Mwandishi Wetu
MASHAMBULIO mawili yaliyofanywa ndani ya wiki hii na Iran katika kambi mbili za jeshi la Marekani nchini Iraq msingi wake ukiwa ni kisasi baada ya Marekani kwa amri ya rais wake Donald Trump kumuua kiongozi wa Kijeshi wa Iran, Qasem Soleimani yamesababisha mafuta ghafi kupanda bei.
Taarifa kutoka katika vyombo vya habari vya kimataifa zilizoripotiwa katikati ya wiki hii zilieleza kuwa gharama za mafuta ghafi zimepanda kwa 1.4% kwa dola 69.21 za Marekani kwa pipa moja.
Kupanda huko kwa bei ya mafuta ni wazi hakuathiri nchi hizo mbili tu zinazogombana bali dunia nzima hasa kwa kuzingatia kwamba Iran na mataifa ya karibu inayopakana nayo ndiyo yanayoongoza kwa kuuza mafuta duniani.
Nchi nyingi duniani, Tanzania ikiwa ni miongoni mwake inategemea nishati hiyo kutoka katika mataifa hayo hivyo unapotokea mgogoro wowote haiyukini lazima ututie hofu sisi wote.
Kwa sababu nchi hizo nyingi zinazopakana na Iran bado zinasalia kuwa chanzo kikubwa cha upatikanaji wa nishati ya mafuta na migogoro inavyozidi kupanuka huwa ni hatari zaidi yatupasa kujiandaa kuchukua tahadhali kila mara hasa ya kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta.
Tayari mgogoro huo wa Marekani na Iran umeelezwa unaweza kuathiri usafirishaji wa mafuta kupitia lango la Hormuz linalotenganisha ghuba ya uajemi na ghuba ya Oman.
Takwimu zinaonyesha takribani moja ya tano ya mafuta duniani husafirishwa kupitia lango hilo linalounganisha eneo la ghuba na bahari ya Arabia.
Taarifa zinaeleza kuwa Mlango wa Hormuz ni muhimu kwa wasafirishaji wakubwa wa mafuta katika eneo la ghuba – Saudi Arabia, Iraq, Umoja wa falme za kiarabu na Kuwait- ambao uchumi wao unajengwa kutokana na uzalishaji wa mafuta na gesi.
Iran pia inategemea kwa kiasi kikubwa njia hiyo kwa ajili ya kusafirisha mafuta.
Qatar ambaye naye ni mzalishaji mkubwa duniani wa gesi, husafirisha karibu gesi yake yote kupitia lango hilo.
Kutokana na hayo ndio maana sisi tunasisitiza ni vyema kila mara tukajipanga kuhusu suala la nishati hiyo ili kukabiliana na hali yeyote mbeleni kwa kuwa na akiba kubwa na ya kutosha.
Tunaamini hatuwezi kuzifikia nchi nyingine kubwa duniani ambazo zimejiwekea akiba kubwa kutokana na hali yao ya uchumi kuruhusu, lakini bado yatupasa kuwa na jicho linalofanana na hilo.
Tunasema hivyo kwa sababu ikitokea hatukujipanga vizuri kukabiliana na hali hiyo, huko mbele tunaweza kujikuta katika wakati mgumu zaidi kiuchumi iwapo mgogoro huo utatanuka zaidi.