30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Migogoro ya ardhi yamrudisha Lugola Morogoro

Na Felix Mwagara

-MOHA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, anatarajia kuwasili kwa mara nyingine mkoani Morogoro leo, kutatua migogoro ya ardhi ambayo imeibua mifarakano baina ya wananchi mkoani humo.

Lugola, wiki iliyopita alimaliza ziara yake mkoani humo iliyokuwa na lengo la kusikiliza kero za wananchi kuhusu utendaji kazi wa taasisi za wizara yake.

Katika ziara hiyo alifanya mikutano ya hadhara ambapo alikutana na migogoro mbalimbali, lakini kero kubwa kati ya hizo ni kuhusu ardhi ambayo inasababisha wananchi kuwekeana chuki, kujeruhiana, kufikishana polisi pamoja na kuuana.

Kati ya wilaya tatu alizozitembelea alipokuwa mkoani humo; Morogoro, Mvomero na Kilosa, licha ya wananchi kutoa kero zao mbalimbali, mgogoro wa ardhi uliibuka kwa sehemu kubwa hasa katika Wilaya ya KIlosa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Waziri Lugola alisema alipokuwa Kilosa, alikutana na mgogoro wa ardhi ambao umeleta mgawanyiko miongoni mwa mwananchi, hivyo akawaahidi kurejea tena wilayani humo kutatua kero zao baada ya kukutana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Lugola alisema mipango yote ipo sawa, hivyo anatarajia kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kilosa kesho Machi 15 ili kuwapa majibu ya kero zao na kumaliza mgogoro wa ardhi unaowakabili.

“Migogoro mingi inaletwa vituo vya polisi hasa Wilaya ya Kilosa, na wananchi katika mikutano yangu ya hadhara wanalalamika kuhusiana na ardhi, baadhi wanawalaumu polisi wangu kutokuwatendea haki na wengine pia wanawapongeza kwa kazi nzuri, na wengi wao wanalalamikia kuwa matajiri ndio wananyang’anya ardhi zao wakitumia fedha wakiwahonga polisi,” alisema Lugola.

Aliongeza kuwa alipokuwa katika mkutano wake wa mwisho katika Tarafa ya Kimamba, Wilaya ya Kilosa mkoani humo, kuliibuka na hoja nyingi za migogoro ya ardhi, na kutokana na usugu wa tatizo hilo, aliwaahidi kuwa atarejea tena kutatua mgogoro huo.

“Ziara yangu niliikatisha kwa ajili ya kwenda Dar es Salaam kuhudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri, hata hivyo, niliwaahidi wananchi nitakutana na Waziri wa Ardhi, ili tushirikiane kutatua mgogoro huu ambao unaweza ukaleta vurugu kubwa pale Kilosa na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla,” alisema Lugola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles