25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, January 29, 2022

MGEJA AMSHANGAA DK. MAGUFULI

Na MWANDISHI WETU- NZEGA


MWENYEKITI wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation inayoshughulikia utawala bora na haki, Khamis Mgeja, amemshangaa Rais Dk. John Magufuli kwa kutoshiriki kuaga miili ya askari polisi waliouawa na majambazi, Kibiti mkoani Pwani wiki iliyopita.

Amesema kama Rais Magufuli angeshiriki kuaga miili hiyo akiwa na askari polisi na familia za marehemu, angeonyesha ni kwa jinsi gani alivyoguswa na mauaji hayo ya kikatili.

Mgeja aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora akiwa njiani kuelekea Shinyanga.

“Pamoja na kwamba siku miili hiyo ilipokuwa ikiagwa Rais alikuwa kwenye ufunguzi wa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa makazi ya wananchi pale Magomeni, Dar es Salaam, ukweli utabaki palepale, kwamba alitakiwa kuahirisha shughuli hizo ili akashiriki kuaga miili ya Watanzania hao.

“Washauri wake wangemshauri juu ya hilo kwani uzito wa tukio la kuuawa kwa askari wetu, ulikuwa wa aina yake na hauwezi kulinganishwa na tukio la kufungua hosteli na nyumba za makazi.

“Kwa hiyo, naamini siku hiyo Rais angetumia busara tu kuhairisha shughuli nyingine ili akawaage askari hao kwa sababu waliuawa wakati wakitimiza majukumu yao ya ujenzi wa taifa na kulinda raia na mali zao.

“Nasema hivyo kwa sababu Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kutwambia kwamba kupanga ni kuchagua, kwa hiyo, siku hiyo Rais alitakiwa kwenda kuaga miili hiyo kwa sababu ya umuhimu wa tukio lenyewe.

“Pamoja na Rais kutoshiriki tukio hilo, viongozi wengi wa Serikali hawakuwapo kwani walikuwa wamekwenda kushiriki matukio ya rais,” alisema Mgeja.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, aliongoza waombolezaji kuaga miili ya askari hao.

Wiki iliyopita, watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, waliwaua kwa risasi askari wanane mkoani Pwani walipokuwa wakitoka kufanya doria.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
177,227FollowersFollow
532,000SubscribersSubscribe

Latest Articles