Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Mhasibu Mkuu wa Klabu ya Simba, Amos Juma amedai aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange (Kaburu) walihamishia Dola za Marekani 300,000 zilizotokana na kumuuza mchezaji Emmanuel Okwi katika Klabu ya Tunisia kwenye akaunti ya Aveva.
Juma amedai hayo leo asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai, shahidi huyo amedai Machi 14,2016 kiliitishwa kikao cha Kamati ya Utendaji cha kawaida kikiwa na ajenda 10 ikiwemo ajenda moja ya fedha zilizoingia kwa mauzo ya mchezaji Okwi ambayo ni ajenda ya Saba.
“Juni 16,2016 nikiwa ofisini kwangu, Kaburu alikuja kuomba nimpe kitabu cha hundi ya akaunti ambayo fedha za Okwi ziliingizwa, nilimpa lakini alipokirudisha karatasi mbili hazikuwepo.
“Alinikabidhi kipande cha karatasi kikionesha kuna Dola za Marekani 300,000 zilihamishiwa katika akaunti ya Aveva, karatasi hiyo ilitoka Benki ya CRDB,” amedai mhasibu huyo.
Katika kesi ya msingi, inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 10 na 16, 2016 Aveva na Kaburu walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya ofisi na kutakatisha fedha.
Mwisho