26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

MGODI BUZWAGI WAPUNGUZA WAFANYAKAZI 200

 Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


KAMPUNI ya Acacia imepunguza wafanyakazi wake 200 katika Mgodi wa Buzwagi, uliopo Kahama, Shinyanga.

Katika idadi ya wafanyakazi hao, 100 ni kutoka katika Idara ya Ulinzi, ambao wameondolewa na badala yake kampuni imeuza tenda na kutoa mkataba kwa Kampuni ya Ulinzi ya G4S.

Mbali na hilo, pia shughuli mbalimbali za mgodi zilizokuwa zikifanywa na wafanyakazi waliokuwa kwenye mikataba zimehamishiwa kwa kampuni binafsi kama njia ya kuongeza ufanisi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi ndani ya mgodi huo wa kampuni hiyo ya ulinzi waliokuwa wameajiriwa na Acacia, kibarua chao kimekwisha rasmi.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa, Acacia itawajibika kuwalipa wafanyakazi hao, lakini wale wa ulinzi endapo watataka kuendelea wametakiwa kuandika tena maombi na kutuma kwenye kampuni mpya iliyopewa tenda ya G4S.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Mgodi wa Buzwagi,  Blandina Munghezi, suala hilo lipo na wala si jambo jipya.

“Hilo suala mbona limeshafanyika tangu wiki iliyopita, lakini kazi za hao si kama tumeajiri wengine, bali sisi tumegawa tenda katika kampuni ambayo itatufanyia kazi,” alisema Blandina.

Suala hilo limekuja ikiwa ni  siku chache tangu Rais Dk. John Magufuli kutoa katazo la usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makinikia) kwa Kampuni ya Acacia na kampuni husika ilieleza wazi kabisa namna katazo hilo lilivyoathiri biashara yao na hasara wanayoendelea kuipata kila siku.

Mgodi wa Buzwagi, unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia, utamaliza rasmi shughuli zake za uchimbaji wa madini  Desemba, mwaka huu, lakini shughuli za uzalishaji zitakwisha rasmi mwaka 2020.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa, Mgodi wa Bulyanhulu, unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia pia, na wenyewe upo mbioni kuanza kupunguza wafanyakazi.

Mwishoni mwa wiki, Kampuni ya Acacia ilitoa taarifa kuwa Kampuni ya Bulyanhulu Gold Mine (BGM) na Pangea Mineral Limited (PML) zimeshatoa notisi ya usuluhishi, kufuatia uzuiwaji wa usafirishaji wa mchanga wa madini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles