Miaka 19 bila Mwalimu tumegeuka Taifa la bahati nasibu

0
1517

OKTOBA 14, 1999 ilikuwa ni siku ya majonzi kwa Taifa letu baada ya kumpoteza kiongozi na mwasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na mpaka kufika Jumamosi ya Oktoba 14, mwaka huu tutakuwa tunatimiza miaka 19 bila ya uwepo wa mwalimu.

Watapita viongozi wengi lakini cheo cha Baba wa Taifa bado mmiliki wake atabaki kuwa Mwalimu Nyerere.

Sote tunafahamu kuwa Mwalimu alikuwa ni kiongozi mwenyen falsafa na imani zake alizoamini kuwa zinaweza kulisaidia taifa ili kupiga hatua na moja ya imani yake kubwa ilikuwa ni kwenye falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea, Mwalimu aliamini ili taifa liwe huru basi lazima litengeneze mifumo yake ya kujitegemea kwenye nyanja zote ikiwamo, siasa, kijamii, kiuchumi na hata kiutamaduni.

Imepita miaka mingi tangu yeye aachie madaraka lakini suala la kujitegemea bado limeendelea kuwa mtihani mgumu kwa taifa hili hali ambayo kama nikiulizwa tumewezaje kumuenzi Mwalimu bila kupepesa macho wala maneno nitajibu ya kuwa tumeshindwa kumuenzi kwa sababu mpaka leo bado sisi ni taifa tegemezi kwenye nyanja nyingi.

Wapo watakaosema kuwa nyakati zimeenda na kila kiongozi ana maono juu ya utawala wake lakini bado imani ya taifa letu kama tusemavyo kwenye Katiba yetu kuwa Taifa letu ni taifa linalofuata misingi ya Ujamaa na Kujitegemea.

Kila zama zina ufalme wake na zama hizi ni zama za John Pombe Magufuli, kama nitaulizwa swali kuwa niwafananishe viongozi hawa wawili basi sehemu ninayoona wanafanana ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kufanya kazi, lakini pamoja na kufanana huko bado kuna daraja kubwa kati yao nalo ni hili zamani kazi zilihamasishwa na mazingira ya kufanya kazi wakati kwa sasa hivi tumegeuka kuwa taifa la bahati nasibu.

Ukifungulia luninga lazima ukutane na matangazo yanayohamasisha wananchi kucheza michezo ya bahati nasibu, ukifungulia redio huko ndio utakereka na hata ukisema usome magazeti huwezi kuepuka kukutana na matangazo ya bahati nasibu hapo sijazungumzia vijana ambao hujikusanya kwa wingi kwenye zile ofisi za michezo ya kubashiri.

Unaweza kusema labda ni mambo ya kibiashara ambayo hayana uhalisia wowote lakini kwa utafiti wangu mdogo nilioufanya kati ya watu watano wa familia moja basi watu watatu wanajihusisha au wameshawahi kujihusisha na michezo ya bahati nasibu hii maana yake nini? Ama inatoa tafsiri gani? Tafsiri inayokuja hapo ni kuwa sasa tumekuwa taifa la kutegemea bahati nasibu na wananchi hawana uhakika na maisha yao sasa hili ndio taifa aliloliasisi Mwalimu?

Mbaya zaidi michezo hii imemkumba kila mwananchi bila kujali hadhi, wadhifa, jinsia wala rika maana hapo zamani ilionekana kama ni mchezo wa vijana wasiokuwa na ajira rasmi ndio wanaojihusisha na michezo ya kubashiri lakini hivi sasa hilo halijalishi kama mtu ni msomi ama la, mtu mzima ama kijana wote wamo si kinamama wala kinababa wote wamo sasa hii ina maana gani kwa taifa? Kwangu mimi kuna vitu vitatu nimeviona

Moja kumekuwa na ukosefu wa ajira, pili hata kwa walioajiriwa vipato vimekuwa havitoshelezi, tatu tumekuwa taifa lisilo na misingi. Siwezi kukataa kuwa suala la kushamiri kwa michezo ya kubashiri ni la ulimwengu mzima lakini kwa nchi za kiafrika hasa nchini ugonjwa huu unaenda kuwa mkubwa sana kwa sababu sioni dalili zozote za utatuzi wa hayo mambo matatu niliyoelezea hapo juu.

Siku moja nikiwa na mzee mmoja aliwahi kuniambia unaona wale vijana waliojikusanya pale na peni na makaratasi ingekuwa zama za Mwalimu ungeshaona karandinga likija kuwasomba waende mashamba ya ujamaa wakazalishe lakini leo hii tuunapoteza nguvu kazi ya vijana lakini hata ukiwaambia wasibeti waache, unayo shughuli ya kuwapa wafanye?

Mwisho wa siku unawaacha na hivyo ndivyo hali halisi ilivyo lakini ukiachana na hilo bado ukosefu wa miiko ama misingi ya taifa unatufanya leo tumekuwa taifa la bahati nasibu na wala sitashangaa siku tukihamia kwenye vitu vinavyoonekana ni vya ovyo kuliko hili, leo tunawashangaa mateja lakini tunakumbushana tu kuwa suala la madawa nalo lilianza hivi hivi kama mzaha.

Mwalimu hakutamani kutengeneza taifa ambalo wananchi wake wanategemea bahati nasibu ili kuishi, taifa la kutengeneza wasomi ambao hatuwezi kuwaajiri na tunaowaajiri tunawalipa kiasi ambacho hakikidhi mahitaji, wapo watakaodhani kuwa labda shutuma hizi nazishusha kwa Serikali ya Awamu ya Tano la hasha! Haya ni matokeo ya ukosefu wetu sote kama taifa na yanayotokea sasa ni matokeo tu hivyo ni lazima kushughulikia hizo changamoto vinginevyo haya mambo tunayoyaleta tutakuja kuzinduka yakitufanya tukiwa maskini maradufu.

Najua ni biashara za watu na zimeajiri wengi lakini huu ndio ukweli, ulale pema Mwalimu lakini hapo ndipo tulipo kama taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here