Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio, amechaguliwa kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni baada ya Josephat Rwegasila kumaliza muda wake.
Urio amechaguliwa kwa kura zote za ndio 21 kutokana na kuwa mgombea pekee katika uchaguzi huo ulifanyika leo Agosti 2024 kwenye Ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kumtangaza Naibu Meya huyo, Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge ameahidi kumpa ushirikiano wa dhati katika kazi zote watakazofanya.
“Urio karibu ufanye kazi, umeahidi utanisaidia naomba unisaidie. Kawaunganishe madiwani wakusaidie,” amesema Songoro.
Kwa upande wake, Urio amewashukuru madiwani wenzake na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano katika kipindi kifupi alichopewa na kufikia malengo waliyokusudia.
“Nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi ambacho ndicho kilichonilea, sijawahi kufanya siasa kwenye chama kingine.Nawashukuru sana viongozi wangu kuanzia wa shina hadi Taifa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Urio.
Miongoni mwa changamoto ambayo ameahidi kuhakikisha inatatuliwa ni hali ya miundombinu ya barabara hasa katika jimbo la Kawe.
“Jimbo la Kawe tuna changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara na toka mvua zimenyesha barabara nyingi hazipitiki,” ameeleza Naibu Meya huyo.
Urio atadumu katika nafasi hiyo hadi Oktoba, 2025