23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

MICHANGO SHULENI PASUA KICHWA

Na WAANDISHI WETU-DAR/MIKOANI


UMEIBUKA mkanganyiko baina ya wadau wa elimu, wazazi na walezi wa wanafunzi kuhusu dhana ya utekelezaji wa utoaji elimu bure.

Mkanganyiko huo umeibuka baada ya kuwapo kauli tofauti kuhusu utekelezaji wa mpango huo ambazo zote zilitolewa hivi karibuni.

Mathalani baada ya Serikali kusitisha michango kwa shule za msingi na Sekondari na kuamuru fedha zirudishwe kwa waliochangia, wazazi katika Shule ya Msingi Ipuli Manispaa ya Tabora waliamua kugawana vyakula vilivyokuwa vimenunuliwa baada ya kuchangia.

Katika Shule ya Msingi Olympio, Jijini Dar es Salaam baadhi ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo wametishia kuandamana kwenda kwa Rais Dk. John Magufuli endapo suala la chakula kwa wanafunzi halitapatiwa ufumbuzi haraka.

Wakizungumza baada ya kikao cha wazazi mwishoni mwa wiki shuleni hapo, walisema kama watoto wao hawataruhusiwa kupata chakula cha mchana shuleni wako tayari kuandamana hadi kwa rais.

Mmoja wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina moja la Sprian alisema anashangazwa na shule hiyo kuingizwa kwenye mkumbo wa kuzuia michango shuleni ikiwamo ya chakula wakati ni ya kulipia tofauti na shule nyingine za Serikali.

“Kwanza Olympio si ni ya kulipia sawa na shule nyingine za binafsi licha ya kwamba ni ya serikali, kwa hiyo uamuzi wa kuzuia michango ya chakula ambayo wazazi tulijipangia kwa kushirikiana na kamati ya shule pamoja na walimu ni batili.

“Watoto wetu wanaamka saa 10 alfajiri wanakuja shuleni na kurudi saa 1 jioni, je hao watasoma au wanataka kuua watoto wetu? Nasikia baadhi ya watoto wameanza kuzimia kwa njaa, ingawa jambo hili linafanywa siri, hao wanaozuia watueleze kisayansi ni nani anaweza kusoma na njaa akafaulu, suala la michango shuleni badala ya kusaidia watoto wa masikini litadidimiza elimu yenyewe,” alisema Sprian.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Olympio, Enock Anyisile alisema wanaanda utaratibu mpya kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ambapo fedha za chakula hazitalipwa kwa walimu kama ilivyokuwa awali bali zitalipwa kwa mpishi moja kwa moja kupitia benki.

Hata hivyo, ushauri huo ulipingwa na wazazi ambao walitaka utaratibu wa awali wa kila mwanafunzi kutoa Sh 1,000 ya chakula uendelee.

Januari 17 mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alitoa onyo kali kuhusu uchangiaji michango shuleni huku akiwatahadharisha wakurugenzi wa wilaya husika.

Lakini juzi, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema serikali haijakataza wazazi kwa hiari yao kuweka utaratibu wa kuchangia chakula au michango mingine.

Akizungumza bungeni, alisema hakuna mahali ambapo serikali ama kwa kupitia waraka ama ufafanuzi wowote ambao umetolewa na viongozi umekataza wazazi kwa hiari yao kuweka utaratibu wa chakula na michango mingine shuleni.

“Baada ya sisi kukemea wale ambao walikuwa wanatoza michango kinyume na maelekezo kuna watu wengine wanataka kupotosha wanasema hadi vyakula kwa wanafunzi wa kutwa hawaruhusiwi kuchangia.

“Waraka umebainisha bayana majukumu ya wadau mbalimbali, wajibu wa mkuu wa shule ni kuwapa maelekezo wazazi kuhusu aina na vifaa vinavyohitajika mfano rangi ya kitambaa cha sare ya shule, idadi ya madaftari na kadhalika.

“Kilichokuwa kinajitokeza baadhi ya walimu walikuwa wanalazimisha wazazi kununua sare shuleni kwa bei kubwa ukilinganisha na mzazi ambavyo angeweza kununua,” alisema Ndalichako.

Kuhusu suala la chakula, alisema mkuu wa shule na kamati yake wanatakiwa kushirikiana na jamii kuweka utaratibu wa kutoa huduma hiyo pamoja na nyingine.

“Kwenye suala la chakula ambalo limeleta sintofahamu huu waraka unasema wazi, kwamba ni jukumu la mkuu wa shule kushirikiana na jamii kuweka utaratibu wa kutoa huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa au kutoa chakula na huduma nyingine kwa wanafunzi wa hosteli.

“Lakini kwenye kamati ya shule unasema ni jukumu la kamati kushirikiana na jamii kuweka utaratibu wa kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi wa hosteli.

“Hivyo wakurugenzi na watu wote ambao wanasimamia utaratibu huu kuhakikisha kwamba wanazingatia waraka huu kama ambavyo umeainishwa,” alisema.

MWONGOZO WA SERIKALI

Desemba 14, 2015 Serikali ilitoa waraka wa elimu bila malipo huku ikiainisha majukumu ya wazazi na walezi.

Kulingana na waraka huo, wazazi wana jukumu la kununua sare za shule, vifaa vya kujifunzia, chakula kwa wanafunzi wa kutwa na matibabu kwa watoto wao.

Pia wanatakiwa kulipa nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo, kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika hosteli za serikali.

Wazazi na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea nguvu kazi na mali ili kuleta ustawi wa maendeleo ya shule zilizoko ndani ya jamii.

Katika waraka huo, Serikali ilisema wizara ina jukumu la kugharamia utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kulingana na idadi ya wanafunzi, kutenga fedha za udhibiti ubora wa shule na fedha za kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimu bila malipo na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi.

WADAU WA ELIMU, WAZAZI

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alishauri wazazi wabebe majukumu yao kwa yale wanayoona yanafaa lakini si kwa kulazimishwa.

“Watu wanatakiwa kumwelewa Rais, asichokitaka ni watu kulazimishwa au watoto kurudishwa nyumbani kwa kudaiwa michango.

“Michango iratibiwe na wazazi kwa kupitia kamati zao, wakiamua kufanya jambo wafanye lakini lisiathiri taaluma ya mtoto,” alisema Dk. Bana.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), Profesa Gaudence Mpangala, alisema Serikali inatakiwa iainishe ni masuala gani yanagharamiwa na yapi hayagharamiwi.

“Wadau na wataalamu wakae wajadiliane pamoja halafu wizara iandae muswada na kuupeleka bungeni ukajadiliwe na kuwa sheria, hapo wazazi watakuwa wanajua wanachangia kwa mujibu wa sheria,” alisema Profesa Mpangala.

Alisema suala la elimu bure ni zuri kwani lilikuwepo tangu enzi za Ujamaa lakini wakati huo wanafunzi walikuwa wachache na hata shule pia zilikuwa chache.

Naye Said Zimbwe mwenye mtoto wa darasa la kwanza anayesoma katika Shule ya msingi Kinyantila, Temeke, alisema mpaka sasa hajui anachopaswa kuchangia ama kutochangia.

“Kutokana na hali hii mimi naona baadhi ya shule zitaendelea kuwatoza wazazi michango ama kuwaomba wachangie vitu tofauti na ambavyo wengi wetu tuliamini sasa hatutachangia chochote,” alisema Zimbwe.

Mzazi mwingine Julieth Shemweta, alisema; “Tuliaminishwa kwamba hakuna michango, mbaya zaidi kuna wenzetu walirudishiwa michango halafu leo hii wanasema tulielewa vibaya sijui kama kuna mtu atakubali tena.

SONGWE

Mkoani Songwe Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, limeazimia kuwa suala la kuchangia chakula katika shule za msingi na sekondari liamuliwe na wazazi kwa kuwa lina umuhimu kwa maendeleo ya taaluma ya watoto wao.

Wakizungumza wiki iliyopita wakati wa kikao cha kujadili mapitio ya bajeti ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2017/18 Mjini Vwawa, baadhi ya madiwani walisema tangu ulipoanzishwa mfumo wa kuchangia chakula kwenye shule za msingi na sekondari utoro umepungua kwa kiwango kikubwa.

Diwani Kata ya Ipunga, Barton Sinienga, alisema licha ya Rais Dk. Magufuli kutoa agizo la kupiga marufuku michango lakini wao kama wazazi ni lazima wachangie vyakula ili kuongeza umakini kwa wanafunzi.

Sinienga alisema watafiti mbalimbali wa masuala ya elimu walitoa ripoti kwamba wanafunzi wengi walikuwa wanafanya vibaya kwenye mitihani yao kutokana na kukaa muda mrefu shuleni bila kupata chakula.

Diwani wa Kata ya Halungu, Maarifa Mwashitete alisema halmashauri hiyo inapaswa kuangalia mbinu zitakazowezesha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya kujfunza na kujifunzia.

Alisema mbinu kubwa ya kuwafanya watoto wafanye vizuri ni kuwapa chakula shuleni na kwamba katika kata yake tangu mfumo wa kutoa chakula uanze kumekuwa na ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba kutoka asilimia 52 mwaka jana hadi kufikia asilimia 72 mwaka huu.

Ofisa Elimu Shule za Sekondari wilaya humo, Hosana Nshullo na Ofisa Elimu Shule za Msingi, Sophia Shitindi walisema mfumo wa utoaji chakula katika shule mbalimbali umechangia ongezeko la ufaulu kwa asilimia kubwa na kupunguza utoro.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Erick Ambakisye, alisema baadhi ya wanafunzi katika halmashauri hiyo wanalazimika kutembea umbali mrefu kutoka shuleni hadi nyumbani hivyo suala la chakula ni muhimu kwa watoto.

KILIMANJARO

Wadau wa elimu mkoani Kilimanjaro wamekosoa hatua ya Serikali ya kupiga marufuku michango katika shule za serikali na msingi kwa madai kuwa jambo hilo litachangia kushuka kwa ufaulu.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Majengo iliyopo mjini Moshi, Peter Lyimo alisema hatu ya serikali kupiga marufuku michango shuleni inafaa kupingwa kwa nguvu zote kutokana na ukweli kuwa itaathiri ufaulu.

Alisema kuzuia michango shuleni kutaleta matokeo mabaya kwa wanafunzi katika elimu na kwamba kila mzazi ana jukumu  na wajibu wa kusaidiana na serikali kumpatia mtoto elimu bora.

 

“Wazazi wana jukumu la kuhakikisha mtoto anapata chakula, malazi, sare za shule, kalamu. Serikali haina uwezo wa kufanya kila kitu hata kwenye nchi za wenzetu wazazi wana majukumu yao na serikali pia ina majukumu yake hivyo hatua ya kupiga marufuku haitasaidia,” alisema Lyimo.

Alisema elimu haiweza kuendeshwa kwa matamko na kutoa wito kwa serikali kukutana na wadau wa elimu ili waweze kutoa mchango wa namna ya kuendesha elimu hapa nchini.

Nao baadhi ya wakuu wa shule za sekondari na msingi za serikali ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, walisema onyo hilo litaleta athari kubwa katika sekta ya elimu siku za usoni.

 

Walisema shule nyingi za serikali zinakabiliwa na changamoto lukuki ambazo zilikuwa zikitafutiwa ufumbuzi kupitia michango.

 

“Michango inatusaidia sana kwa mfano hapa shuleni kwetu hatuna walimu wa sayansi na hesabu lakini tumekubaliana na wazazi tuwaajiri na wao watawalipa, sasa serikali inaposema hakuna michango hali hii itaathiri taaluma,” alisema mmoja wa walimu hao.

 

MBEYA

Baadhi ya walimu katika shule za msingi na sekondari jijini Mbeya wameiomba serikali kusambaza waraka unaohusu michango shuleni ili kuondoa sintofahamu iliyojitokeza.

Wakizungumza na MTANZANIA jana kwa nyakati tofauti, baadhi ya walimu ambao hawakuwa tayari kutajwa majina yao gazetini walisema asilimia kubwa ya wazazi na walezi wamepokea kauli ya Rais kwa mitazamo tofauti hivyo kusababisha suala la michango ya hiari lililokuwa likifanywa na jamii kuwa gumu.

Walisema jamii kwa sasa imeamua kuiachia serikali masuala yote hasa kuhusu chakula kwa wanafunzi ambalo lilikuwa likifanyika kwa makubaliano baina ya kamati za shule na wazazi na kupunguza vitendo vya utoro na uchelewaji wa wanafunzi darasani.

“Tumemsikia Waziri Ndalichako bungeni akizungumzia na kutolea ufafanuzi kauli ya Rais, ni vema waraka huo ukasambazwa kwenye shule ili kusaidia kupunguza sintofahamu hii,”alisema mmoja wa walimu ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Walimu wengine walisema kwa sasa wazazi wamegoma kuendelea na michango wakidai kwamba serikali imesema itagharamia jambo ambalo halina ukweli.

Habari hii imeandaliwa na Nora Damian (Dar), Upendo Fundisha (Mbeya), Upendo Mosha (Kilimanjaro), Ibrahim Yassin (Songwe).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,226FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles