Na Mwandishi Wetu, Geita
Serikali imepanga kupeleka umeme katika migodi 336 nchini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa gharama ya takriban Sh bilioni Sita ili kazi za uchimbaji wa madini nchini zifanyike kwa tija na hivyo kukuza uchumi wa nchi.
Hayo yalielezwa Julai 15, 2022 wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, January Makamba mkoani Geita ambayo ililenga kukagua miradi inayotekelezwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara, kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Pamoja na migodi hiyo kusambaziwa umeme na REA, Waziri wa Nishati, alisema kuwa, TANESCO pia ina mkakati wa kufikia migodi mingi zaidi kupitia mradi wa Gridi Mapato ambao tayari una Sh bilioni 300 ambazo zitapeleka umeme kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwemo migodi na viwanda ili shirika hilo liweze kukua na kuongeza mapato.
Akiwa mkoani Geita, Waziri wa Nishati alikagua kazi ya upelekaji wa umeme katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na kueleza kuwa mgodi huo utaanza kutumia umeme wa gridi kuanzia mwezi wa Tatu mwaka 2023 na hivyo kuiongezea mapato TANESCO.
“Mgodi huu unaohitaji megawati takriban 40, tangu umeanza kufanya kazi umekuwa ukitumia jenereta za dizeli kuendesha mitambo, hivyo TANESCO italeta umeme wa gridi kutokea kituo cha mjini Geita pamoja na cha Mpomvu. Hii kwa TANESCO ni biashara kubwa sana itakayoingizia Serikali mapato,” amesema Makamba
Waziri wa Nishati pia alikagua shughuli za usambazaji umeme katika Jimbo la Busanda lililo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo vijiji vilivyounganishwa na umeme ni 26 kati ya Vijiji 84 na kuahidi kuwa vijiji vilivyosalia vitasambaziwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa Pili pamoja na mradi wa umeme wa Geita-Nyakanazi kwa vijiji vilivyopitiwa na mradi huo.
Akiwa katika kijiji cha Shilungule kwenye Jimbo la Busanda, Waziri wa Nishati alitembelea zahanati ya kijiji hicho ambayo inapata changamoto ya utoaji huduma kutokana na kutokuwa na umeme ambapo aliuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufunga mitambo ya umeme jua wakati zahanati hiyo inasubiri kusambaziwa umeme kupitia mradi wa Geita-Nyakanazi.
Waziri wa Nishati pia alifanya ziara katika Wilaya ya Chato na kuzungumza na wananchi katika eneo la Buselesele ambapo aliahidi kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote vilivyosalia wilayani humo pamoja na kuweka taa za barabarani kwenye eneo la Buselesele.
Ziara ya Waziri wa Nishati mkoani Geita pia ilihusisha ugawaji wa mitungi ya gesi kwa vikundi mbalimbali vya wanawake katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Busanda na Chato ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.