NA AMON MTEGA, SONGEA
MIILI ya watu tisa waliokufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Mto Ruvuma wiki iliyopita, imepatikana.
Abiria hao waliokuwa wakazi wa Kitongoji cha Mkenda katika Kijiji cha Nakawale wilayani Songea, walikufa maji walipokuwa wakienda Kijiji cha Mitomoni wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk. Binilith Mahenge, alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea Julai mbili mwaka huu, saa 8.00 mchana.
Dk. Mahenge aliitaja miili iliyopatikana kuwa ni ya Omari Jela (11), Fadhili Hamisi (8), Hadija Said (41), Zurfa Aly (14), Awetu Mohamed (14), Omari Waziri (13), Stumai Abdallah (miezi mitano), Rajabu Machupa (17) na Tupishane Mustapha (5), wote wakazi wa Kijiji cha Mitomoni.
Pamoja na vifo hivyo, Dk. Mahenge alisema abiria 36 waliokolewa wakiwamo sita waliokuwa na hali mbaya.
“Pamoja na kufanikiwa kuipata miili hiyo, nawashukuru sana wote walioshiriki kuitafuta miili hiyo ukiwamo uongozi wa Halmashauri ya Nyasa kwa jinsi walivyotoa boti ya kisasa iliyofanya kazi ya kuitafuta miili ya wenzetu hao,” alisema Dk. Mahenge.
Wakati huo huo, Dk. Mahenge alisema wakati wa ajali hiyo, boti hiyo ilikuwa imejaza abiria na mizigo kupita kiasi.
Aliwaagiza wakuu wa wilaya zote za mkoa huo kuvitambua na kuvianisha vivuko vyote vilivyopo ndani ya wilaya zao kwa ajili ya kukabiliana na ajali zinazoweza kuepukika.