27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

MIHADARATI: MAPAMBANO YAKE NI YA KIDUNIA, TUJIPANGE

NA THOMAS MONGI,

NAAM sasa ‘naona’ kilicho ndani ya nafsi ya Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kijana kabisa watoto wa mjini wanaweza kusema ameamua  ‘kujilipua’ tena kwa moto wa gesi!

Kwa sasa dhamira na mori wa azma yake vinaanza kuthibitika katika kampeni yake ya kupambana na watumiaji, wauzaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya katika JijI lake la Dar es Salaam, jina lenye maana ya nyumba ya amani au salama.

Akizungumza  na waandishi wa habari katika programu aliyoiita ‘Awamu ya pili ya mapambano yake dhidi ya madawa ya kulevya’ Februari 6, 2017, aliwataja baadhi ya watu wenye ‘majina makubwa’ wakiwamo wafanyabiashara mashuhuri kama Yusuf Manji, wanasiasa akiwamo Mwenyekiti wa Chadema na aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2005, Freeman Mbowe, aliyekuwa Mbunge wa CCM Jimbo la Kinondoni, Idd Azzan na Mchungaji Kiongozi  Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.

Hawa walikuwa ni kati ya watu 65 , waliotajwa na Makonda na kuwa wanatakiwa kwa mahojiano  Februari 10, 2017.

Kuonesha vita hii ameidhamiria kwa dhati na si ‘usanii’ Makonda alinukuliwa akisema kuwa haoni kuwa vita hii ni kubwa kama isemwavyo na watu. Naendelea kusema kuwa Makonda yaonesha  umedhamiria kweli lakini siku zote ili uweze kupambana na adui yako vizuri na uweze pia kumshinda, kujua udhaifu na nguvu zake ni jambo la msingi sana.

Tsa Tzu (inatamkwa Sa Zu) ambaye alikuwa ni mtaalamu wa masuala ya kivita nchini China karne nyingi zilizopita katika kitabu chake kiitwacho ‘The Art of War,’ kikiwa ni miongoni mwa vitabu vilivyouzwa nakala nyingi duniani anasema  ‘Usiiingie katika vita yoyote bila kujua udhaifu  na nguvu za adui yako.’

Ni ukweli usiohitaji kutumia muda na nguvu nyingi kuuthibitisha juu ya nguvu kubwa  na mtandao thabiti walionao wafanyabiashara  haramu wa mihadarati au dawa za kulevya katika sayari yetu hii ya dunia. Nguvu hizo zimetokana na  uchumi mkubwa na uliotopea wanaoumiliki, kuwaweka mfukoni viongozi wa Serikali wasio waadilifu, kumiliki makundi au magenge yasababishayo hasara au mauaji kwa watu wanaowasumbua pia umiliki makundi ya utekaji katika nchi mbalimbali duniani.

Nchini mwetu Tanzania, haya matukio mazito hayajawahi kutokea na pia namuomba Mwenyezi Mungu atulinde nayo kwani amani ni kila kitu lakini tukumbuke na tujiongeze, pamoja na kudhani vita hii si ngumu au si  nzito bado kuna haja  ya kuongeza nguvu kubwa katika kupambana na wafanyabiashara hawa haramu.

Makonda naiona dhamira na ushujaa wako lakini ndugu yangu bila shaka unajua ni jinsi gani nchi tofauti duniani zinavyolia na kusaga meno kwa madhara na madhila ambayo waliletewa au ambayo bado wanaletewa na makundi ya wafanyabiashara hii haramu ya dawa  za kulevya.

Baadhi ya nchi zilizo kwenye heka heka kubwa katika kusumbuliwa na magenge ya matajiri wa dawa za kulevya ni pamoja na Columbia, Brazil, Chile na Mexico hizi zinatoka katika Bara la Amerika Kusini au Latini America, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria na Senegal kutoka Bara la Afrika, China, India na nchi zilizo Masharika ya Kati, barani Ulaya ni Italia, Ubelgiji na Uholanzi.

Jinsi mtandao wa biashara hii unavyogusa mabara yote duniani

Tukianzia barani Afrika, katika makala yake aliyoyapa jina la  ‘Diaspora and drug trafficking in West Africa’ ikiakisi Ghana na athari ya biashara za dawa za kulevya, Mwandishi Emmanuel Akyeampong, anaandika kuwa ’Uchunguzi unaonesha kuwa kiasi cha Dola za Marekani 20,000, kinamuwezesha mfanyabiashara wa dawa za kulevya wa Ghana  kufanya ‘Triangle Trip’ (safari ya mabara matatu kwa wakati mmoja), ambapo atafanya safari hadi India au Pakistan, huko hununua kiwango cha hali ya juu ya mihadarati iitwayo brown au kwa jina lingine off-white ambayo huinunua kwa takribani Dola za Marekani 4,500 kwa kilo, kisha hurudi Ghana, kwa ajili ya ufungaji upya na baadaye husafirishwa dawa hizo hatari hadi Marekani. Mfanyabiashara huyu hupata kiasi cha Dola za Marekani kati ya 100,000 hadi 150,000. Anayebeba hulipwa ujira wa Dola za Marekani kati ya 50,000 na 10,000…’

Mtindo huu wa biashara hii hata hapa Bongo hufanywa na wafanyabiashara hawa wa mihadarati, kwa kuwa unachunguza muda ukifika utagundua.

David Shirk katika ripoti yake iitwayo ‘The Drug War in Mexico’ anaonesha jinsi Mexico, inashirikiana na Marekani katika mapambano haya ambayo yanahusisha wafanyabiashara wakubwa ambao wanamiliki silaha pamoja na vikundi ambavyo wakati mwingine huanzisha mapigano ambayo husababisha mauaji katika sehemu mbalimbali, lakini pia makundi haya yamekuwa na ushawishi hata kwa viongozi wa umma nchini Mexico, kwa kuwahonga ili mambo yao yaende.

Wafanyabiashara hawa wa dawa za kulevya Mexico ndiyo kwa kiasi kikubwa wanaoingiza dawa za kulevya kwa kiasi kikubwa Marekani. Pamoja na nguvu za kifedha, kiuchumi na kiteknolojia lakini hadi sasa Marekani inalia kwa jinsi wananchi wake hasa vijana wanavyoathirika na dawa hizi hatari za kulevya mengi zikiwa zinatoka katika nchi zenye uchumi wa chini na teknolojia isiyotisha Mexico, lakini wameshindwa kuwazuia wauza unga wa Kimexico kuingiza dawa za kulevya kwenye ardhi ya Marekani!

Kwahiyo tunapomuona Rais wa Marekani, Donald Trump, akishinikiza kujenga ukuta kuzitenganisha Marekani na Mexico, tusidhani kuwa hajielewi…kuna sababu nyingi na kuteswa kwa watu anaowaongoza na dawa za kulevya toka Mexico ikiwamo.

Dk. Shreedhara Rao wa Taasisi ya Mafunzo ya Ulinzi na Uchambuzi (IDSA) katika Jiji la New Delhi nchini India, anaeleza jinsi uuzaji na usafirishaji wa dawa haramu za kulevya unavyosababisha vita na mzunguko wa fedha haramu katika jamii  barani  Asia, anasema biashara ya dawa ni tishio kwa usalama wa nchi, anaendelea kusema katika Asia wameshuhudia uanzishwaji wa makundi ya kiharamia kwa sababu ya fedha iliyopatikana kupitia ya biashara ya ‘unga’ Rao anatoa mfano wa makundi hayo ambayo yanaleta mashaka ya amani kama vile katika majimbo ya Jammu na Kashmir nchini India na Taliban nchini Afghanistan.

Ikiwa vita hii haitopewa kipaumbele tusishangae haya nasi yakatutoke, kwani fedha chafu za dawa za kulevya Tanzania zimeshaanza kufanya kazi ukweli, ndiyo huo.

Kuhusika kwa watu wenye dhamana nzito serikalini au wanaoheshimika kwenye jamii

Akyeampong, katika makala yake ya Diaspora and Drug trafficking in West Africa, anaeleza katika makala yake hayo jinsi baadhi ya watu waliopewa dhamana na nchi zetu kuwa mabalozi au kupewa nafasi yoyote nyeti ya Serikali wanavyoweza kusaliti kwa kufanya biashara haramu na zenye kuathiri uwezo wa kiakili wa watu wake bila huruma  hata chembe anaandika ‘Emmanuel Boateng Addo, pamoja na  Said Sinare Mkurugenzi Mtendaji wa Global Medical Supply na ambaye mwaka 1993 alikuwa Mbunge na Balozi wa Burkina Faso nchini Ghana.

Sinare akiwa balozi nchini Ghana, alimtengenezea pasi ya kusafiria feki yenye hadhi ya kidiplomasia Emmanuel Addo ya nchini Burkina Faso, wakati Addo ni raia wa Ghana. Sinare alikubaliana na Addo amsafirishie  heroine (madawa) kiasi kilo 7.5 hadi  Ufaransa  na baada ya kutua tu Ufaransa kabla ya kutimiza mpango wao huo haramu Emmanuel Addo alikamatwa jijini Paris. Hata hivyo Sinare alimwekea mwanasheria na ndani ya muda mfupi Emmanuel Boateng Addo, akaachiwa huru kwa kuonekana kuwa hana  hatia, hii ilikuwa Juni 1986…

Hapa tunamuona Sinare, pamoja na hadhi aliyonayo na heshima aliyopewa na nchi anahusika na uchafu mzito kabisa na yaelekea ni kigogo katika biashara hii na inawezekana mtandao wake wa kidunia ndiyo uliohakikisha Emmanue Addo, anakuwa huru pamoja na kuwa alikamatwa na dawa za kulevya na kwa wakati huo kiasi hicho hakikuwa kidogo.

Hebu soma kipande hiki uone jinsi wauzaji ‘unga’ wazoefu  na hatari wanavyojiweka katika macho ya jamii  ‘Raymond Amankwaah anaweza kuelezwa kama ni mbeba ‘unga’ au ‘mzigo’ (madawa ya kulevya) wa kimataifa kulingana na jinsi alivyoifanya biashara hiyo. Alikuwa kijana mtanashati (Handsome) kutoka kabila la Asante, alizaliwa katika familia yenye kipato cha kati na alikuwa na elimu ya kutosha Amankwaah angeweza kuwa hata mwanasheria lakini alijielekeza kwenye biashara, biashara ya dawa za kulevya. Alikuwa anaishi Ulaya, jijini London Uingereza, hakuwa anafahamika vizuri nyumbani Ghana kwa kuwa muda mwingi alikuwa nje, wengi walimfahamu kuwa ni mfanyabiashara tajiri.

Katika  miaka ya 90, aliweza kujenga kiwanda cha Ice cream  kilichokuwa kikiitwa Flamingo Food Ltd, katika Barabara ya Spintex road katika eneo la viwanda nchini Ghana. Pia alijenga nyumba nzuri ya kuishi katika eneo la watu mashuhuri vile vile alikuwa na kampuni iliyosajiliwa inayoitwa Himpex Ltd, ikiwa na ofisi katika Mtaa wa Kwame Nkrumah, lakini hakuna aliyejua biashara zake hasa zinahusiana na nini.

Lakini Aprili 1995 polisi wa Uingereza, baada ya miezi 18 ya uchunguzi dhidi ya  Amankwaah, ikagundulika kuwa Raymond Kwame Amankwaah ni mfanyabiashara mkubwa na hatari wa Cocaine (dawa za kulevya) duniani. Taarifa pia hii imepatikana katika makala ya Akyaempong.

Tanzania watu kama Amankwaah wapo wengi na katika majina yaliyokwishafika kwako Makonda, yasemekana wapo, jamani mpooo!

Vyombo mbalimbali vya habari duniani Juni, 2016 viliripoti  kuwa, Joaquin Guzman ‘El Chapo’, Mfanyabiashara haramu na hatari  wa dawa za kulevya alifanikiwa kutoka katika gereza lenye  ulinzi wa hali ya juu nchini Mexico, kutoroka kwake kulihusishwa na mbinu zilizofanywa na viongozi wa juu wa magereza nchini Mexico.

Mifano hii michache inaonesha usambazaji wa biashara hii haramu katika pande zote nne za  dunia, Magharibi, Mashariki, Kusini na Kaskazini zimeguswa na zahma ya biashara hii. Nchi yetu Tanzania ingawa haikutajwa kama nchi iliyoathiriwa na dawa ya kulevya kulingana na ripoti nyingi za kimataifa lakini ukweli tupo katika janga kubwa sana la kupotea kwa nguvu kazi nyeti ya Taifa letu kwani  vijana wengi wa Kitanzania kwa sasa wanatumia mihadarati.

Nafasi ya  Serikali katika mapambano haya

Kwa kuwa mapambano haya ni endelevu na haijulikani lini yatakwisha Serikali inatakiwa iwe na Bajeti maalumu katika kupambana na biashara  hii haramu ambayo imetandaa dunia nzima huku tukiwa tunashuhudia vijana wetu wapenzi wakipoteza maisha yao kwa matumizi haya ya dawa zisiyofaa, bila kuwa na Bajeti ya kupambana na wafanyabiashara hawa wenye ushawishi katika vyombo mbalimbali ndani na nje ya nchi yetu vita itakuwa ngumu.

Serikali pia inatakiwa kuwa na mkakati maalumu katika mapambano haya kwa kuhusisha si askari polisi pekee katika mapambano haya lakini ni vyema kuhusisha hata Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kama  India, Afrghanstan na Mexico zinavyoshirikisha wanajeshi wao na vyombo vya kutunga sheria.

Jeshi la Magereza nalo yabidi lipangwe vyema kwa kuwa bila kujipanga katika magereza yetu kuna uwezekano wafanyabiashara hawa hata kama wakifungwa wanaweza wakawa wanaendelea na biashara hizo kwa kutoa maelekezo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo simu, kwa mfano Mheshimiwa Makonda, katika mkutano huo alieleza kuwa baadhi wa wafanyabishara walioko gerezani sasa wanaendelea kufanya biashara zao kwa kutoa maelekezo mbalimbali kwa kupitia simu za mkononi.

Pia  kuwapo na vitengo vyenye hadhi bora katika mikoa na wilaya zote ambavyo vitakuwa kwa ajili ya kusaidia waathirika wa dawa za kulevya ambavyo vitakuwa na wataalamu wa kutosha kuwasaidia waathirika wa dawa ambao ni vijana wetu.

Mwisho

Watanzania tujue vita hii ni yetu, wazazi wa watoto walioathirika  wanaumia sana, wanashindwa wafanye nini kuwaokoa watoto wao ambao walitaraji waje kuwa ndiyo walezi na waokozi wao katika maisha yao ya utu uzima. Na tujue tukiwatazama wauza unga katika mitaa yetu na kuwaacha tu waendelee na ukatili wao huu wa kuangamiza kizazi chetu tutakuwa hatujaitendea haki jamii yetu, kumbuka   mtoto wako  kesho anaweza kuwa teja ikiwa leo utashindwa kumtaja muuzaji wa dawa za kulevya mtaani kwako.

Anachofanya Makonda ni cha kupongezwa na  anayebeza jitihada za Makonda katika kukumbusha ahadi ya Rais wakati wa Kampeni za Urais 2015 na pale alipolizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano pale Dodoma juu ya nia yake ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya, yatubidi tumuangalie kwa jicho la tatu kwa kuwa vita hii ni ya kila mtu na Taifa kwa jumla.

Tunaweza kusaidia kukosoa na kuelekeza pale tunapoona si sawa lakini si vyema kumshambulia Makonda, tubadilike ili tuweze kulinda afya za watu wetu na amani ya nchi yetu kwa jumla huku tukitambua kuwa vita hii ni ya kidunia tujipange vyema.

Tutashinda, naamini Mungu yupo pamoja nasi.

0713-690637

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles