30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

MGODI GGM WADAIWA SH BILIONI 24 ZA USHURU

Na HARRIETH MANDARI


HALMASHAURI ya Mji wa Geita inaudai Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM)   Sh bilioni 24.6   za   ushuru wa huduma ambazo   mgodi huo ulitakiwa kuzilipa katika   miaka tisa kutoka mwaka 2004 hadi 2014.

Hata hivyo GGM imepinga madai hayo ikisema  sheria ya kodi ya huduma ilitungwa mwaka 2004 kuanza kutumika mwaka 2005.

Mgodi huo ulisema  ulitakiwa kulipa   dola za Marekani 200,000 na baadaye mwaka 2014 sheria ilibadilishwa na   kutakiwa kuanza kulipia asilimia 0.3 ya mapato yao ya mwaka hivyo kudai siyo sahihi kudaiwa kiasi hicho cha fedha.

Tayari Halmashauri hiyo ya Mji wa Geita imekwisha kuwasilisha hati ya madai kwa mgodi huo na kutoa siku 30 kulipwa  dola za Marekani milioni 11.04  (Sh bilioni 24.6) zikiwa ni malipo ya tozo ya ushuru wa huduma.

Suala hilo  hilo liliibuliwa na madiwani  katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Geita, baada ya Mwakilishi wa GGM, Joseph Mangilima kuomba ufafanuzi kwa kamati ya kudumu ya fedha na uongozi juu ya deni hilo.

Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Queen Luvanda alisema deni hilo lilitokana na taarifa iliyotolewa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA)  baada ya kufanya ukaguzi katika mgodi huo mwaka 2016.

Alsema ukaguzi huo uliaini deni hilo ambalo inadaiwa mgodi huo uligoma kulilipa kwa kigezo kuwa halmashauri haikuwa na sheria ndogo ya kudai kodi hiyo.

Akizungumza jana na MTANZANIA kwa   simu, Meneja Uhusiano   wa GGM,    Mangilima,  alikiri alihoji jambo hilo katika kikao hicho akitaka kupata ufafanuzi.

“Nilikuwapo jana (juzi) kwenye kikao cha baraza na nikasikia deni hilo, walieleza kuwa GGM inadaiwa   dola za Marekani milioni 11 na nilipowauliza walisema limelipata kwa TMAA.

“Niliwashauri kukutana na uongozi wa mgodi na kujadiliana kwa kuwa sheria ya kodi ya huduma ilitungwa mwaka 2004 kuanza utekelezaji wake 2005,” alisema.

Alisema   sheria hiyo  a ilianza kutumika mwaka 2005 ambako walikuwa wakilipa   dola za Marekani 200,000 kama maelekezo ya sheria mpaka mwaka 2014 baada ya sheria kubadilika na kutakiwa kulipa asilimia 0.3 ya mapato ya mwaka ikitegemeana na uzalishaji wao.

“Tumekuwa tukilipa mpaka leo, sasa wao kuibua hoja kuwa wanatudai Sh bilioni 24 nadhani siyo sahihi.

“Hata kama tungekuwa hatujalipa kabisa kwa mujibu wa sheria hiyo kama wanavyodai, basi deni letu la ya ushuru wa huduma lingekuwa ni Dola za Marekani milioni 2.7 na siyo dola milioni 11,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles