24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 60 ya Uhuru| Wizara ya Kilimo kusaidia wakulima kulima kwa tija

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

WIZARA ya Kilimo imesema mwelekeo wake hiyo ni kujikita katika utafiti lengo likiwa ni kumsaidia mkulima aweze kulima kwa tija.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Novemba 28,2021 jijini Dodoma, Waziri wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda, kuhusu mafanikio ambayo yamefikiwa katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara, amesema utafiti ndio kipaumbele cha Serikali.

“Utafiti ndio kipaumbele chetu lengo tupate mbegu bora ambazo zitawasaidia wakulima, ili kufanya vizuri katika kilimo mikakati yetu ni kujikita katika utafiti kwa kuwasaidia watafiti kuweza kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia na kuleta tija katika sekta ya kilimo.

“Wizara imeongeza vituo vya utafiti kutoka vitano mpaka 17 lengo likiwa ni kuweza kupata mbegu bora ambazo zitawasaidia wakulima kulima kilimo chenye tij,” amesema Prof. Mkenda.

Sehemu ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano huo.

UHABA WA MAFUTA

Alipoulizwa kuhusiana na uhaba wa mafuta nchini Prof. Mkenda amesema serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuanzisha kampeni ya kulima zao la alizeti pamoja na kilimo cha michikichi lengo likiwa ni kupata mafuta ya kiutosha.

“Kwenye michikichi itachukua muda mrefu kidogo na tutaenda mbali zaidi kuhakikisha tunajitosheleza katika kila kitu ikiwemo kwenda mpaka katika soya,”amesema Prof. Mkenda.

TIJA NDOGO

Prof. Mkenda amesema changamoto kubwa ambayo wanakutana nayo ni tija ndogo ambapo amedai wakiingia katika soko lazima tija iwe kubwa ili waweze kushindana katika biashara.

“Mchango wa kilimo kwenye uchumi ni asilimia 26 na mazao ni asilimia 15 na nimesema nchi ikiendelea mchangao unapungua lakini mchango wa kilimo katika ajira lazima upungue zaidi, sisi bado watu ambao wanategemea kilimo moja kwa moja ni asilimia 58 maana yake ni tija ndogo,”amesema

Amesema kiwango hicho kimepungua ikiwanganishwa na asilimia 90 ya wananchi waliokuwa wakitegemea kilimo, lakini hivi sasa kuna hatua kubwa imepigwa ambapo imesalia asilimia 58 pekee.

UGANI NA KUWAFIKIA WAKULIMA WENGI

Aidha, Prof. Mkenda amesema kwa sasa Watanzania wameongezeka tofauti na miaka ya nyuma, hivyo wanahitajika Maafisa Ugani wengi ambao watawafikia wakulima kiurahisi.

Amesema kutokana na umuhimu huo mwelekeo wa wizara hiyo ni kuzidi kuongeza maafisa ugani ikiwa ni pamoja na kuwapatia pikipiki na kuongeza bajeti.

“Tunanunua pikipiki kwa ajili maafisa ugani lengo likiwa ni kuwafikia wengi ikiwa ni pamoja na kufanya mafunzo,”amesema

JITIHADA KATIKA UMWAGILIAJI

Aidha, ameongeza kuwa serikali itaendelea kuongeza jitihada katika kilimo cha umwagiliaji ikiwa ni pamoja na kufungua Skimu za umwagiliaji ambapo amedai wameongeza bajeti lengo likiwa ni kuwafikia watu wengi.

MASOKO

Prof. Mkenda amesema Wizara imekuwa ikitafuta masoko mbalimbali kwa ajili ya wakulima ambapo amedai kwa sasa wanataka kuvitumia vyama vya ushirika ili kuweza kuuza nje ya nchi.

“Tunaongeza jitihada katika masoko sasa hivi tuna kituo Juba Sudani Kusini na tumeanza kuuza unga Kenya na tunataka kuuza katika maeneo mengine,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles