28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

MIAKA 53 YA MUUNGANO, KERO ZAKE BADO HAZIJATATULIWA

Na Salim Said Salim


NI miaka 53 sasa tangu Tanganyika na Zanzibar kuungana na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano wa nchi hizi mbili; moja kubwa na nyingine ndogo, umepitia mitikisiko mingi, lakini si kwa kuwa wamoja, bali juu ya mfumo.

Mara nyingi pamesikika malalamiko Bara na visiwani, lakini mwisho wa siku Watanzania wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuuenzi Muungano na watu wake kuendelea kuwa kitu kimoja, huku wakitafuta ufumbuzi wa kero zilizopo.

Hata viongozi wa juu wa pande zote mbili  wamesikika mara nyingi kukerwa na namna baadhi ya shughuli za Muungano zinavyotekelezwa. Hali hii ilisababisha Rais Julius Nyerere kusema Muungano wa Serikali mbili ni wa hiari na hakuna kulazimishana.

Rais Karume alitoa kauli zinazonukuliwa mara kwa mara kuonyesha hakuwa tayari kuwa na Muungano usiokuwa na masilahi na Zanzibar. Moja ya nukuu yake maarufu ni ile aliyosema; “Muungano ni kama koti ambalo ukiona limechoka na halitiliki viraka unalivua na ukipenda unanua au kushona jingine kwa mtindo tofauti.”

Kelele za kutaka Muungano ukarabatiwe kwanza zilisikika visiwani na baadaye palizuka zogo Bara, baada ya Wabunge 55 waliojulikana kama G55 waliotaka ifufuliwe Jamhuri ya Tanganyika.

Wengi wa wabunge wa kundi lile walipoteza nyadhifa zao serikalini na wengine kupikiwa jungu la kuwa si raia wa nchi hii. Huko ndiko tulikotoka. Malalamiko yaliyosikika visiwani ni pamoja na madai ya wenzao wa upande wa pili wa Muungano kufaidika zaidi.

Lakini liliowakera zaidi Wazanzibari ni zile kauli za kusema Zanzibar ni sawa ni wilaya ndogo tu ya Bara na kutoichukulia kama nchi. Wazanzibari pia wamekuwa wakilalamika kuwa wamekuwa wakikataliwa kujiamulia mambo wanayoyaona yana masilahi na Zanzibar. Lakini kwa upande wa pili wa sarafu, wapo watu kutoka Bara waliosema Zanzibar inadekezwa na inafaidika zaidi katika Muungano.

Madai mengine ni kuwa Wazanzibari wamejazana katika Bunge la Muungano na wanajadili mambo ya Bara wakati wabunge wa Bara wamefungiwa milango kuingia Baraza la Wawakilishi na kujadili mambo ya Zanzibar.

Wapo pia waliohoji ni kwanini Rais wa pili mstaafu wa visiwani, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, alipoondolewa madarakani mwaka 1985  kwa kutaka mabadiliko ya kuwa na Muungano wa Serikali tatu, hapakutakiwa kura ya maoni ya Wazanzibari? Tetesi zilisikika ni kwamba Jumbe angefukuzwa na Wazanzibari katika kikao ambacho kingefanyika visiwani na si katika kikao kilichofanyika Dodoma na wengi wa walioshiriki kuamua hivyo wakiwa watu wa Bara.

Muungano ulipoundwa, Rais wa Zanzibar alikuwa moja kwa moja Makamu wa Kwanza wa Rais na kama rais angelitoka visiwani, mwenzake wa Bara angekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais. Hili limeondolewa bila ya kura ya maoni na lililamikiwa na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour.

Baada ya kila muda mfupi, Watanzania wamekuwa wakiambiwa Serikali iko mbioni kumaliza  kero za Muungano, lakini hakuna anayeelewa hizo mbio ni za masafa mafupi, kati au marefu, zilianzia wapi, zilipo na wapi mwisho wake.

Hata hivyo, Kikwete aliweza angalau kumaliza moja ya kero iliyokuwa inapigiwa kelele nyingi  na Zanzibar. Nayo ni kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa na mamlaka kamili juu ya mafuta yaliyopo katika ardhi na bahari ya visiwa vya Unguja na Pemba, Muungano ulikuja ghafla, kama kimbunga bila ya hodi.

Wakati ulipoasisiwa na marais wa nchi hizi mbili, Mwalimu Nyerere (Tanganyika) na Sheikh Karume (Zanzib), nilikuwa nina miaka 18 na nilikuwa katika matayarisho ya kwenda Czechoslovakia (sasa Jamhuri ya Czech) kwa masomo ya uandishi wa habari, kazi niliyoianza nikiwa shule (Zanzibar tunaita skuli).

Siku ile ya Aprili 26, mwaka 1964, Mwalimu na Karume walipotia saini mkataba wa kunganisha nchi hizi mbili, nilikuwa nimekaa katika kijiwe kimoja cha mtaa wa Barastekipande mjini Unguja.

Wakati ule jua lilikuwa linamalizia safari yake ya kila siku ya kutoka mashariki kwenda magharibi ndipo alikuja mwalimu mmoja wa shule, Mohammed Shatry na kueleza kuwa Zanzibar na Tanganyika zimeungana.

Wazee na vijana waliacha mazungumzo waliokuwa na michezo ya bao, dhumna na karata na kuanza kuzungumzia huo uamuzi wa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar.

Bwana  mmoja aliyeshiriki Vita Kuu vya Pili ya Dunia (1938-45)  na kuwa miongoni mwa wajenzi wa daraja la Mto  Kwai (angalia filamu ya Bridge over the River Kwai) kule Mynamar, wakati ule ikiitwa Burma, mzee Maulidi (aliyejulikana kwa jina la Kade Vondik) alisema: “Tumekwisha.”

Siku iliyofuata watu wengi walikaa majumbani na kwenye vijiwe kusikiliza redio na kusoma magazeti kujua habari za Muungano. Hapakuwa na sherehe  kuadhimisha kuungana kwa nchi hizi mbili.

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa, alikiri mara nyingi kuwa makubaliano ya Muungano yalifanyika kwa siri. Msekwa aliyekuwa katibu wa Bunge  la Muungano ulipoasisiwa, alisema hatua ya kuziunganisha nchi hizi mbili ilichukuliwa  haraka kwa kile alichokieleza kama upepo wa kisiasa, usalama na woga wa waasisi wake,  Mwalimu na Karume.

Kwa wakati ule hakuna aliyethubutu kuuliza  kwa vile kuikosoa Serikali ilikuwa ni usaliti, lakini siku hizi lugha imelainishwa na anayelaumu huitwa ‘si mwenzetu’ au ‘haitakii mema Tanzania’.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Wolfango Dourado ambaye aliwekwa kizuizini na Mwalimu na mawaziri wa Serikali ya Rais Karume, walieleleza mara nyingi kuwa hawakushauriwa. Siku chache baada ya kuundwa muungano  palifanyika mkutano mjini Unguja.

Askari wenye silaha walikuwepo kila pembe, mzee Karume alipowauliza watu kama walifurahia  kuungana na kutakiwa waseme ndiyo au ha siyo, Umma uliojaa hofu uliitikia ‘ndiyo’. Hapa inafaa kujiuliza kama ridhaa ya wananchi ilihitajika kwanini hiyo ridhaa haikutafutwa kupitia kura ya maoni kabla ya nchi hizi kuungana?

Zipo kauli tofauti za nani kati ya Mwalimu na Karume alitoa ushauri wa nchi hizi kuungana na hili limebakia siri ambayo waasisi hawa wamekufa nayo.

Muungano ulipoundwa ulikuwa na sura ya kisiasa na ulibeba maeneo 11, ikiwa pamoja na mambo ya ndani na nje. Fedha, biashara, kilimo, elimu, afya, mafuta na mawasiliano hayakuwemo katika orodha hiyo.

Ushirikiano wa kimataifa pia haukuwa katika aorodha hiyo na ndiyo maana Zanzibar chini ya utawala wa Rais mstaafu, Salmin Amour, ilijiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC). Uamuzi huu ulizusha  zogo ambalo hatimaye lililazimisha Zanzibar kujitoa baada ya kuahidiwa kwamba Tanzania ingejiunga na jumuiya hiyo, lakini sasa ni miaka zaidi ya 20 na OIC suala la  Tanzania kujiunga na OIC halizungumzwi.

Wapo wanasiasa wa visiwani wanaosema  kuingizwa ushirikiano wa kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje kulilenga kuibana Zanzibar isinufaike na misaada kutoka katika OIC. Mara nyingi mawaziri wa  zamani wa Serikali ya  Zanzibar, wakiwamo walionisomesha shule  na kuuawa katika mazingira ambayo ukweli wake haueleweki, waliniambia walishtukizwa tu na kuundwa kwa Muungano.

Walioufurahia uamuzi wa kuziunganisha nchi hizi mbili walitarajia kumalizika mauaji ya watu yaliyokuwa yakifanyika visiwani. Mauaji haya ni pamoja na yale yaliyofanyika msikitini wakati watu wakifanya ibada.

Waliofanya hayo walipewa majina kama ya ‘mamba’ ‘Sancho’ na ‘Dracula’. Muungano huu uliopitia dhoruba nyingi na bado unaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi.

Kwa Watanzania wengi, Bara na visiwani, inaonekana Muungano si tatizo. Kinacholeta mivutano ni mambo gani ni ya Muungano na yepi yapo chini ya mamlaka ya Serikali ya Zanzibar.

Wapo wanaotaka muundo wa Serikali mbili uendelee, lakini wapo wanaosema uwe wa Serikali moja. Tume ya Katiba iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, kutokana na maoni iliyokusanya kwa wananchi na viongozi mbalimbali, ilipendekeza mfumo wa Serikali tatu.

Vile vile pamesikika kile kilichoitwa muungano ambao utaipa Zanzibar mamlaka kamili. Kinachoshangaza watu wengi ni kusikia viongozi wa  CCM  na wa Serikali wakisema wanapenda wananchi washirikishwe kutoa maoni yao juu ya Muungano wakisema lolote lile la kuubadili mfumo wa sasa wa Serikali mbili haliwezekani.

Muungano ulipoundwa ulikuwa na mambo 11, lakini sasa wapo wanaosema ni 29 na wengine wamedai kuwa yamefikia 50. Vile vile kumekuwa na utata juu ya kuongezeka kwa mambo ya Muungano na wapo viongozi wa Zanzibar, wakiwemo wanasheria  wa Serikali, waliosema kuwa mambo mengi yameongezwa kinyemela au kutumia mizengwe kupitia katika Bunge ambapo watu wa Bara ndio wengi.

Nchi kubwa na ndogo zikiungana mdogo ndiye anayelalamika sana, baadhi ya wakati bila ya sababu za msingi. Katika kila upande wa Muungano wapo watu wanaodai  wenzao wa upande wa pili ndiyo wanaofaidika zaidi.

Tangu Muungano kuundwa, tumeshuhudia  wanasiasa wengi walipokuwa serikalini walikuwa watetezi wakubwa wa muungano wa serikali mbili, lakini walipotoka au kufukuzwa wakawa ndio wakosoaji wakubwa wa mfumo huu.

Kila siku tunaambiwa Serikali zote mbili zipo mbioni kutatua kero za Muungano, lakini matunda ya tume, kamati na mikutano ya kuzungumzia suala hili hatuyaoni.

Muungano pia umekuwa ukitumiwa kama karata ya mwisho na baadhi ya viongozi na wanasiasa  wa Zanzibar kulazimisha mambo waliyoyaona yanawanufaisha kisiasa.

Kila agenda zao zikikwama utasikia wana tisho kuwa tayari kuuvunja Muungano. Kwa vyovyote vile, ni vizuri maoni yaliyotolewa na wananchi katika tume mbalimbali na ile ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, yakaheshimiwa na si kuendelea kutoa maelezo ya kuwa suala hili linaendelea kushughulikiwa kwa masilahi ya Taifa na watu wake.

Muungano wetu ni mfano mzuri wa maelewano kwa watu wa Bara la Afrika, lakini chini kwa chini kunafoka moto ambao unahitaji kuzimwa haraka ili usije kuripuka na kubaki kulaumiana.

Matatizo ya Muungano yanapaswa kumalizwa kwa kuchukuliwa hatua zitakazowaridhisha wananchi wa pande zote mbili na si propaganda za kisiasa zisizojaza kikombe wala kikapu.

Tukiwa tumetimiza miaka 53 ya Muungano, tuache kujifunika chandarua cha unafiki au kukinga mvua  kwa mikono ili tusirowe na tuchukue hatua madhubuti za kutatua matatizo yaliyopo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles