27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mhagama atoa wito kujengwa Viwanda vya kutengeneza Virutubishi nchini

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, ameushauri ushirika wa wazalishaji wakubwa wa vyakula nchini kujenga viwanda vya kutengeneza Virutubishi vinavyoongezwa kwenye vyakula badala ya kuviagiza virutubishi hivyo nje ya nchi.

Virutubishi hivyo ni madini ya chuma, Zinki, Asidi ya foliki na Vitamini B 12.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama akipata maelezo ya namna ya Kifaa maalumu cha kuongeza virutubishi kwenye vyakula (dosifier) kinavyofanya kazi wakati alipo tembelea kiwanda cha S.S Bakhresa Plant jijini Dar es Salaam,  lengo likiwa ni kujionea hali ya urutubishaji.

Waziri Mhagama ametoa ushauri huo baada ya kutembelea viwanda vya S.S Bakhresa Plant na Murzah Wilmar complex, jijini Dar es Salaam, lengo likiwa ni kujionea hali ya urutubishaji, ambapo wamiliki hao wa viwanda vya usindikaji wa chakula (Unga wa ngano, unga wa mahindi na mafuta ya kula) wamebainisha kuwa wamekuwa na changamoto ya kupata virutubishi hivyo kwa wakati kutoka nje ya nchi.

“Sisi kama serikali tupo tayari kushirikiana na nyie na tutatengeneza mazingira mazuri ya kuwawezesha kufanya uwekezaji wa viwanda hivyo. Tunaamini virutubishi hivi vikizalishwa hapa nchini gharama mnayotumia kununua virutubishi hivyo itapungua, lakini pia tutakuwa na uhakika zaidi wa aina ya virutubishi tunavyotumia kwenye vyakula vyetu,” amesisitiza Mhagama.

Ameongeza kuwa uanzishwaji wa viwanda hivyo utaongeza ajira kwa Watanzania ambao bado wapo kwenye soko la ajira, pia amebainisha kuwa viwanda hivyo vitapunguza matumizi makubwa ya fedha za kigeni kwa kufanya manunuzi nje na fedha za kigeni zitaongezeka nchini kwa kuwa kuna nchi jirani ambazo wameamza kutekeleza sheria na Programu za kuongeza virutubishi hivyo zitakuja kununua virutubishi hivyo hapa nchini.

“Eneo jingine ambalo tungependa mfikirie ni kutengeneza vifaa vya kurutubisha chakula (dosifier). Mkiweza kuvitengeneza hivi vifaa hapa nchini na mkatumia nyie wenyewe lakini vikatumiwa na wasindikaji wa Kati na wadogo tutakuwa tumetengeneza vizuri mnyororo wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula,” amesisitiza Mhagama.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Viwanda vya S.S Bakhresa, Husein Sufian amefafanua kuwa ujenzi wa viwanda hivyo ni muhimu kwa kuwa kiwanda hicho hutumia gharama kubwa ikiwa ni takribani shilingi bilioni 1.4/=, kwa kila mwaka hutumika kununua virutubishi vya kuongeza kwenye vyakula vinavyozalishwa na kiwanda hicho.

Awali, wakiongea kwa nyakati tofauti  wakati Waziri Mhagama alipokutana na wadau na Taasisi zisizo za serikali zinazojishughulisha na  masuala ya urutubishaji,  kutoka Technoserve Tanzania Meneja Mradi, George Kaishozi, pamoja na Meneja Mradi wa urutubishaji vyakula, Gain Tanzania, Archad Ngemela, wamebainisha kuwa wanaendelea kushirikiana na serikali katika ufuatiliaji wa uhakiki wa udhibiti wa ubora wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi nchini.

Aidha; wamesisitiza kuwa wanaendelea kuwasaidia wasindikaji wadogo kupata   virutubishi na vifaa vya kufanyia urutubishaji pamoja na kuhamasisha wasindikaji hao kuzalisha, kusindika na kuyafikisha kwa walaji mazao yaliyorutubishwa kibaiolijia. 

Mwaka 2011 Viwango na kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula viliandaliwa, ambapo Mwaka 2013, Uongezaji virutubishi ulizinduliwa rasmi hapa nchini. Hadi sasa jumla ya viwanda vikubwa na vya kati 35 vya ngano, mahindi na mafuta ya kula vinaongeza virutubishi kwenye vyakula. Tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 88 ya ngano na asilimia 68 ya mafuta yanayozalishwa na viwanda vikubwa  vinaongezwa virutubiishi ipasavyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles