NA CHRISTINA GAULUHANGA
DAR ES SALAAM
WATANZANIA wametakiwa kuhakikisha wanalinda usalama wa bahari na maziwa  kuepusha kutoweka  samaki na viumbe vingine baharini.
Utafiti mbalimbali  unaonyesha hadi kufikia miaka 30 ijayo hakutakuwa na mazalia mapya ya samaki baharini bali kutakuwa na mifuko ya plastiki.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano sekta ya Uchukuzi, Stella Katondo alipozungumzia usalama wa bahari na maziwa katika maadhimisho ya Siku ya Bahari na Maziwa Afrika.
“Tuna changamoto kubwa za uchafuzi wa mazingira kupitia uchafu baharini hasa mifuko ya plastiki jambo ambalo linasababisha kufa mazalia ya samaki kadri siku zinavyoenda.
“Badala ya kuwa na samaki, mifuko ya plastiki inazidi kuongezeka baharini,  hali hiyo kama haitabadilika vizazi vya samaki vitazidi kutoweka,”alisema Stella.
Alisema serikali imeanza jitihada za kutoa elimu ya kuacha kutupa mifuko ya plastiki baharini kuokoa mazalia ya samaki kama utafiti wa  dunia  umetahadhalisha.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Giliard Ngewe alisema maadhimisho hayo ambayo ni ya kwanza Afrika yatasaidia kujenga uelewa wa jamii kuona umuhimu wa uchumi wa bahari.