24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Mganga Mkuu Dar ataka wananchi wasibweteke mapambano ya corona

Aveline Kitomary, Dar es salaam

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume, ametoa wito kwa wananchi hususani wa Jiji la Dar es Salaam, kutobwete badala yake waendelea kuchukua tahadhari ili kujikinga na virusi vya corona. 

Dk  Mfaume alitoa wito huo jana, wakati akipokea msaada wa barakoa 17,500 na vipukusi (sanitizers) lita 700 -kutoka kwa Shirika lisilo la kiserikali la Medipeace linalohusika na mradi wa mama na mtoto katika Mkoa wa Dar es Salaam. 

“Licha ya elimu tunayoendelea kutoa juu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya corona, tunawahamasisha wananchi wasibweteke katika kipindi hiki, ili kuumaliza kabisa ugonjwa huu katika nchi yetu na hili linawezekana kabisa,” alisema Dk Mfaume. 

Alisema msaada uliotolewa utaelekezwa katika vituo vya vya Sinza Hospitali, Vijibweni Hospitali, Rangi Tatu Hospitali, Kituo cha afya Kimara, Kituo cha afya Tandale, Kituo cha afya Mbezi, Kituo cha afya Round table, Kituo cha afya Kimbiji, Kituo cha afya Buguruni, Tegeta Dispensari, Bunju Dispensari.

Alisema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za Afya, hususan katika Jiji la Dar es Salaam baada ya Serikali kuziteua baadhi ya hospitali kuwa vituo vya kutolea huduma kwa wagonjwa wa Covid-19, hivyo kuelekezwa msaada huo katika vituo vya afya kutasaidia mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya corona. 

“Sasa hivi tumeona wagonjwa wameongezeka sana katika vituo vya kutolea huduma za afya, mfano katika Mkoa wa Dar es Salaam baada ya Serikali kuitangaza Hospitali ya Amana kuwa kituo cha kuhudumia wagonjwa wa COVID-19, wagonjwa wengi wamekuwa wakienda katika vituo vingine, hivo msaada huu utasaidia sana kupambana dhidi ya maambukizi mapya,” alisema. 

Dk  Mfaume aliwataka wadau wengine kutoka mashirika mbalimbali nchini kuendelea kuisaidia Serikali vifaa kinga dhidi ya corona ili kuvisaidia vituo vya kutolea huduma za afya viweze kujitosheleza mahitaji hayo, hasa kutokana na vituo vya afya kuwa sehemu inayopokea watu tofauti kwa wingi. 

Hata hivyo alisema hali ya afya katika Mkoa wa Dar es Salaam ni shwari, huku akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuchukua tahadhari za karibu dhidi ya maambukizi hayo ili kuumaliza kabisa ugonjwa huo nchini. 

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Medipeace Tanzania  Sukyung Kim, alisema shirika hilo linalofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea ya Kusini (Koica), limekuwa likishirikiana na Wizara ya Afya na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika Mkoa wa Dar es salaam.

Alisema kutokana na mlipuko wa corona, shirika hilo linaunga mkono juhudi za Serikali za kupambana corona kwa kutoa vifaa kinga ambavyo vitasaidia watoa huduma za afya na wagonjwa wataofika kupata matibabu katika vituo hivyo. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,310FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles