Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Mhariri wa MTANZANIA Digital, Faraja Masinde, ameibuka mshindi namba moja wa tuzo za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Mwandishi mwingine wa MTANZANIA DIGITAL, aliyepata tuzo hiyo ni Elizabeth Kilindi anayeiwakilisha MTANZANI mkoani Njombe.
Tuzo hizo zilitolewa kwa waandishi 15 wa kampuni tofauti, Ijumaa ya wiki iliyopita katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Nashera, mjini Morogoroni zikihusisha waandishi bora wa habari za watoto kwa mwaka 2019/20.
Akizungumza wakati wa tuzo hizo, Ofisa Mawasiliano wa UNICEF Tanzania, Usia Nkoma Ledama alisema huo umekuwa ni mwendelezo wa kuthamini kazi nzuri za waandishi wa Habari ambazo zimekuwa zikileta mrejesho chanya.
“Huu umekuwa ni mwendelezo wa kuwatambua waandishi wanaofanya vizuri katika kuripoti habari za watoto, tuzo hizi zilianza kutolewa mwaka 2018 lakini hapo katikati zilisimama kutokana na changamoto za corona, hivyo tunawahimiza wanahabari kuendelea kuandaa kazi nzuri, kwa maslahi ya watoto wa taifa hili,” amesema Usia.
Akizungumzia tuzo hiyo, Masinde, amesema: “Tuzo hii imenipa hamasa kubwa kwa sababu furaha ya Mwandishi wa Habari ni kuona kazi yake inatoa mrejesho chanya kwa jamii yake anayoiandikia.
“Nishukuru UNICEF na TEF kwa kunipa heshima hii na kutambua mchango wa waandishi wa habari za watoto hapa nchini,” amesema Masinde.