MIAKA 56 YA MAPINDUZI Dk. Shein atoa onyo kali Z’bar

0
759

Na ANDREW MSECHU -DAR ES SALAAM

IKIWA imebaki miezi michache kuelekea Uchaguzi Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Dk Ali Mohamed Shein, ametoa onyo kwa watu wanaotaka kuvuruga amani na katu serikali  hatomvulia mtu yeyote  kwa kisingizio cha kudai haki.

Kutokana na hali hiyo amesema kwa sasa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), inaendelea kutekeleza wajibu wake wa maandalizi ya uchaguzi huo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha pale itakapotangazwa rasmi.

Akizungumza katika maadhimisho ya sherehe za Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanazibar, Dk Shein alisema tume hiyo inaendelea na maandalizi hayo ya uchaguzi mkuu katika tarehe itakayotangazwa hapo baadaye, hivyo alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi waende kujiandikisha ili siku itakapofika waweze kuchagua viongozi watakaowataka.

Hata hivyo, Dk Shein ambaye hii ni mara yake ya mwisho kushiriki sherehe hizo za Mapinduzi akiwa kiongozi wa nchi, aliwaonya wale wote wanaotaka kuvuruga amani na usalama wa Zanzibar akiwaeleza kuwa Serikali inaendelea vyema na jukumu lake la ulinzi wa watu na mali zao.

“Niwakumbushe tu kuwa tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kisheria na kikatiba, kwa kulinda amani na usalama wa watu na mali zao na hatutachelea kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayejaribu kuhatarisha amani ya nchi yetu,” alisema.

Alisema ni wazi kuwa hakuna mbadala wa amani katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja jamii na taifa kwa ujumla, hivyo uvunjaji wa amani huanza kwa vitendo visivyozingatia sheria za nchi, kwa hiyo wananchi wajiepushe na vitendo hivyo.

Alitoa wito kwa kila mwananchi kuzingatia suala la amani na usalama kuwa ni suala la lazima na la msingi.

Dk Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuendelea kutunza Muungano kwa dhamira ile ile ya waasisi wa Muungano huo, ambao ni hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume, pamoja na viongozi wa Serikali za awamu zilizotangulia ili nchi iendelee kupiga hatua kubwa zaidi na kuwa ya amani na utulivu.

Dk Shein alisema miongoni mwa mambo ya kujivunia katika Serikali yake ni kupitishwa kwa mabadiliko ya Sheria ya Utumishi wa Umma mwaka 2011 na marekebisho ya mishahara yaliyofanyika kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2017 kwa ajili ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma.

MISHAHARA

Alisema ana matumaini makubwa kuwa kutokana na hali nzuri ya makusanyo ataweza hata kuongeza mishahara ya wafanyakazi kama sehemu ya jitihada ya kuimarisha masilahi ya watumishi wa umma.

Alisema ongezeko la mishahara ambalo limefanyika tangu kupitishwa kwa mabadiliko hayo limeongeza matumizi ya Serikali kwa zaidi ya mara 5.1 kutokana na kuongezea mishahara na kuongezeka pia kwa pensheni kwa watumishi wa umma.

Alisema kutokana na maboresho hayo ya maslahi matumizi ya mishahara yalitoka Sh bilioni 83.1 mwaka 2011 hadi kufikia Sh bilioni 417.9 mwaka 2019 sawa na ongezeko la mara 5.1, hata hivyo kasi ya ukuaji wa uchumi imewezesha kulipa maslahi yote kwa kipindi chote hicho.

Alisema mafanikio yaliyopatikana katika sekta zote za maendeleo ndani ya miaka 56 ya mapinduzi ni kutokana na kuednelea kuwepo kwa sababu za msingi za kufanyika mapinduzi hayo ya kuondoa ubaguzi na dhuluma na kujenga amani na umoja.

KAULI YA JUZI

Juzi wakati akipokea matembezi ya ‘amsha amsha’ yaliyowashirikisha makanda na wapiganaji wa vikosi vya ulinzi na usalama katika Viwanja vya Mnazi Mmoja mjini Unguja, Dk. Shein,  alisema kila mwananchi ana jukumu la kudumisha amani iliopo nchini pamoja na kulinda na kuyaenzi kikamilifu Mapinduzi  ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Alisema hatua ya wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama ya kuanzisha  aina hiyo ya matembezi, inafaa kupongezwa kwani inafanikisha dhamira ya kuwajengea ari wapinaji pamoja na kuwajengea matumaini wananchi ya kuendelea kuiamini Serikali yao.

Alisema dhana ya kudumisha usalama wa nchi inatokana na Sera ya chama cha Afro Shirazi Party (ASP) iliyowekwa baada ya Mapinduzi ya 1964, na kusema dhana hiyo ni endelevu na haitokuwa na mbadala.

Dk. Shein alisema baada ya Mapinduzi ya 1964, Zanzibar ilianzisha Jeshi la Ukombozi (JLU) na baada ya Muungano wa Tanzania, Jeshi la wananchi wa Tanzania liliundwa, lengo kuu likiwa ni kudumisha ulinzi na usalama  ndani na nje ya mipaka yake.

Rais Dk. Shein alikemea tabia ya baadhi ya watu ya kujifanya wababe na kuidharau Serikali  na kusema kila jambo lina mipaka yake, akibainisha usawa uliopo kwa kila mwananchi mbele ya sheria.

Alisema Serikali zote mbili za SMT na SMZ zinaendeshwa kwa misingi ya sheria, chini ya usimamizi wa vyombo vilivyowekwa ambavyo hufanyakazi kwa misingi ya katiba na sheria.

Aliwataka wale wote waliojiandaa kufanya vituko kwa kisingizo cha uchaguzi mkuu mwaka huu kuacha mara moja na kubainisha kuwa Zanzibar ni nchi ya Mapinduzi iliopinduliwa ili wananchi waweze kuishi kwa amani na usalama.

Alisema siasa isiwe sababu ya watu kufanya fujo na kusema uchaguzi unaendeshwa kwa misingi ya sheria, akibainisha azma ya Serikali ya kuwashughulikiya wale wote watakaojihusisha na uvunjifu wa amani.

Alieleza kuwa vyombo vya ulinzi viko makini na vinajuwa wajibu wao na kufafanua kuwa hakutakuwepo na mtu atakaeonewa katika ushughulikiaji wa jambo hilo.

CHANGAMOTO

Rais huyo wa Awamu ya Saba wa Zanzibar, alisema katika kipindi chake cha mika tisa madarakani, miongoni mwa changamoto katika sekta ya afya ni suala la hospitali nyingi kubaini kasi ya ongezeko la maradhi yasiyo ya kuambukiza kama moyo, saratani na kisukari na kwamba anaamaini wataalamu wa afya watafanya tafiti zao kwa bidii ili serikali iendelee kuchukua hatua za haraka na salama kupunguza kasi ya ongezeko la maradhi hayo.

Hata hivyo, Dk Shein aliamua kukatisha kusoma hotuba yake yote kwa kuwahurumia watu waliokwua uwanjani kutokana na jua kali na kwaomba wananchi waridhie aeleze machache na kwa kuwa vitabu vimechapishwa kuhusu hotuba hiyo watasoma kwa wakati wao.

“Saa zimekwenda, jua limekuwa kali sana ninafahamu mtihani wanaopata watoto na vijana wetu na watu wengine katika uwanja huu, ningetamani nisome hotuba yangu yote lakini lazima tuwahurumie wale wanaotaabika na jua, jua jingi lina madhara sana,” alisema kihs akuhitimisha hotuba yame muda mchache baadaye.

Alisema katika miaka tisa ya Serikali ya Awamu ya Saba ya Zanzinbar katika miaka tisa cha iliyopita ya uongoziw ake, Dk Shein alisema imefanya juhudi za maendeleo katika maeneo mbalimbali.

Alisema Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imeweza kuvutia wawekezaji kwenye miradi 304 mtaji wa dola bilioni 3.74 imetekelezwa na kuzalisha ajira 16,866 katika miaka tisa iliyopita.

Alisema sekta ya elimu imeimarishwa na kutoa elimu bure bila ubaguzi kama uilivyitangazwa na Karume, serikali imeongeza skuli, taasisi za elimu na wanafunzi katika ngazi zote kuanza skuli za maandalizi hadi vyuo vikuu, kadhalika sekta ya afya, maji na huduma nyingine za jamii.

VIONGOZI WALIOHUDHURIA

Katika sherehe hizo, viongozi mbalimbali wakiwamo wastaafu walihudhuria sherehe hizo akiwamo, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli wote walihudhuria sherehe hizo.

Pamoja nao, alikuwepo pia Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume na waliokuwa viongozi katika Serikali yake, akiwemo Shamsi Vuai Nahodha, ambaye alikuwa Waziri Kiongozi.

Kwa mara ya kwanza tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Rais Dk. Shein, mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye nao walihudhuria sherehe hizo.

MAONYESSHO

Katika sherehe hizo, maonyesho ya makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yalitia fora, kutokana na makomandoo hao kuonyesha ujuzi ambao haikuwahi kuonyeshwa awali.

Makomandoo hao waliduwaza washiriki katika sherehe hizo kwa kuonyesha mbinu mbalimbali ikiwemo kuvunja vigae kifuani, kuvunja vigae chini ya mkono kwa kutumia nyumndo, kuvunja vigae mkononi kwa kutumia nyumdo na shoka, mateka kuvutwa na gari na kisha kuhitimisha onyesho hilo.

Awali, makomandoo hao walifanya onyesho la kutoa heshima kwa kupita wakiwa wamebebba mabegi yenye uzito wa kilogramu 30 za vifaa vuinavyowasaidia wakiwa kazini, kutoka kwa kikundi maalumu cha JWTZ.

Katika maonyesho ya vikundi mbalimbali katika kuenzi Mapinduzi ya Zanzibar, JWTZ pia ilionyesha namna ya kulinda viongozi wao na askari anavyoweza kumiliki silaha.

Askari polisi waliingia na onyesho la askari wa zamani, askari tarabushi, kuonyesha kwata maalumu iliyochezwa kabla ya mapinduzi ya Zanzibara mwaka 1964.

Kwata hiyo iliitwa tarabushi kutokana na na kofia waliyokuwa wakivaa, ambayo iliitwa ‘taabushi’ kwa kiarabu lakini wazanzibar wakazi walishindwa kuitamka hivyo na kuiita tarabushi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here