Derick Milton, Bariadi
MGOMBEA ubunge jimbo la Bariadi Mkoani Simiyu, kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Mhandisi Andrew Kundo amehaidi kurejesha shamba la kijiji cha Mwahalaja Kata ya Ikungu-Lyabashashi Jimboni humo ambalo limepolwa kwa muda mrefu na baadhi ya watu kinyume na utaratibu.
Mhandisi Kundo amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, kazi yake ya kwanza kwa wananchi wa kijiji hicho ni kuhakikisha anarudisha shamba hilo ambalo ni zaidi ya hekari 50 na ni mali yao halali.
Mgombe huyo ametoa ahadi hiyo leo mbele ya umati wa wananchi wa kijiji hicho, waliofika kwenye mkutano wa hadhara wa kampeini za mgombea huyo ambazo zinaendelea katika maeneo mbalimbali ya jimbo humo.
Amesema kuwa anatambua kuwa viongozi wa kijiji hicho wameangaika kwa muda mrefu kulipata shamba hilo, lakini imeshindikana ambapo aliwaomba kura wananchi hao ili aweze kupambana kurejeshwa kwa shamba lao.
Ameongeza kuwa shamba hilo ambalo lilikuwa mali ya kijiji hicho, lilichukuliwa kinyemela na baadhi ya watu, hivyo linatakiwa kurejeshwa kwao kwa ajili ya kukiletea maendeleo kijiji hicho.
“Nimeambiwa hapa shamba la kijiji limechukuliwa muda mrefu, nitakapokuwa mbunge kazi yangu ya kwanza itakuwa kuhakikisha shamba hilo linarejea kwenu, maana viongozi wamehangaika sana kulipata lakini wameshindwa, Mimi nitaenda kulirejesha shamba hilo,” Alisema Mhandisi Kundo.