26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mhandisi Sanga ambana mkandarasi

Mwandishi Wetu- Simanjiro

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony  Sanga amemtaka mkandarasi Jandu Plumbers wa Arusha anayejenga mradi wa maji wa Orukesment wilayani Simanjiro kuukamilisha ndani ya muda uliyopangwa.

Alitoa maelekezo hayo juzi,alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wilayani Simanjiro sambamba na kuzungumza na mkandarasi.

Akiwa katika ukaguzi wa utekezaji wa mradi, Mhandisi Sanga alibaini shughuli zinazoendelea kutekelezwa na mkandarasi kuegemea zaidi maeneo ambayo hayapelekei wananchi kupata huduma ya maji mapema iwezekanavyo kama ilivyo dhamira ya Serikali.

Alisema mkandarasi anajenga maeneo ambayo siyo kipaumbele cha mradi,hivyo alimtaka kuhakikisha anaelekeza nguvu zaidi ujenzi wa maeneo yatakayowapatia wananchi maji, ikiwamo ujenzi wa chanzo, kituo cha tiba ya maji na bomba kuu la kusafirishia maji.

”Nilichokiona kwenye mradi,mkandarasi amejikita zaidi kujenga majengo ya ofisi na nyumba za wafanyakazi ambayo hayapeleki maji kwa wananchi,badala ya kujielekeza maeneo yenye tija ya kuleta huduma ya maji kwa haraka ili wananchi waanze kunufaika,” alisema Mhandisi Sanga.

Alisema mradi wa maji  mji wa Orukesment, unao umuhimu mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo hasa ikizingatiwa kuwa umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu.

“Wananchi wameusubiri  huu mradi, wamekuwa na shauku kubwa ya kuanza kupata huduma kutoka hapa, sijaridhishwa na huu utaratibu anaoendelea nao Mkandarasi, ningependa kuona matokeo ya haraka kutoka hapa,” alisema.

Akiwasilisha taarifa ya maendeleo  ya ujenzi wa  mradi  huo,Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA), Mhandisi Iddi  Msuya alisema tayari wamemuagiza mkandarasi kuhakikisha anaongeza nguvu kazi ili kutekeleza maeneo nyeti kwa haraka zaidi.

Alisema kukamilika kwa mradi kutanufaisha zaidi ya wakazi 52,000 na mifugo katika mji wa Orkesumet  na vijiji vinavyozunguka mji huo.

Mwakilishi wa Kampuni ya Jandu Plumbers, Mhandisi Kotturu Ramnadh aliahidi kukamilisha ujenzi wa mradi huo katika kipindi kilichowekwa cha mwezi Aprili, 2020.

Mradi wa maji Orukesment unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu kwa nchi za Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa nchi zinazozalisha mafuta (OFID) kupitia mkopo wa masharti nafuu ambao umetengewa jumla ya Dola za Marekani milioni 18.42.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles