30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

MIAKA 22 YA SOPHIA SIMBA KATIKA SIASA

Aziza Masoud, Dar es Salaam


SOPHIA Simba ni miongoni mwa wanawake maarufu nchini katika ulingo wa siasa.

Ni wanawake shupavu mwenye uwezo wa kujipambanua na kusimamia misimamo yake anayoiamini.

Mwanasiasa huyo ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM(UWT) nafasi inayompa fursa ya kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano  .

Sophia Simba amezaliwa Julai 1950, kitaaluma ni mwanasheria.

Kisiasa amepata kuwa na umaarufu wa kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) hususani katika ushawishi. Ni mmoja kati ya wanawake waliokitumikia chama hicho kwa muda mrefu, amekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa miaka 22 sasa.

Katika nafasi za kiserikali amepata kuwa   Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto katika serikali ya awamu ya nne, chini ya utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.

Ushawishi mkubwa ndani ya CCM ndio umemwezesha mwanamama huyo kuwa  Mjumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya CCM na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho tawala.

Sofia Simba amewahi kufanya kazi katika Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), ambapo pia  alikuwa Katibu wa Wanawake wa CCM (UWT)  kuanzia mwaka 1973 hadi 1979.

Aidha, mwanasiasa huyo alikuwa diwani wa Kata ya Upanga Magharibi Wilaya ya  Ilala na baadaye 1995 alishinda ubunge wa Viti Maalumu kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mwishoni mwa wiki hii ya kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, mbali ya kutoa ujumbe kwa wanawake na kuwataka kufanya kazi kwa bidii,  alitumia fursa hiyo kutangaza rasmi kutogombea tena nafasi ya uenyekiti wa UWT baada ya kuitumikia jumuiya hiyo kwa miaka kumi.

 

Akizungumza na hadhara ya wanawake wa UWT Sophia anasema wanawake wanapaswa kujituma kwa midi na kutokata tamaa.

“Tunapaswa kutambua kuwa maisha ya mwanamke ni mapambano, mwanamke akijishughulisha ana nafasi kubwa ya kuinua familia, wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi,”anasema Sophia.

Anaongeza kwa kutumia kaulimbiu ya mwaka huu ‘Tanzania ya viwanda wanawake ni msingi wa mabadiliko ya uchumi’  kuna kila haja ya wanawake kuwahamasisha watoto kwenda katika vyuo vya ufundi kujifunza.

“Kuna watoto hawana kazi, wakiwezeshwa wakaanzisha viwanda naamini tutafika mbali, wanawake tubadilike na sisi ndiyo msingi wa mabadiliko, tusikate tamaa,”anasema Sophia.

Anasema wazazi  wanatakiwa kuwa waangalifu kwa watoto kwa sababu wengi wao wanaharibika kwa kukosa uangalizi.

“Tujiwekee muda wa kuwaangalia watoto wengi wanaharibika kwa sababu ya kukosa muda, tujitahidi kuwa karibu na watoto wetu tusikubali watoto wetu wafundishwe na televisheni na mitandao ya kijamii,”anasema Sophia.

Akizungumzia kuhusu kutogombea nafasi ya Uenyekiti wa UWT katika uchaguzi wa chama unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, Sophia anasema  tangu alipofanikiwa kupata nafasi hiyo mwaka 2007  nia yake ilikuwa kuitumikia jumuiya hiyo kwa  vipindi viwili tu na si zaidi ya hapo.

 “Napenda kutumia fursa hii adhimu kuwatangazia wana UWT  na wanawake wengine ambao ni wana CCM kwamba, mimi Sophia Simba kwa hiari yangu mwenyewe nimeamua kutogombea nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa UWT katika uchaguzi ujao.

“Nitaachia kiti baadaye mwaka huu, baada ya kuitumikia jumuiya kwa mapenzi, utii, uaminifu na uadilifu mkubwa kwa kipindi cha kutosha, naona sasa ipo haja ya mimi kupumzika na kuwaachia wanawake wenzangu waendeleze pale ninapoachia, nitakabidhi kijiti hiki kwa uongozi utakaochaguliwa.

“Nimeamua niwatangazie mapema ili kuwaweka huru na kuwapa muda wa kujipanga vizuri wale wote wanaokusudia kugombea nafasi hii kubwa ndani ya Jumuiya yetu ,pia kutoa majibu kwa waliokuwa wakiniuliza na kunihamasisha nigombee,tusiogopane nafasi zipo wazi hakuna nafasi ya mtu,`”anasema Sophia.

 

Anasisitiza  kuwa anaamini wapo wanawake wanaoweza kuwaunganisha wanajumuiya hiyo katika kupigania  haki zao za msingi,haki za ustawi wa watoto  na masuala ya jamii kwa ujumla likiwemo jukumu kubwa la kisiasa.

 

Kipindi kigumu ndani ya siasa

Ushupavu wa Sophia Simba ulithibitika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 pale alipothibitisha wazi kuwa yupo upande wa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.

Alitoa uamuzi huo mgumu wakati ambapo ndani ya CCM kulikuwa na vita kali ya kisiasa iliyosababisha wa mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho kikongwe.

Sophia Simba hakukubaliana na kukatwa kwa jina la Lowassa wakati wa mchakato wa kura za kumpata mgombea urais kupitia CCM.

Mwanasiasa huyo anaeleza kuwa katika safari yake ya kisiasa wakati mgumu aliupata kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka juzi .

Katika msimamo huo Sophia alikuwa na Adam Kimbisa na Dk. Emmanuel Nchimbi, wote kwa pamoja walionyesha msimamo ho hadharani dhidi ya hatua  ya Kamati Kuu ya CCM kukata jina la  Lowassa ambaye  alikuwa mmoja wa wagombea wa urais katika kura za  maoni.

“Katika kipindi cha kura za maoni nilikuwa naamini kuwa kulikuwa na mtu anafaa kuwa mgombea urais, lakini ule ulikuwa ni mtazamo wangu wa kidemokrasia nilikuwa na kipindi kigumu,”anasema Sophia.

Anasema pamoja na kuwa na msimamo huo baada ya mchujo kufanyika na kupatikana mgombea wa urais alibadili mawazo na kumuunga mkono Rais  Dk. John Maguli na kuwashawishi wanawake kumpigia kura.

Anasema bado anaamini katika Uhuru wa kidemokrasia ndani ya chama unaokwenda sambamba na kuheshimu mawazo ya wanachama husika. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles