31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA 15 WIZARA YA NISHATI NA MADINI HAINA WAZIRI ALIYEDUMU

 

 

NA MARKUS MPANGALA,

KUTEULIWA kuwa Waziri wa Nishati na Madini hapa nchini ni sawa na kutupwa ndani ya tanuri ili uteketezwe kwa moto. Utaruka vihunzi vya kila namna. Utanyeshewa na mvua, utapigwa na radi au jua, utakimbia huku na huko ukinyoosha mkono na kutamba wewe ni waziri safi na huna makando kando yoyote ya kukunasa. Lakini dude au jinamizi la wizara ya nishati madini likitikisika kidogo, unayumba, unapepesuka, umeloweshwa, jasho linakutoka haswa na mwishowe unatupwa kando kama kitu kisicho na thamani.

Hayo yametokea Mei 24, mwaka huu baada ya Rais John Magufuli kumfukuza kazi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, mara baada ya kupokea ripoti ya Kamati maalumu ya uchunguzi wa mchanga wa madini (Makinikia) kwenye mkontena 277 yaliyokuwa yakisafirisha mchanga kwenda nje ya nchi (hususani Japan) kwa ajili ya kuyeyushwa, ili kupata kiwango cha madini aina ya dhahabu au shaba. Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa rais na Mwenyekiti wake Profesa Abdulkarim Mruma.  

Aidha, Rais Magufuli amevunja Bodi ya Wakala wa Madini nchini (TMAA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo kutokana na ripoti hiyo ya kamati maalumu.

Kufukuzwa kazi Profesa Muhongo kumedhihirisha kuwa Wizara ya Nishati na Madini ni kitimoto tangu Awamu ya Kwanza ya Rais Julius Nyerere. Kwa mujibu wa kitabu cha ‘Uongozi na Utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere’ kilichoandikwa na Pius Msekwa katika ukurasa wake wa 121, anasema Baraza la Mawaziri la kwanza la Serikali ya CCM , Waziri wa Nishati na Madini Awamu ya Kwanza, ambayo iliitwa ‘Wizara ya Maji, Umeme na Madini’, waziri wake alikuwa Anoor Kassum. Katika awamu hiyo, Rais Nyerere alimpiga marufuku waziri Kassum kuipatia tenda kampuni yoyote ya uchimbaji wa madini hadi pale nchi itakapokuwa tayari. Utawala wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi haukujishughulisha kabisa na uchimbaji wa madini hadi ulipomaliza muda wake.

KUKAANGWA MAWAZIRI

Wizara ya Nishati na Madini kihistoria imekuwa na mitikisiko mingi ambayo imesababisha wengi wao kuondolewa madarakani kutokana na kuzingirwa na kashfa walizohusika moja kwa moja au watendaji wengine waliopo chini yao.

Aidha, taarifa zinasema kuwa wizara hii wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Nyerere, alikuwepo Waziri wa Nishati na Madini, Alnoor Kassum ambaye aliambiwa ni marufuku kuchimba madini katika migodi yote.

Awamu ya Pili ya uongozi wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Waziri wake wa Nishati na Madini alihangaika sana na uagizaji wa mafuta ili uchumi ukae sawa, lakini hakuweza kugusa sekta ya madini. Lakini kuingia madarakani kwa Rais Benjamini Mkapa mwaka 1995, akamfungulia waziri wake wa nishati na madini 'neema' kuruhusu wawekezaji kuchimba madini.

Wachambuzi wa masuala ya uongozi, uchumi na biashara wanasema wizara ya nishati na madini ni kama vile ‘imelaaniwa’. Tangu kuingia madarakani Rais Jakaya Kikwete  mwaka 2005, ukimuondoa George Simbachawene, mawaziri waliokuwapo pale hawajawahi kumaliza salama. Licha ya juhudi mbalimbali za Kikwete kutaka kuisafisha na kuunda tume maalumu, lakini bado mawaziri hawakudumu.

Kati ya mwaka 2002 hadi 2006, awamu ya mwisho ya utawala wa rais Mkapa, Waziri wa Nishati na Madini alikuwa Daniel Yona, ambaye aliishia kufungwa jela. Uwaziri wa Yona ulidumu kwa miaka miwili tu.

Mwaka 2006 hadi 2007 chini ya utawala wa Awamu ya Nne, Waziri wa Nishati na Madini alikuwa Ibrahim Msabaha. Huyu aliondolewa kwa kashfa ya Kampuni ya kufua umeme ya Richmond.

Aidha, mwaka 2007 hadi 2008 wizara hiyo ilikuwa chini ya Waziri Nazir Karamagi, naye aliondolewa kwa kashfa ya Richmond. Mwaka 2008 hadi 2012  wizara hiyo ilikuwa chini ya William Ngeleja. Naye aliondolewa baada ya kelele nyingi na malalamiko kwamba ni mmoja wa mawaziri mizigo wasiomsaidia Kikwete.

Mwaka 2012 hadi 2014, wizara hiyo ilikuwa chini ya Profesa Sospeter Muhongo kabla ya kuondolewa nafasi yake kutokana na kashfa ya Akaunti Maalumu ya kuhifadha fedha ya Tegeta Escrow. Muhongo aliteuliwa Awamu ya Pili katika wizara hiyo 2015-2017 alikodumu kwa miaka miwili.

Katika awamu yake ya kwanza wizarani mara baada ya kuondolewa, nafasi yake ilichukuliwa na George Simbachawene. Ni waziri huyu ndiye alimaliza mwaka mmoja salama 2014-2015 kabla ya kuingia kwenye uchaguzi. Ndiyo kusema katika kipindi cha miaka takribani 20 hakuna waziri ambaye aliondoka madarakani bila sakata lolote lililomtikisa.

KIINI CHA MATATIZO WIZARANI

Akiandika kwenye ukurasa wake katika mtandao wa Twitter, Profesa Issa Shivji alisema: “Tulikosa njia tulipopitisha sheria ya madini mwaka 1998 iliyofanya mikataba iwe na nguvu zaidi kuliko sheria. Tukajifungia pingu. Nani wakulaumu?

Maoni ya Profesa Shivji yamebeba kiini cha matatizo ya Wizara ya Nishati na Madini tangu mwaka 1998, ikiwa na maana toka kuingia utawala wa Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa.

Msingi wa matatizo katika wizara ya nishati na madini ni mengi, lakini yapo makubwa mawili; kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow na Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond.

Akizungumzia suala hilo, mmoja wa viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo alisema: “Kadhia ya IPTL ya akina Patrick Rutabazibwa na msingi wa Mkataba wenyewe wa Rais Ali Hassan Mwinyi. Pili, uamuzi wa kibabe wa Rais Benjamin Mkapa, (kama sharti la SAP’s) kutuingiza kwenye uvunaji madini. Sheria ya Madini ya Mwaka 1998 ni tanuri la kuwachomea  mawaziri (maana Watanzania mnaridhika akifukuzwa Waziri kila yakifichuliwa madudu na mnaliwazwa kwa hilo ili msidai sheria husika ifumuliwe.

“Lakini la muhimu ni kwamba masuala ya Richmond na Escrow ni kashfa za Umeme, si rasilimali. Moja ni ufisadi wa kidola, ya pili ni mkakati wa kutumia makosa na kumng’oa Waziri Mkuu madarakani.”

Baada ya maelezo hayo nilimuuliza swali kiongozi huyo: “Kwa maana hiyo tunarudi nyuma hadi mwaka 1995 wa IPTL, kisha mwaka 1998 kwenye mambo ya madini. Na mwaka 2001 uchenjuaji wa mchanga. Nini mustakabali wa Wizara ya Nishati na Madini, pamoja na sekta yenyewe kwa ujumla wake?

Naye alisema; “Mambo ya IPTL ni ubeberu kabisa, kisha Escrow ni wizi wa dola yenyewe dhidi ya wananchi, ni kama ufisadi mwingine uliotokea huko nyuma wa Meremeta na Mwananchi Gold.

“Sheria ya Madini ni mwaka 1998 ndio tulitunga Sheria kwa ushauri wa IMF (Shirika la Fedha duniani) WB (Benki ya dunia). Kuna kitu kinaitwa Structural Adjustment Programs (SAP’s) ndio msingi wa sheria. Tulisamehewa madeni kwa kuruhusu madini yaende na kupewa misaada.

“Uchenjuaji kufanyika nchini ni pendekezo la Kamati ya Bomani (Jaji Mark Bomani) ya mwaka 2008-2009. Zamani mgodi uliohitaji uchenjuaji ni Bulyanhulu tu, baada ya Buzwagi ndio mchanga unaochenjuliwa ukawa mwingi. Hivyo mapendekezo ya Kamati ya Bomani yalisaidia kubadili kidogo sheria ya Madini ya mwaka 1998. Ndio iliongeza mrahaba kutoka asilimia 3 hadi nne ikaweka msingi wa makampuni kulipa Corporate Tax, na pia kuunda TMAA (zamani makinikia yalitoka bila na kuwa na usimamizi wa kueleweka mamlaka ya usimamizi wake).

“Kuna wazo la Capital Gain (ilikuwa ni muswada binafsi wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe mwaka 2012). Bunge liliukataa muswada, Mama Makinda (Spika wa Bunge Annie Makinda) akaupitisha kibabe kuwa sheria. Capital Gain ilisaidia kupatikana kwa mapato yaliyotokana na uuzaji wa hizi kampuni za madini.

Aliongeza kuwa: “Kwa hiyo kwangu mimi kuondoka kwa mawaziri ni ‘danganya toto’ ya kuwatuliza Watanzania msiguse mzizi wenyewe-Sheria ya Madini ya mwaka 1998. Na mawaziri walioondolewa kwa sababu ya mambo hayo ni huyu huyu Profesa Muhongo tu. Wengine Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi waliondoka na Richmond, ambayo ni ya kisiasa zaidi,”

NINI NAFASI YA WANASHERIA WA WIZARA?

Pamoja na mambo mengine, swali linalopaswa kuulizwa hapa ni nini nafasi ya wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali?

Ikumbukwe wizara hiyo imewahi kupata huduma za kisheria kutoka kwa watu wazito kama Naibu Waziri wa Nishati na Madini wa sasa, Dk. Medard Kalemani, William Ngeleja, Dk. Ibrahim Msabaha, Daniel Yona na Edgar Maokola Majogo.

Aidha, kumewahi kuwapo na wanasheria wakuu wa Serikali kama vile Andrew Chenge (1995-2005), Johnson Mwanyika (2005-2009), Jaji Frederick Werema(2009-2014), George Masaju(2015 hadi sasa), ni kwanini sekta ya madini imekuwa na mikataba mibovu ambayo haitoi nguvu kwa mmiliki badala yake imewapa nguvu hizo kampuni za uchimbaji?

Je, wanasheria hawa katika nafasi zao hawakuona matatizo yoyote katika kipindi chote cha uongozi wao katika kadhia hiyo?

Ndiyo kusema kuwaondoa mawaziri kwenye wizara hiyo hakuna maana kuwa kunatatua tatizo la msingi iwapo wataalamu wanaohusika na masuala ya sheria na madini wataendelea kufumbia macho kadhia hii. Ndiyo kusema kuwaadhibu mawaziri wanaotokana na nafasi za kisiasa bado hakutoi jawabu la njia sahihi au suluhisho la kuondokana na kuibiwa kunakofanywa katika sekta ya madini. Kwanini hali hiyo?

Mtaalamu mmoja wa masuala ya uchumi, ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake gazetini alisema, “Nishati na madini inavutia mitaji na uwekezaji mkubwa ambavyo visiporatibiwa vyema ni chanzo cha rushwa. Kumekuwapo mgongano mkubwa wa maslahi baina ya wasimamizi wetu wa sheria na sera, kwa kukubali (kwa namna ya moja ama nyingine) kuhadaiwa ama na maslahi binafsi, au ufahamu mdogo katika majadiliano. Lakini vilevile tusisahau sehemu kubwa ya hii sekta inatolewa macho na Taasisi za kimataifa duniani ambayo daima huwataka kuhakikisha Tanzania inafaidika na taratibu zake. Na kwa kutumia vyombo vyake kama vile WB na IMF  wamekuwa wanaweka masharti ambayo pengine hatuwezi yaona wakati wa kutia saini, lakini athari zake ni kubwa na mbaya kwa taifa,”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles