MIAKA MINNE YA JPM: Ilipotoka Muhimbili na ilipo sasa

0
1826
Wagonjwa wa figo wakipata huduma ya kusafishwa damu.

Na  AVELINE  KITOMARY

SIKU nne mara baada ya kuapishwa Novemba 5, mwaka 2015, Rais Dk. John Magufuli, alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo alibaini kasoro mbalimbali ikiwamo mashine za CT-Scan na MRI kuharibika na kero ya vitanda kuwa vichache.

Kutokana na changamoto hizo, Rais Magufuli aliamua kufanya mabadiliko katika usimamizi wa hospitali hiyo kutokana kusikitishwa na hali ya uhaba wa vitanda na kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi. Rais alikuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili, ilihali mashine kama hizo katika hospitali binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa sehemu ya kwenda kutafuta huduma.

Rais aliamua kumteua Profesa Lawrence Museru, kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo na kumsimamisha Hussein Kidanto, ambaye alikuwa Kaimu Mkuu wa hospitali hiyo, huku akimtaka arudi Wizara ya Afya kwaajili ya kupangiwa majukumu mengine.

Licha ya uteuzi huo, Rais pia alivunja bodi ya usimamizi ya hospitali hiyo, ambayo ilikuwa tayari imemaliza muda wake wa kuhudumu na kutaka uongozi mpya kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinatengenezwa na kuhudumia wananchi ipasavyo. 

Hata hivyo, kwa miaka minne ya uongozi wake mafanikio ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa viongozi hao yameoneka, kwa kiasi kikubwa huduma imeimarika.

Maagizo mengine yaliyotolewa na Rais yalikuwa ni kushughulikia tatizo la ukosefu wa dawa, wagonjwa waliokuwa wakilala chini kupewa vitanda, kulipa stahiki za wafanyakazi, kuboresha mazingira ya kazi, kununua na kuboresha vitendea kazi na kutoa huduma bobezi ili kupunguza rufaa za nje.

UTEKELEZAJI WA MAAGIZO

Rais Dk. John Magufuli akiwafariji wagonjwa Muhimbili.

Mkurugenzi Mtendaji wa (MNH), Profesa Lawrence Museru, anasema katika miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli, hospitali hiyo imeweza kutekeleza maagizo yaliyotolewa huku mikakati mipya ya usimamizi ikiundwa.

Kwa mujibu wa Profesa Museru, Serikali imewekeza kiasi cha Sh bilioni 37.405 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba na mashine, uboreshaji wa miundombinu na kuwajengea uwezo wa wataalamu.

“Matengenezo ya mashine ya MRI yalifanyika kikamilifu, hadi sasa mashine hii inaendelea kufanya kazi vizuri. Pia matengenezo ya mashine ya CT-Scan nayo yalifanyika na bado  inaendelea kufanya kazi vizuri tangu ilipotengenezwa Desemba, 2015. 

“Upatikanaji wa dawa umekuwa mzuri tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. Sasa hivi wagonjwa wanapata dawa kwa zaidi ya asilima 96 kutoka kwenye maduka ya hospitali ukilinganisha na wastani wa asilimia 40 kabla ya uboreshaji. Hospitali ilianzisha mfuko maalumu kwa ajili ya dawa (Drug revolving fund) ambapo fedha zote zinazopatikana kutokana na mauzo hutumika kwaajili ya ununuzi wa dawa na jumla ya Sh bilioni 1.5 hutumika kununua dawa kila mwezi, sawa na Sh bilioni 18 kwa mwaka. Hadi sasa hospitali imenunua dawa na kuwapa wagonjwa  zenye thamani ya Sh bilioni 72,” anaeleza Profesa Museru.

Anaongeza: “Agizo la vitanda lilitekelezwa kufuatia kuhama kwa wagonjwa wa Taasisi ya Mifupa (MOI), kutoka wodi za Hospitali ya Taifa Muhimbili walizokuwa wakitumia ambazo ni wodi 17 na 18 zilizopo jengo la Sewahaji pamoja na wodi namba 2 iliyopo jengo la Mwaisela, ambayo kwa sasa ni ICU yenye vitanda 15. Baada ya jengo hilo kubadilishwa hospitali ilipewa jengo lililokuwa likitumiwa na Wizara ya Afya kama ofisi ambalo kwa sasa limekuwa wodi yenye nafasi ya vitanda 91. 

Anabainisha maagizo mengine yaliyotolewa na Rais kuwa ni kuwalipa wafanyakazi wa hospitali hiyo na kuboresha mazingira ya kazi, agizo ambalo tayari limetekelezwa.

“Katika kipindi cha miaka minne, hospitali imeweza kulipa wafanyakazi malimbikizo ya madai yao waliyokuwa wakidai kwa kipindi kirefu. Malipo ya wauguzi wanaokesha usiku, posho mbalimbali hususani kwa madaktari na kada nyingine za afya zinazoshughulika moja kwa moja na wagonjwa. 

“Malipo mengine ni nauli za likizo, hali iliyochangia wafanyakazi kuwa na ari ya kujituma zaidi,” anasema.

HUDUMA BOBEVU  ZILIZOANZISHWA

Profesa Museru anasema hospitali hiyo imeanzisha huduma nyingi za ubobevu ili kupunguza rufaa za nje ya nchi, ambapo kiasi cha Sh bilioni 32.149 zimeokolewa.

Anasema wakati wanaanza kutoa huduma hiyo, hospitali ilipeleka wataalamu mbalimbali wa afya ili kupata mafunzo ambayo yamegharimu Sh bilioni 3.597.

“Hospitali ilipeleka wataalamu nje ya nchi kwaajili ya kupata mafunzo, miongoni mwao walikuwamo madaktari bingwa, wauguzi, wataalamu wa maabara, wataalamu wa radiolojia, magonjwa ya mfumo wa chakula na ini.

“Pia tulipeleka watalaam wa saratani za damu ili kupata ujuzi na elimu ya kutoa huduma hizi kwa ufanisi, hali iliyowawezesha Watanzania wengi kuhudumiwa hapa nchini badala ya kupelekwa nje, pia imesaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha serikalini,” anasema. 

Anataja huduma za ubobevu zilizoanzishwa kuwa ni pamoja na upandikizaji wa vifaa vya kusaidia watoto kusikia, upandikizaji wa figo, tiba radiolojia, tiba na uchunguzi wa mfumo wa chakula na ini, vyumba vya upasuaji, tiba ya saratani na mfumo wa oxygen wodini.

Anafafanua: “Kwa mara ya kwanza Hospitali ya Taifa Muhimbili ilifanikiwa kuanzisha huduma ya upandikizaji wa vifaa vya kusaidia watoto kusikia (cochlear implant), ambapo wagonjwa 34 wamenufaika, wawili kati yao wamelipia matibabu wenyewe na 32 Serikali ilitoa gharama ya Sh bilioni 1.15 sawa na Sh milioni 36 kwa mgonjwa mmoja. Fedha iliyookolewa ni Sh bilioni 2.05 kama wangetibiwa nje ya nchi kwa gharama ya Sh milioni 100. 

“Novemba 2017, Tanzania iliandika historia ya pili baada ya Muhimbili kufanya upandikizaji wa figo kwa mara ya kwanza.

“Tangu kuanzishwa kwa huduma hii, wagonjwa 51 wamenufaika. Serikali iliweza kutoa Sh bilioni 1.530 kwa gharama ya Sh milioni 30 kwa mgonjwa mmoja hivyo, iwapo wangeenda kutibibiwa nje ya nchi, Serikali ingelazimika kutumia Sh bilioni 6.120 kwa kila mgonjwa. Hivyo, Serikali imeokoa Sh bilioni 4.590.

“Kabla ya huduma hii kuanza nchini, Serikali ilisafirisha wagonjwa 150 nje ya nchi katika kipindi cha miaka 15, wastani wa wagonjwa 10 kwa mwaka ambapo kwa miaka miwili, imefikia asilimia 34 ya wagonjwa waliopelekwa nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 15,” anabainisha.

Profesa Museru anasema kwa upande wa huduma za radiolojia, wagonjwa 558 tayari wameshatibiwa ambapo kati yao 274 walikuwa na uvimbe wa kinywa.

“Gharama huwa ni Sh milioni nane kwa mgonjwa mmoja, kama wangeenda nje ya Serikali ingelazimika kutoa Sh bilioni 26.304 sawa na Sh milioni 96 kwa mgonjwa mmoja kwa safari nne zinazohitajika. Kwa maana hiyo Serikali imeweza kuokoa Sh bilioni 24.112.

“Pia tumeboresha huduma za uchunguzi kwa wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa chakula na ini. Wagonjwa 380 walipata huduma kwa gharama ya Sh milioni 116.82 ambao kama wangeenda nje ya nchi gharama ingekuwa Sh bilioni 1.51 hivyo, hospitali imeokoa Sh bilioni 1.39,” anasema na kuongeza:

“Kwa upande wa huduma  ya uchunguzi wa ugonjwa wa saratani na matibabu ya awali kwa wagonjwa wenye tatizo hilo, hospitali inakamilisha mipango ya uanzishwaji wa huduma ya upandikizaji uloto (bone marrow transplant) ifikapo mwishoni mwa Desemba, 2019 au mapema mwakani. Hospitali imetumia Sh milioni 117 kwa ajili ya mafunzo hayo, fedha zilizotokana na vyanzo vya ndani vya mapato hospitalini.” 

Anasema pia ili kuendana na kasi ya ongezeko la wagonjwa na uanzishwaji wa huduma mpya, umefanyika ukarabati na kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka 13 hadi 20 vikiwamo viwili vya upasuaji maalumu kwa ajili ya watoto na wagonjwa wanaohitaji kupandikizwa figo. 

“Hospitali imepunguza msongamano wa wagonjwa kusubiri tarehe ya mbali ili kufanyiwa upasuaji. Vyumba vya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU) pia viliongezeka kutoka vitanda 25 hadi 78 ambavyo vimejengwa na kuwekewa vifaa tiba, ukarabati huo wote umegharimu Sh bilioni 2.46.

Anataja ukarabati mwingine kuwa ni wodi za mfumo wa oksijeni ambayo ina vitanda 28, mashine za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo kutoka 17 hadi 42 na ukarabati wa majengo mengine.

“Hii imesaidia wagonjwa wa kiharusi kuonwa kwa utalaam zaidi na kuwa na uangalizi wa karibu ikilinganishwa na ilivyokuwa awali walipokuwa wakilazwa katika wodi za kawaida.

“Wale wanaohitaji oxygen sasa wanapata kupitia bomba zilizounganishwa wodini hivyo kuondokana na adha ya kubeba mitungi. Ukarabati huo wote umegharimu Sh milioni 650. 

“Hospitali imeongeza mashine za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo kutoka 17 hadi kufikia 42 sawa na ongezeko la mashine 25 kwa gharama ya Sh milioni 629.2. 

MAFANIKIO YA MLOGANZILA

Oktoba 03 mwaka jana, Serikali iliagiza hospitali hiyo kuwa chini ya usimamizi na uendeshaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) hivyo, kwa sasa inaitwa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.

Uamuzi wa kusimamiwa na Muhimbili umesaidia kuendelea kutoa huduma za ubobezi kutokana na kuwa miundombinu na vifaa tiba stahiki.

Profesa Museru anaeleza kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ni pamoja na upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe katika mishipa ya damu kwenye ubongo na matatizo ya mgongo.  

“Kwa mara ya kwanza ilifanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe katika mishipa ya damu kwenye ubongo (cerebral aneurysms) kwa wagonjwa wanne,  gharama za upasuaji kwa mgonjwa mmoja ikiwa ni Sh mililioni 20 wakati nje ya nchi ingegharimu Sh milioni 40. Wagonjwa wanne wamegharimu Sh mililioni 80 badala ya Sh mililioni 160 ambayo ingetumika iwapo wangekwenda nje ya nchi hivyo, Serikali imeokoa Sh milioni 80.

“Pia inafanya upasuaji wa ubingwa wa juu wa matatizo ya mgongo hivyo, inakuwa ya pili ya umma nchini kutoa huduma hii baada ya MOI.

“Mafanikio mengine ni wagonjwa kupunguzwa Muhimbili, ambapo wagonjwa 869 wamepokelewa Mloganzila na kupatiwa huduma, hatua ambayo imepunguza msongamano wa wagonjwa Muhimbili.

MPANGO KUPANDIKIZA MIMBA 

Mipango tuliyonayo ni miwili mikubwa, kwanza ni kujenga kituo cha umahiri upandikizaji viungo yaani ‘transplanta center.’ Serikali imetoa fedha za kuanzia kujenga kituo hiki na sasa hivi usanifu unafanyika ili kukijenga Mloganzila.

Kwa mujibu wa Profesa Museru, tayari Sh bilioni nne zimeshatengwa  kwaajili ya huduma ya upandikizaji mimba (IVF) na tayari wataalamu wameshapata ujuzi wa kufanya hivyo.

“Hili la IVF nalo litaanzishwa  kwa mfumo ule ule, tumeshapeleka wataalamu India wameona namna ambavyo upandikizaji mimba unavyofanyika kwenye public institution,  miundombinu gani na vifaa gani vinahitajika. Kwahiyo, sasa hivi mafundi wetu wameanza usanifu wa kukarabati jengo Muhimbili litakalotumika mwanzo  kabla ya lile kubwa linalojengwa Mloganzila.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here