwazo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi kwa kuzingatia mahitaji na masilahi ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi na Magereza na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB).
Kuhusu michezo na utamaduni alisema Serikali yake itahakikisha suala la michezo, utamaduni na sanaa linapewa kipaumbele maalumu.