26.2 C
Dar es Salaam
Friday, December 3, 2021

Miezi mitatu, majambazi 18 wauawa Mwanza

Na BENJAMIN MASESE

-MWANZA

IKIWA ni chini ya miezi mitatu tangu Novemba 16 mwaka jana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, limeripoti kuua watu 21 wanaodhaniwa kuwa majambazi.

Usiku wa kuamkia Novemba 16 mwaka jana, watu saba wanaodaiwa kuwa majambazi waliuawa katika mapambano ya kujibizana kwa risasi na askari polisi katika tukio lililotokea eneo la Kishili jijini hapa.

Januari 26, watu wanane waliuawa wilayani Ukerewe katika tukio la kushambuliana kwa risasi na polisi waliokuwa wanawafuatilia.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana, alisema tukio hilo lililodumu kwa dakika 45 lilitokea saa 7:40 usiku katika daraja linalounganisha vijiji vya Bukima na Igala wakati watu hao walikuwa katika mpango wa kwenda kufanya uvamizi.

Shana alisema walipata taarifa za siri kutoka kwa raia wema na zile za kitengo cha kiintelejensia kwamba kuna watu wanapanga njama za kufanya uhalifu wa kutumia silaha nyakati za usiku katika maeneo mbalimbali ya Kisiwa cha Ukerewe, ndipo wakatuma kikosi maalumu kufanya doria kali na kuweka mtego uliofanikiwa kuwaua na kukamata silaha.

Jana jeshi hilo mkoani Mwanza lilitangaza tena kuua watu watatu kati ya sita wanaodaiwa kuwa ni majambazi   waliokuwa wakijaribu kuvunja maduka ya wafanyabiashara eneo la Nyakabungo, Kata ya Isamilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Mwanza, Advera Bulimba alisema majambazi hao waliuawa saa nane usiku wa kuamkia jana baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema, kwamba eneo la Nyakabungo kuna watu wanavunja maduka kwa kutumia silaha za jadi huku wakipiga risasi za hewani.

Alisema baada ya polisi kufika eneo hilo, majambazi hao waliokuwa wakivunja maduka matatu walianza kuwafyatulia polisi risasi ndipo majibizano yalipoanza na kufanikiwa kuwaua watatu na wengine kutoroka na silaha ya moto na kutelekeza silaha za jadi zikiwamo panga, mkasi wa kukatia vyuma, nondo, sime na nyinginezo.

“Majambazi hao hawakufanikiwa kuiba chochote katika maduka hayo kwani polisi waliwahi kufika kabla ya kuingia ndani ya duka, hivyo hakuna hasara yoyote  iliyotokea na miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa Sekoutoure kwa uchunguzi na utambuzi.

“Kwa mujibu wa majirani wa eneo hilo ambao walikuwa wakichungulia madirishani walitueleza polisi kwamba majambazi hao walikuwa sita, hivyo tumeua watatu na wengine watatu wametoroka na bunduki ambayo hatujaijua ilikuwa ya aina gani, natoa wito kwa watu wenye nia ya kufanya uhalifu kuacha mara moja.

“Pia naomba wananchi kuendelea kutoa taarifa mapema kama walivyofanya wakazi wa Nyakabungo na polisi kuwahi kufika eneo la tukio na kuokoa wizi uliokuwa umekusudiwa na majambazi tuliyowaua, kikubwa tumejipanga sasa kuhakikisha raia na mali zao zinakuwa salama muda wote,” alisema Bulimba.

Hata hivyo MTANZANIA ilipotaka kujua sababu ya polisi kutotumia mbinu za kijeshi kuwanasa wahalifu wakiwa hai badala ya kuwaua, Bulimba alidai kuwa majambazi wengi wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kujihami kwa kutumia bunduki, hivyo ni lazima polisi watumie mbinu ya kuwaua ili kuwashinda.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,875FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles