MGOMBEA URAIS ASHAMBULIWA KWA KISU

0
652


BASILIA, BRAZIL

MGOMBEA wa chama cha mrengo wa kulia katika kinyang’anyiro cha kuwania urais, Jair Bolsonaro, amejeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa kwa kisu wakati alipokuwa akifanya kampeni kusini mashariki mwa Brazil.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, tukio hilo limetokea juzi nchini humo na kuthibitishwa na mtoto wa mwanasiasa huyo, Flavio Bolsonaro, ambaye alisema  kuwa, baba yake, mwenye umri wa miaka 63 amepata majeraha katika ini, mapafu na tumboni na kupoteza damu nyingi.

Baada ya tukio hilo, Bolsonaro alikimbizwa hospitali ya jirani iliyoko mji wa Juiz de Fora katika Jimbo la Minas Gerais, nchini humo kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa dharura na inaripotiwa kuwa upasuaji umekuwa na mafanikio.

Msemaji wa polisi nchini humo amelieleza shirika hilo kuwa mtu mmoja mwanamume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 ametiwa mbaroni akihusishwa na shambulizi hilo na taarifa zaidi zinasema mshukiwa alikuwa na kisu.

Wakati huo huo, rais wa zamani wa nchi hiyo, Luiz Inacio Lula da Silva, amezuiwa na mahakama kuwania nafasi hiyo ya urais katika uchaguzi wa Oktoba 7, mwaka huu.

Utafiti wa maoni wa hivi karibuni unaonesha Bolsonaro anaongoza kwa asilimia 22 kulinganisha na wagombea wengine wawili kwenye kinyang’anyiro hicho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here